27 July 2012

Sheria mifuko ya hifadhi sasa mwiba mkali



Na Benedict Kaguo, Dodoma

MBUNGE wa Mwibara, mkoani Mara, Bw. Kangi Lugola (CCM), amewalipua wabunge waliopitisha sheria kandamizi ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na kurejea kauli yake kuwa, chombo hicho hakiko makini kwenye kutunga na kupitisha sheria.

Bw. Lugola alitoa tuhuma hizo bungeni mjini Dodoma jana baada ya kuomba mwongozo wa Spika kutokana na hatua ya Mbunge wa Kisarawe, Bw. Suleiman Jaffo (CCM), kuomba mwongozo wa kulitaka Bunge lisitishe shughuli zake za jana ili kujadili hoja ya dharura ya malalamiko makubwa yanayotolewa na wananchi
kuhusu sheria hiyo.

Baada ya kuruhusiwa kuzungumza, Bw. Jaffo alisema sheria hiyo ni kandamizi ambapo mfanyakazi hawezi kupata mafao yake hadi afikishe umri wa miaka 55 hadi 60.

Alisema yapo malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi wa sekta mbalimbali hivyo kulitaka Bunge liahirishe shughuli za siku hiyo na kujadili kwa dharura hoja hiyo.

Aliongeza kuwa tangu jana (juzi), kuna tatizo la wanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), na Mfuko wa Pensheni ya Mashirika ya Umma (PPF), kutofahamika sheria hiyo hivyo kuzidisha malalamiko ambapo Mwenyekiti wa Bunge Bi. Jenister Mhagama, alikiri hoja hiyo ni ya muhimu, nzito na kumtaka Bw. Jaffo kuitafutia taarifa zaidi kujua wafanyakazi wanalalamikia eneo gani ili Bunge liweze kujua namna ya kusaidia.

Hata hivyo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini Bw.  Zitto Kabwe na Mbunge wa Singida Mashariki, Bw. Tundu Lissu (wote CHADEMA), walitaka iitishwe kamati ya uongozi ya Bunge ili  kujadili jambo hilo lenye madhara makubwa kwa wafanyakazi.

Kutokana na hali hiyo, Bw. Lugola aliomba mwongozo na kueleza kuwa, suala hilo ni la kisheria na Bunge limehusika kuitunga sasa wabunge wanapolalamikia sheria hiyo ni wazi kuwa Bunge haliko makini kwenye kutunga na kupitisha sheria zake.

Bw. Lugola aliyasema hayo siku chache tangu anukuliwe na gazeti hili akijutia ubunge wake na kudai kuwa, Bunge ambalo ni chombo muhimu cha kuisimamia Serikali, linaonesha kupoteza mwelekeo, kwenda kinyume na matarajio ya wananchi wengi.

Katika gazeti hilo, Bw. Lugola alisema inasikitisha kuona mambo mengi yakijadiliwa bungeni yanahusisha itikadi za vyama badala ya kuisimamia na kuishauri Serikali.

“Nasikitishwa na mwenendo wa Bunge kutawaliwa na unafiki pamoja na woga hasa katika masuala muhimu yanayohusu mustakabali wa nchi,” alisema Bw. Lugola katika gazeti hilo.

Akizungumza bungeni jana, alirejea kauli yake ya kulishangaa Bunge kupitisha sheria hiyo ambayo imeonekana mwiba kwa wanachama wa mifuko hiyo.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni suala la kisheria...Bunge haliko makini kwenye kutunga sheria...naomba mwongozo wako kama ni halali Bunge hili kuileta hoja hiyo kama jambo la dharura wakati sheria imepishwa humu ndani Juni mwaka huu,” alisema Bw. Lugola na kupata upinzani mkubwa kutoka kwa wabunge.

Baada ya malumbano makubwa, Bi. Mhagama aliagiza Kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge ikutane ili kulijadili suala hilo kuona ni namna gani Bunge linaweza kusaidia na kuifanyia marekebisho.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Kitengo cha Mawasiliano na Uhamasishaji, ilisema marekebisho kuhusu kusitisha fao la kujitoa, yamefanyika ili

Imesema Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Sheria ya Mamlaka, zimefanyiwa marekebisho ambapo mchakato wake, ulihusisha wadau kwa kuzingatia utatu yaani wawakilishi kutoka Vyama vya Wafanyakazi, Chama cha Waajiri na Serikali.

Ilisema kwa kutambua tofauti ya ajira, mazingira ya kazi, sababu za ukomo wa ajira na umuhimu wa mwanachama kunufaika na michango yake wakati akiwa kwenye ajira, mamlaka itaendelea na mchakato wa kuandaa miongozo na kanuni za mafao.

Lengo ni kuboresha masilahi ya wanachama ambapo miongozo na kanuni hizo, zitajadiliwa na wadau wakiwemo wafanyakazi, waajiri na Serikali kabla ya kuanza kutumika.

“Kutokana na kuanza kutumika sheria hii, maombi mapya ya kujitoa yamesitishwa kwa kipindi cha miezi sita hadi miongozo itakapotolewa ili kuiwezesha Mamlaka na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoa elimu kwa wadau.

“Tangazo hili halitawahusu wanachama waliojitoa kabla ya Julai 20 mwaka huu na mamlaka inakanusha vikali kwamba, sitisho la fao la kujitoa si kwa sababu ya Serikali au mifuko kufilisika,” imesema taarifa hiyo na kuongeza kuwa, mifuko yote ipo thabiti na michango yote ya wanachama ipo salama.

Mamlaka imewaomba wanachama na wadau wote wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii, kuwa na utulivu wakati mchakato huu ukiendelea ili kulinda na kutetea masilahi ya mwanachama.

6 comments:

  1. huu ni unafiki, tume iliyoandaliwa kwa ajili ya kuregulate mifuko hii iko wapi? tumeingilia mambo mengine ambayo tume yenyewe haikutumwa.kwa nini watu wengine wanastaafu na mamilioni na wengine mamia ndiyo ilikuwa hoja, sasa hoja hizi wa miaka 55 na 60 bunge limezitoa wapi? msitufanye kichwa vya wendawazimu ili tusahau mada hapa. serikali itoe maamuzi juu ya hoja mama na sio kuibua malumbano ambayo yanataka kutusahaulisha lengo kuu. Tanzania yetu haina mwelekeo wa matukio yake, kila kunapokucha tume zinaanzishwa ambazo lengo lake ni kula pesa za vikao tuuuuu. bushit

    ReplyDelete
  2. hivi huyu mbunge wa mwibara alikuwepo bungeni kipindi hicho cha kupitisha sheria au ni miongoni mwa wale waliokuwa akitafuta ngawira kwenye halmashauri zao wakati bunge likiendelea na vikao vyake. Km alikuwepo haoni na yeye ni kapuku asiyefaa hapo mjengoni? Bunge likishapitisha sheria yeyote haijalishi ulikuwepo au la, kwa maana hiyo anataka kujinasua ktka lawama hizo kuwa yeye hakuwepo? Huyu ni kati ya wale wenye nywele lakini hawana akili. asituzuge kuwa yeye ni safi, mwizi tena fisadi mkubwa.apeleke ukurya wake na unafiki wake huko. tena itakuwa mara yake ya mwisho kuwa hapo bungeni kwani sisi tumeshachoshwa na mambo anayoyafanya hapo mjengoni. Kitambi kikubwa kama cha tembo utadhania ndicho tulichomtuma kukinenepesha?

    ReplyDelete
  3. UKISTAAJABU YA MUSSA UTAYAONA YA FILAUNI

    ReplyDelete
  4. UKO USEMI KUWA TULIDANDIA DEMOKRASIA YA VYAMA VINGI BILA MAANDALIZI KAMA SHERIA ILITUNGWA NA HILI BUNGE LA TAARIFA NA MIONGOZO KWA WENYE AKILI HILI NI BUNGE LA MAKABWELA "HOUSE OF COMMONS" JE MABUNGE MENGINE MAWILI YAKO WAPI? "HOUSE OF SENATES" NA "HOUSE OF LORDS" HIVI MUNATEGEMEA BUNGE LA MAKABWELA[HOUSE OF COMMONS]MAARUFU SIKU HIZI KAMA BUNGE LA TAARIFA NA MIONGOZO LITATUNGA SHERIA YENYE TIJA ??

    ReplyDelete
  5. uozo huu uliofanywa na bunge letu pamoja na serikali yake kuuona kwamba unafaa ni dalili tosha kabisa kwamba serikali haiwajali wananchi wake na haiko tayari kuwatetea au kulinda maslahi yao, na badala yake kuwaibia wafanyakazi kuanzia tozo kubwa la Pay as you earn hadi kufikia kukandamiza hata mafao yao kama walivyojipangia ilimradi tuu wale washibe kwa jasho la wengine.

    ReplyDelete
  6. Tunapofika kuomba kura tunapiga hadi magoti sasa ni wakati wa kuonesha kama kweli ulikuwa unamainishi kuwasaidia wananchi au tumbo lako tuna wabunge wazuri kuhoja lakn kama mlipokuwa mkidai posho zenu mdai na hili mana kuwa chagua tunakesha usiku hatulali

    ReplyDelete