Na Reuben Kagaruki
RAIS Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, amezitaka taasisi, mashirika na serikali yenyewe kusaidia Vijiji vya SOS ili viendelee kutimiza azima yake ya
kusaidia watoto waliopoteza wazazi na wale wanaotoka kwenye familia masikini.
Mzee Mwinyi alitoa kauli hiyo Dar es Salaam juzi, wakati wa hafla ya kutunukiwa tuzo ya kuwa balozi wa heshima wa Vijiji vya SOS Tanzania Bara na Zanzibar.
Alitunukiwa tuzo hiyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 40 ya Vijiji vya SOS tangu kuanzishwa barani Afrika.
"Nawashukuru kwa kazi nzuri inayofanywa na SOS kwa kuwapa watoto msaada, wamejengewa makazi, mnawapa msaada na kuwasomesha kuanzia madarasa ya awali hadi vyuo vikuu,"alisema Mzee Mwinyi.
Kutokana na kazi hiyo nzuri inayofanya Mzee Mwinyi alitoa mwito kwa taasisi, wadau na hata serikali yenyewe isaidie watu wanaojitokeza kusaidia Watanzania wenye matatizo.
"Bila wao (SOS) watoto wengi wangekuwa barabara wakikwapua vitu...kule Zanzibar wengine wamepata kazi baada ya kuhitimu vyuo vikuu na wamekuwa wakienda vituoni kusaidia wenzao waliopo vituoni...ili kumaliza tatizo hili unahitajika mshikamano unaothamini malezi," alisema Mzee Mwinyi.
Alisema mchango wa vijiji hivyo ni mkubwa na anaufahamu akiwa Rais wa Zanzibar kwani vimekuwa mstari wa mbele kusaidia watoto ambao wamepoteza wazazi na wale wanaotoka kwenye familia masikini.
Kutokaka na kazi nzuri inayofanya na vijiji hivyo, Mzee Mwinyi alisema wakati umefika sasa wa kuhakikisha vinaanzishwa kila mkoa, wilaya na tarafa ili kuwafikia watu wengi zaidi. Kwa sasa upande wa Tanzania Bara Vijiji vya SOS vipo Dar es Salaam na Arusha.
Aliahidi kuwa atatumia heshima aliyopewa ya kuwa balozi mzuri wa SOS kwa kuhamasisha wadau mbalimbali ndani na nje ya Tanzania kusaidia vijiji hivyo ili viweze kutimiza lengo lake.
Naye Mwenyekiti wa Bodi wa Vijiji vya SOS, Dkt. Mary Nagu, anasema lengo la vijiji hivyo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa sehemu salama ya kukulia watoto.
Alisema wakati Tanzania inaadhimisha miaka 50 ya uhuru, SOS inaadhimisha miaka 40 ya kuanzishwa barani Afrika. Alisema vijiji hivyo ni miongoni.
Mkurugenzi wa Taifa wa Vijiji vya SOS, Bi. Rita Kahurananga, alisema mkakati wa sasa wa vijiji hivyo ni kujenga vituo vingine katika mikoa mingine nchini ili kuwafikia watu wengi.
No comments:
Post a Comment