27 September 2011

Kikongwe jela kwa kugushi hati, udanganyifu

Na Rehema Maigala

MKAZI wa Mbezi Kimara Manispaa ya Kinondoni Dar es Salaam Bi.Judithi Ndimbo (70) amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa kosa la kujipatia fedha kwa
njia ya udanganyifu na kugushi hati ya kiwanja.

Hukumu hiyo ilisomwa na Hakimu Bw. Kwey Rusemwa, wa mahakama ya Kinondoni huku  akipitia ushahidi uliotolewa na pande zote mbili kabla ya kuusoma.

Hata hivyo kabla ya kuanza kusoma hukumu hiyo Hakimu Rusemwa alimuuliza Mwendesha Mashitaka Bw. Benedict Nyagabona, kama ana kumbukumbu yeyote ya mashitaka inayomuhusu mshitakiwa huyo.

Bw.Nyagabona alijibu hana kumbukumbu yeyote ya mashitaka inayomuhusu mshitakiwa huyo kwa muda huo.

Mahakama ilimpa nafasi mshitakiwa kujitetea kabla ya ya kutamka adhabu kulingana na kosa lake alilolifanya.

Mshitakiwa alidai kuwa anaomba kupunguziwa adhabu kwa kuwa umri wake ni mkubwa.

"Baba yangu Hakimu naomba unipunguzie adhabu mjukuu wangu hebu, niangalie mwenzako ni shetani na vishawishi ndivyo vilinifanya mpaka leo hii niwe hapa.

Miguu inanisumbua kila wakati pia ninategemewa na wajukuu zangu ambao hawana wazazi,"alisema mshitakiwa huyo huku akitiririkwa na machozi.

Baada ya maombi hayo Hakimu Rusemwa alijibu kuwa kutokana na umri wake kuwa mkubwa atampunguzia adhabu lakini akiletwa tena kwa kosa kama lile atampa adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wenye tabia kama hiyo.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mshitakiwa na wenzake ambao hawajawahi kufikishwa Mahakamani hapo waligushi hati ya kiwanja kilichopo Kimara block 18 na kuweka jina lake kitu ambacho si kweli.

Katika shitaka la pili mshitakiwa  huyo  akishirikiana na wenzake walijipatia pesa taslimu sh.40,000,000 mali ya mlalamikaji Bi. Irene Lyimo.

No comments:

Post a Comment