26 September 2011

Polisi watangaza vita Igunga

*Ni baada ya kulalamikiwa kufanya kazi kwa upendeleo
*Walinzi CCM wadaiwa kumtwanga mwandishi wa habari
*Habari zake zatajwa kumdhalilisha kigogo wa chama
*Aliyepigwa CUF atoka hospitali, wahusika bado kunaswa

Benjamin Masese na Peter Mwenda,Igunga

SIKU chache baada ya Jeshi la Polisi wilaya ya Igunga kulalamikiwa na vyama vya siasa vikiwemo
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na chama cha Wananchi (CUF) kushindwa kufanya kazi yake kama inavyostahili, sasa limejibu mapigo kwa kutangaza vita dhidi wakiukaji sheria na taratibu za uchaguzi.

Jana jeshi hilo lilijitokeza na kueleza kuchukizwa na na vitendo vinavyojitokeza kila siku katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Ubunge, vikiwemo vya ukatili, uhalifu, mashambulio ya kudhuru, vitisho, udhalilisha na ulipizaji wa visasi.

Pia limetoa onyo kwa vyama vya siasa, taasisi, wakazi na wananchi waliokwenda katika wilaya ya Igunga kwa shughuli mbalimbali kufanya kazi zao kufuata sheria na taratibu zilizopo, vinginevyo halitakuwa na huruma wala aibu pale watakapobainika kwenda kinyume.

Hivi karibuni CCM na CHADEMA vilitoa malalamiko dhidi ya jeshi hilo kushindwa kuweka ulinzi katika mikutano yao ya kampeni na wakishindwa kuchukua hatua za haraka wanapopelekewa taarifa za uhalifu au uvunjaji wa sheria za uchaguzi.

CCM ilidai kuwa polisi wamekuwa wakiacha kushughulikia taarifa wanazotoa kwao juu ya vitendo wanavyofanyiwa huku CHADEMA wakilituhumu kwa kujihusisha na masuala ya kisiasa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) anayeshughulikia Oporesheni Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Telesphory Anacleth alisema kuwa kadri siku zinavyokaribia uchaguzi, ndivyo kunavyoibuka tabia mbaya na matukio yenye sura ya uvunjifu wa amani.

SACP Anacleth alisema kutokana na vitendo hivyo sasa Jeshi la Polisi limesema limejipanga kuwashughulikia watu wanaokwenda kinyume na taratibu zilizowekwa pamoja kuvunja sheria na kujichukulia maamuzi ya papo kwa papo huku wakijua ni kosa kisheria.

"Haijawahi kutokea ndani ya miaka yangu 40 kazini kupongezwa, na sitaki nipongezwe na wanasiasa, mimi nitapongezwa na bosi wangu hivyo wanaolituhumu Jeshi la Polisi Igunga kufanya upendeleo hawajui walisemalo," alisema.

Aliongezwa kuwa kuna baadhi ya vyama vimekuwa vikitetewa katika uchaguzi, hivyo walitarajia itakuwa hivyo kila siku na kuwataka wanasiasa kufanya kampeni zao kwa kufuata sheria na sio kutegemea msaada wa kutoka polisi.

Alisema hivi sasa Jeshi la Polisi limejiimarisha kukabiliana na matukio yanayojitokeza na kuvionya vyama vya siasa, wananchi na wakereketwa wa vyama hivyo kuishi kwa kufuata sheria za uchaguzi, vinginevyo watajikuta wakishughulikiwa na kukabiliwa na kesi.

Bw. Anacleth alisema kuwa tangu kampeni zianze kumetokea matukio takribani sita ya kuzuru, uvunjifu wa amani, udhalilishaji, unyanyasaji, ulipizaji wa kisasi na mengineyo kama utumiaji wa risasi ambapo majalada ya matukio hayo yamefunguliwa.

Alitaja baadhi ya matukio ni la kumwagiwa tindikali, Mkuu wa Wilaya Bi. Fatuma Kimario kufanyiwa vurugu na wafuasi wa CHADEMA, kukamatwa kwa watu wakijihusisha na ununuzi wa shahada za kupigia kura na wengine wakichana bendera na mabango ya wagombea, uchomaji wa nyumba na mengineyo.

Alisema kuwa matukio kama hayo hayaleti sura nzuri ndani ya jamii na kwamba kuanzia sasa polisi haitakubali kupewa lawama ya kushindwa kudhibiti uhalifu na kukomesha matukio hayo.

Alisema tayari polisi wamesambazwa na kuweka kambi kila kata wakifuatilia mwenendo mzima wa kampeni hadi siku ya kupiga kura Oktoba 2, mwaka huu.

Wakati huo huo alitoa wito kwa waandishi wa habari kushirikiana nao ili kuwasaidia kutoa taarifa za ukweli kwani asilimia kubwa hushuhudia matukio yanayofanywa na wanasiasa.

"Polisi tunaomba waandishi kufanya kazi yetu kwa ushirikiano wa karibuni kwani lengo ni kuimarisha miundombinu ya usalama, amani na utulivu katika kipindi hiki cha mchakato wa kampeni ili wananchi wapate fursa ya kutumia demokrasia kuchagua chaguo lao kwa hiari yao bila kushurutishwa," alisema.

Hata hivyo, alionya waandishi kutojihusisha na siasa au vitendo vitakavyohatarisha amani na badala yake waelimishe jamii kupitia taaluma hiyo ili uchaguzi usipate dosari.

Wakati huo huo, baadhi ya askari waliokuwa katika tukio la kurindima risasi usiku wamelieleza Majira kwamba wamechukizwa na kitendo cha mbunge wa viti maalum vijana kutoka Mara Bi. Bulaya kuwatukana na kutoa kauli chafu ambazo zilikuwa zikiwadhalilisha.  

Askari hao ambao hawakutaka kutajwa majina yao walisema kitendo cha kufokewa na mbunge huyo huku akiwauliza kama wanapenda kazi zao, kiliwachukiza na kuonesha kama yeye ndiye mwajiri wao.

Alipotafutwa Bi. Bulaya kujibu tuhuma hizo alisema "by short this is wrong information, sio kweli, sikuwatukana wala kuwafokewa bali nilikuwa nawaeleza kuwakamata wahusika walioshambulia gari na kuvunja vyoo," alisema.

Walinzi CCM watembeza kipigo

Watu nane wanaosadikiwa kuwa walinzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamempiga mwandishi wa habari wa gazeti la Dira Mtanzania kwa kile kinachodaiwa aliandika habari za kukiponda chama hicho na kumdhalilisha Katibu wa Fedha na Uchumi, Bw. Mwigullu Nchemba.

Akisimulia mkasa huo mwandishi huyo, Bw. Mussa Mkama alisema tukio la kupigwa lilimpata Jumamosi saa 1 usiku akiwa na mwenzake, Bw. George Maziku baada ya kumaliza mahojiano na Mbunge wa Viti Maalum, Bi. Ester Bulaya katika hoteli ya The Peak ambako wanakaa viongozi wa CCM.

"Baada ya kumaliza mahojiano yetu na Bulaya wakati tukitoka getini niliwaaga walinzi nikiwambia sasa nimemaliza kazi yangu naondoka, mara niliitwa na mtu mmoja aliyevalia sare za CCM na baada ya kumkaribia nilizingirwa na kupigwa mateke na ngumi hadi kudondoka, hawakuishia hapo waliendelea kunipiga," alisema Bw. Mkama.

Alisema mwandishi wenzake aliyekuwa naye Bw. Maziku akisaidiwa na mtu mwingine walifanikiwa kuwatuliza walinzi hao ndipo alipopata nafasi ya kukimbia na kwenda Kituo cha Polisi cha Igunga kutoa taarifa.

Bw. Mkama alisema baada ya kutoa taarifa alikwenda hospitali ili kupata matibabu kutokana na maumivu mkononi, shavuni na sehemu za mbavu ambako walimpiga mateke hata baada ya kudondoka.

Alisema mahojiano na Bi. Bulaya yalihusu tukio la mbunge huyo kudai kutupiwa risasi na Mratibu wa Kampeni za CHADEMA, Bw. Mwita Mwikwabe kwa kile alichodai CCM kuharibu mikakati ya chama hicho ya kukusanya shahada za kupigia kura.

"Nadhani sababu kubwa ya mimi kupigwa ni zile habari zangu katika gazeti la Dira ya Mtanzania Jumatatu iliyopita likiwa na bahari mbili kubwa, ya kwanza ni ile ya 'CCM aibu tupu Igunga' ikieleza kufumaniwa kwa Mratibu wa Kampeni za CCM, Bw. Nchemba na nyingine ikisema kuwa 'CCM yakiri Rostam Kiboko'," alisema Bw. Mussa.

Alisema katika tukio hilo amepoteza vifaa vya kutendea kazi yake na fedha taslimu sh. 450,000 ambazo zilikuwa katika pochi yake

Mratibu wa Kampeni Bw. Nchemba alipoulizwa kuhusu walinzi wake kumpiga mwandishi alisema hana taarifa hizo, Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Igunga, alisema hajapokea taarifa za mwandishi huyo.

Aliyepigwa CUF atoka hospitali

Katika tukio jingine Mwenyekiti wa Wazee wa CUF, Bw. Salum Masanja ameruhusiwa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Igunga baada ya kudaiwa kupigwa na mabaunsa wa CCM waliokuwa katika msafara wa Katibu Mkuu wa UVCCM, Bw. Martin Shegela Jumanne iliyopita.

Msemaji wa CUF, Bw. Silas Bwire alisema kiongozi huyo wa CUF aliyepigwa wakati akipandisha bendera ya CUF katika Kijiji cha Iyogelo kesi yake itasimamiwa na chama mpaka ukweli ubainike na wahusika waliompiga wachukuliwe hatua.

CUF ambacho kiko katika kampeni zake za chini kwa chini, nyumba kwa nyumba na mikutano ya hadhara kimewataka wananchi wakichague kwa sababu ndicho pekee chenye kuhubiri amani kwa Watanzania wote bila kujali itikadi.

Meneja wa Kampeni wa CUF, Bw. Antony Kayange alisema vyama vinavyowapiga viongozi wa vyama vingine wanachama wao na kumwagia watu tindikali wataendeleza visasi baada ya mbunge wa chama chao kuchaguliwa.

Mgombea Ubunge wa CUF, Bw. Leopold Mahona alisema imefika wakati CCM iache madaraka kwa upinzani ili walete maendeleo kwa wananchi wa Igunga ambao maisha yao ni duni na ya kubahatisha.

Kaimu Katibu Mkuu wa CUF, Bw. Julius Mtatiro akihutubia wananchi wa Igunga katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Sokoni mjini hapa juzi alisema chama chake kitachukua jimbo la Igunga kwa sababu kina mtaji wa kura 11,321 alizopata mgombea wao mwaka 2010 na kinakubalika kwa vwananchi kwa sababu hakina vurugu wala siasa za chuki.

Alisema katika kampeni zao katika Kata 26 za Igunga wananchi wameahidi kuwapigia kura za ndiyo kwa sababu ya kuhubiri amani na utulivu kwa Watanzania.

Mangula: CCM imeleta maendeleo

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Bw. Phillip Mangula amewataka wananchi wa Igunga wakipigie kura chama hicho kwa sababu kimeleta maendeleo makubwa kutoka upatikane uhuru nchini.

Bw. Mangula akihutubia mkutano wa kampeni katika Kata ya Mwamasunga katika kata ya Igunga alisema wakati wa uhuru hakuna Mtanzania aliyemiliki baiskeli ikilinganishwa na sasa hivi ambako kila mmoja anao uwezo wa kununua.

Alisema wakati huo pia mkoa wa Tabora kulikuwa na shule mmoja ya Sekondari lakini sasa hivi kuna shule zaidi ya 154 katika mkoa wa Tabora.

Hata hivyo, wananchi hao walitoa masharti kwa CCM wamelete mgombea ubunge wa Jimbo la Igunga, Dkt. Dalaly Kafumu awaahidi jinsi atakavyotatua matatizo yanayowakabili ya uhaba wa maji, masoko ya mazao yao na upatikanaji wa pembejeo.

Wananchi hao walisema hawako tayari kupewa ahadi hewa kama alizowahi kutoa mbunge aliyejiuzulu, Bw. Rostam Aziz aliyejivua gamba kutoka CCM.

Kuhusu amani,  Bw. Mangula alisema: “Puuzeni uchochezi unaofanywa na wanasiasa ili kuenzi amani na utulivu vilivyopo nchini”.

9 comments:

  1. "Haijawahi kutokea ndani ya miaka yangu 40 kazini kupongezwa, na sitaki nipongezwe na wanasiasa, mimi nitapongezwa na bosi wangu hivyo wanaolituhumu Jeshi la Polisi Igunga kufanya upendeleo hawajui walisemalo," alisema.

    Aliongezwa kuwa kuna baadhi ya vyama vimekuwa vikitetewa katika uchaguzi, hivyo walitarajia itakuwa hivyo kila siku na kuwataka wanasiasa kufanya kampeni zao kwa kufuata sheria na sio kutegemea msaada wa kutoka polisi.

    Wakati huo huo, baadhi ya askari waliokuwa katika tukio la kurindima risasi usiku wamelieleza Majira kwamba wamechukizwa na kitendo cha mbunge wa viti maalum vijana kutoka Mara Bi. Bulaya kuwatukana na kutoa kauli chafu ambazo zilikuwa zikiwadhalilisha.

    Askari hao ambao hawakutaka kutajwa majina yao walisema kitendo cha kufokewa na mbunge huyo huku akiwauliza kama wanapenda kazi zao, kiliwachukiza na kuonesha kama yeye ndiye mwajiri wao.

    kila JAMBO LINA MWISHO! MWISHO WA UBABE WA ccm U KARIBU!

    ReplyDelete
  2. Ningewajua hao waliompiga mwandishi wa habari ningewapa zawadi na tuzo ya kazi bora,nyie waandishi huko mmeenda kufanya kazi za vyama na si za uandishi,sasa hayo ndiyo matokeo yake. Kwa sasa mnatamani mpande majukwaani muwapigie kampeni wagombea,hii ni aibu kwa sekta ya uandishi wa habari,hivyo vijisenti vidogo mnavyopewa na vyama vinawatoa kwenye utu na taaluma yenu. SIJAONA WAANDISHI WAPUMBAVU KAMA WALIOKO IGUNGA. HUO NI MWANZO TU BAADAYE ITABIDI HIVYO VYAMA VINAVYOWARUBUNI VIWAWEKEE ULINZI VINGINEVYO HATA VIFO VITAWAKUMBA

    ReplyDelete
  3. Maoni yako ni ya kishetani nadhani wewe ni mtumwa wa ADUI IDILISI. NINGEKUFAHAMU JAPO KWA SURA NINGEKUAMBIA NI LINI ADHABU YENU ITAKUJA. EENDELEENI, JAPO KIDOGO TU CHAMA CHENU KITAKUWA CHA UPINZANI. WAANDISHI WANAKOSA NINI?

    ReplyDelete
  4. wewe ndugu yangu!!!!! ama kweli ni fukara mkubwa wa mawazo. Kumbe wew hamnazo!!!
    kama sio waandishi hao hao, un gejua je kuwa Mwandishi kapigwa halafu ukajitapa kuzawadia? Lo! binadamu asiye na akili ni kama ng'ombe tu!

    ReplyDelete
  5. Sisi tujuavyo Polisi hawana chama chochote na hawaruhusiwi kujihusisha na siasa. Iweje Polisi wanaotakiwa kulinda usalama leo hii watutangazie vita? Kisa tu ushabiki wa chama fulani na nadhani chama tawala kwa sababu Polisi ni watimizaji amri za hao mabwana wakubwa mafisadi. Ninashauri Polisi wafanye kazi yao na si kuburuzwa na watawala kwa sababu iko siku hicho chama kinachowatuma kitagaragazwa. Tusiwe na imani 100 kwa 100 kwamba CCM itaendeleaga tu kutawala milele na milele ni makosakuwa na mawazo hayo tuangalie mifano ya nchi za wenzetu hapo hapo tusome alama za nyakati jamani.

    ReplyDelete
  6. CCM mwisho wake umekaribia sasa,Hivi karibuni Mh.Rais alipokuwa kwenye ziara yake mkoani Kigoma.Wakati anaweka jiwe la Msingi Kwenye daraja la Mto wa Malagarasi.
    Mh.J.Magufuli alitamka kwenye Mkutano wa hadhara kuwa CCM ni chama cha Mungu.
    Mungu huwa anachama?
    Hawao wanaodhani kuwa CCM itatawala milele wamepotoka kimtazamo husani watoto wa vigogo na wala rushwa na mafisadi.
    Kutokana na tamko hilo la Mh.Magufuli asipoomba msamaha kwa Mungu ajue CCM ndio inakwenda ikifa kama UNIP ya Zambia.
    Hiyo ni Changa moto kwa Waziri.

    ReplyDelete
  7. waandishi waliopo igunga ni njaa tupu. wanahongwa na slaa hela kidogo tu wanaanza kuadika habari za hovyo. wanadhalilisha taaluma yetu ya uandishi

    ReplyDelete
  8. Mimi nashangaa sana watu wasiotaka ukweli! Mimi si mwanachama wa chama chochote wala si CCM wala CUF wala Chadema. Lakini ukweli unabaki pale pale kwamba Chadema wanafanya fujo nyingi sana Igunga. Na hilo litawagharimu. Hawapati kitu kule. Ndio vijana ni limbukeni wakiwa fedha kidogo tu basi wanaanza mkusheli. Ninajua sana kwamba Wachaga wamepitia magazeti kuwahonga waandishi wa habari ili wasieleze ukweli wa mambo hata kwa watu tuliombali na Igunga. Lakini iwe isiwe uchaguzi ukiwa huru na wa haki Chadema hawatakuwa na chao. Kwani waandishi wa habari si wapiga kula wao wanashughulika na saikolojia ya uchaguzi. Wanawatumainisha wapenzi wa Chadema kwa kuwaambia uongo. Sasa siku hizi rushwa mpaka kwenye uandishi wa habari. Tuko vibaya sana Tanzania. Waandishi wenye njaa akipewa na Mbowe laki moja tu anaanza kuandikia kukipendelea Chadema hajiulizi hivi hizi fedha Mbowe kazipata wapi? Na atazirudishaje hizi fedha akipata hicho cheo. Ni kuongeza matatiza juu ya matatizo ufisadi mpaka kwenye uandishi wa habari. Muuu yetu macho tu.

    ReplyDelete
  9. Acha wongo wako. Imekuwaje uwe hakimu dhidi ya CHDM. Wewe ni mjumbe wa upande moja. Usingejitokeza ukanyamaza ungekuwa na hekima tena.

    ReplyDelete