09 September 2011

Tibaijuka atangaza vita kwa wavamizi wa ardhi

*Asema itaanzia jijini Dar es Salaam

Na Gladness Mboma

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ametangaza hali ya hatari kwa wezi na wavamizi wa ardhi nchi nzima kuanzia
Jiji la Dar es Saalam.

Waziri huyo pia ameenda mbali zaidi na kuzionya halmashauri zote akisema ndizo chanzo cha migogoro ya ardhi.

Mbali na kauli hiyo alisema kuwa wale waliodhani kuwa amesinzia bado yuko macho na kwamba maofisa wa ardhi watakaothibitika hawafuatii maadili ya kazi zao watafukuzwa kazi.

Prof. Tibaijuka aliyasema hayo jana Dar es Salaam wakati alipokuwa akizungumzia operesheni ya kurejesha utaratibu katika masuala ya ardhi mijini nchi nzima.

"Tutarejesha hali ya usalama katika miji yetu maeneo mengi katika majiji  yetu yamevamiwa ripoti ya Bw. William Lukuvi wakati alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaa inaonesha hali halisi ya uvamizi wa maeneo mbalimbali Dar es Salaam. Wale waliodhani kuwa nilikuwa nimesinzia nawataarifu kwamba sijasinzia bado niko macho watu waliovamia maeneo hayo ninawafahamu na hayo maeneo ninayafahamu yapo wapi,"alisema.

Alisema watu hawaruhusiwi kufanya maendeleo yoyote katika maeneo ya mijini bila kibali cha maandishi kutoka kwenye mamlaka za upangaji, ambazo ni halmashauri za jiji, manispaa, miji na wilaya nchini ya usimamizi wa wizara husika.

"Tumekuwa na migogoro mingi ya ardhi katika operesheni hii kuna halmashauri zitanyang'anywa madaraka maana imeonekana baadhi yao wamekuwa chanzo cha migogoro hiyo na wizara kutupiwa lawama,"alisisitiza.

Alisema kuwa mtu atakayejiusisha kupata hati kinyume na sheria atakuwa amepoteza haki yake na kuwataka wananchi kuwa macho na utapeli huo ambao umeenea maeneo mbalimbali nchini.

Prof. Tibaijuka alisema mtu asifikirie kuwa atapata hati ya kiujanjaujanja, kwani hati ya kwanza ndiyo itatawala na ramani na kusisitiza kuwa hatatishika na mtu ambaye ataona hakuridhika ruksa kwenda mahakamani.

Alisema mtu anayetaka kubadilisha matumizi ya ardhi kuna taratibu zinazotakiwa kufuatwa na siyo kufanyika kiholela  bali kwa sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa.

"Tabia ya ujanja ujanja  katika kutafuta viwanja mijini kwa operesheni hii haitapata nafasi na hati zote feki zitaishia mezani mwangu,"alisema

Alisema mpaka sasa wamekwishafuta hati feki 12 za viwanja vya mabwawa Mikocheni na hati 30 Mbezi Beach na kusisitiza kwamba mtu ambaye anafikiria kwamba ataishi kwa ujanja itakuwa ngumu.

Prof. Tibaijuka alisema kuwa ngazi za chini kama kata, mitaa na halmashauri ndio chanzo cha migogoro, hivyo wasipofuata taratibu wanababisha wizara hiyo kuonekana ina migogoro.

Alisema mabadiliko yote ya ardhi ambayo yamefanyika bila kufuata utaratibu ni batili na yanatakiwa yaondolewe mara moja, ambapo aliwataka wananchi kuwa macho wasitapeliwe na maofisa wasio waadilifu.

"Chini ya kamati iliyoundwa na Bw. Lukuvi maeneo ya wazi yapatayo 153 yaliyopo katika Halmashauri za Manispaa zote tatu za Mkoa wa Dar es Salaam yalichunguzwa,"alisema.

Alisema katika uchunguzi huo ilibainika kwamba maeneo 88 sawa na asilimi 80 kati ya maeneo 110 ya wazi yaliyopo katika manispaa ya Kinondoni yamevamiwa, ambapo manispaa ya Ilala maeneo yaliyokaguliwa ya wazi yalikuwa 30, kati ya hayo maeneo 11 yamevamiwa, hiyo ni sawa na asilimia 37 ya maeneo yote yaliyokaguliwa na kamati.

Prof. Tibaijuka alisema kwa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, imeonekana kuwa na asilimia ndogo ya uvamizi, ambapo yalibaikina maeneo matano sawa na asilimi 30 ya maeneo ya wazi yaliyotembelewa ambayo ni 14.

Alisema kuwa wale wananchi wenye mashamba na kisha wanashindwa kuyaendeleza watanyang'anywa, ambapo aliwataka wale wa vijijini ambao wanakodisha mashamba kuacha mara moja na badala yake mashamba hayo wayatumie wenyewe wakishindwa wamrudishie Rais.

1 comment:

  1. Mh. Waziri,Tibaijuka, hao maofisa wako wa Kinondoni na kwingineko wamekushinda???. Kila kukicha migogoro inaendelea kuongezeka, na wao wapo. Kwa nini wasindolewe wapishe watu/vijana wasomi mbona wapo wengi tu. Siamini kama wao ni muhimu sana kuwepo kuliko watu wengine.
    Tunakuomba chukua hatua kali zaidi. You are the change we were waiting for. Please, make positive changes thereof.

    ReplyDelete