Na Mwandishi Wetu
PAMBANO la mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Equatorial Guinea na Gabon kati ya
Tanzania 'Taifa Stars' na Algeria 'Desert Warriors' limeingiza sh.148,220,000.
Mechi hiyo ilichezwa Septemba 3 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura fedha hizo zimepatikana kutokana na mashabiki 29,892 kuingia kushuhudia mechi hiyo.
Alisema mashabiki 17,650 walikata tiketi kwenye viti vya kijani ambavyo kiingilio kilikuwa sh. 3,000.
"Sehemu ya viti hivyo ndivyo vilivyovutia mashabiki wengi zaidi ikiwa ni zaidi ya nusu ya mashabiki wote walionunua tiketi kwa ajili ya viti hivyo," alisema.
Alisema VIP A ambapo ndipo kulikokuwa na kiingilio cha juu cha sh. 30,000, jumla ya mashabiki 394 walinunua tiketi kwa ajili ya eneo hilo.
Wambura alisema eneo la viti vya bluu ambapo kiingilio kilikuwa sh. 5,000, mashabiki walionunua tiketi walikuwa ni 8,166.
Alisema viingilio vingine katika pambano hilo vilikuwa sh. 7,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 VIP C na sh. 20,000 VIP B.
No comments:
Post a Comment