23 September 2011

Tamasha la Bia kufanyika Oktoba

Na Zahoro Mlanzi

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Kilimanjaro Lager ikishirikiana na Kampuni za Bongo 5, Alliance Francaise na Taasisi ya Goethe, zimeandaa tamasha la
bia litakaloshirikisha wasanii mbalimbali litakalofanyika Viwanja vya Leaders, Dar es Salaam Oktoba Mosi na 2, mwaka huu.

Tamasha hilo ni la kwanza kufanyika nchini, litajulikana Kilimanjaro Beer Festival likiwa na lengo la kusherehekea miaka 50 ya Uhuru, ambapo kampuni hiyo imedhamini kwa zaidi ya sh. milioni 25.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Meneja wa bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema tamasha hilo litapambwa na burudani wakiwemo wasanii wa ndani na nje ya nchi, bendi kongwe nchini Msondo Ngoma na Sikinde na michezo mbalimbali, ambapo baadaye zitatolewa zawadi kwa washindi.

"Alisema tamasha hilo litafanyika kwa siku mbili mfululizo ambapo watu watapata burudani zote na hakutakuwa na mapumziko mpaka tamasha litakapokwisha, kwa hiyo mtu akiingia Leaders akiamua anaweza kubaki mpaka siku inayofuata kwani huduma zote zitakuwepo.

"Kwa nchi za wenzetu huwa na festival sesion, ambapo hufanya kwa wiki mbili mfululizo bila watu kwenda kazini, lakini hapa kwetu bado na ndiyo maana tumeona tuifanye kwa siku mbili," alisema.

Alisema miongoni mwa waalikwa ni wasanii mbalimbali wa filamu nchini, ambapo watajichanganya na watu wengine kubadilishana mawazo ambapo ulinzi utakuwepo wa kutosha kwa kuhakikisha kila mmoja anaondoka salama.

Aliwaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi siku hiyo, kwani tiketi zitauzwa kwa sh. 10,000 kwa siku mbili na mtu akinunua kwa siku moja kila moja itakuwa ni sh. 7,000.

Naye Mkurugenzi wa Matukio wa Bongo 5, Olive Nimaga aliushukuru uongozi wa TBL kwa kuwawezesha kufanikisha tamasha hilo na ana imani litakuwa la aina yake, kwani kitu kama hicho hakijawahi kutokea.

No comments:

Post a Comment