Na Moses Mabula, Igunga
IKIWA ni siku ya kwanza kuanza kwa kampeni jimboni Igunga Chama cha Wananchi (CUF) kupitia mgombea wake Leopard Mahona kiliweka pingamizi kwa
wagombea wa vyama vya (CHADEMA) kwa Joseph Kashindye na Dkt. Peter Kafumu CCM kikidai kuwa wagombea hao ni
wafanyakazi wa serikali hivyo hawapaswi kuwania nafasi hiyo.
Hata hivyo msimamizi wa uchaguzi Bw. Protace Magayane alisema kwa mujibu wa sheria na maadili ya utumishi wa umma na sababu alizozitoa si za msingi hivyo pingamizi hilo amelitupilia mbali kwa kuwa watumishi hao waliomba ruhusa mapema kutoka katika Idara zao juu ya mchakato huu.
Awali cha Wananchi (CUF) jana jioni kiliweka pingamizi dhidi ya Dkt. Kafumu na Bw. Kashindye kwa madai kuwa ni wafanyakazi wa Serikali na kwamba hawajawahi kuandika barua za kujiuzulu nyadhifa zao.
Akiwakilisha pingamizi hizo kwa Mkurugenzi wa uchaguzi Jimbo la Igunga jana, Ofisa wa Haki za Binadamu wa Taifa (CUF) Bw. Hashim Mziray, alisema wagombea hao hawajawahi kuchukua hatua za kuandika barua za kuachia ngazi serikalini.
Katika kujibu pingamizi hilo Bw. Magayane alibainisha kuwa mgombea wa chama cha Demokrasia na Maendeleo alikuwa mtumishi wa Idara ya Elimu katika Halmashauri ya Igunga na mpaka sasa mgombea huyo ameacha kazi mapema na ofisi husika inatambua suala hilo.
’’Mpaka sasa Joseph Kashindye na Peter Kafumu hao si watumishi tena, Kafumu aliomba ruhusa ya bila malipo toka mwezi tisa na Bwana Kashindye alikwishaomba ruhusa pia kwa sababu hizo madai yao si ya msingi nimeyatupilia mbali,” alisema Magayane msimamizi wa uchaguzi huo.
Kwa nyakati tofauti chama cha Sauti ya Umma(SAU) kilipeleka pingamizi mapema jana kwa msimamizi huyo kikidai kuwa wagombea wa CCM na CHADEMA si wanachama wa vyama vyama husika.
Kwa mujibu wa msimamizi wa uchaguzi huo Bw. Protace Magayane baada ya kuangalia uthibitisho wa sheria na tamko la mahakamani imeonekana kuwa kwa pamoja
wagombea hao ni wanachama wa vyama vyao kwa kufuata taratibu na kanuni za sheria.
Alisema kuwa wagombea hao wanatambulika kitaratibu na kauni za vyama vyao pamoja na sheria ya vyama vya siasa kuhusu uanachama wao.
Bw. Magayane alisema kuwa mapingamizi yote hayo hayana ushahidi wa kutosha kwa kuwa kama
walalamikaji hawatoridhika na majibu hayo muda bado wa kukata rufaa mahakamani upo kwa saa 24 zijazo ndipo shauri hilo laweza kusikilizwa.
Katika hatua nyingine CUF kimejigamba kwamba kitachukua jimbo hili kwa vile kina kila sababu kwa kuwa kihistoria Mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho Bw. James Mapalala amekuwa akisema kwamba CUF kilianzia Igunga.
Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Mwanza Bi. Mokiwa Kimwanga na Mbunge wa Jimbo la Mkoani Zanzibar Bw. Ally Hamis Seif, walisema CUF itazindua rasmi Kampeini zake Septemba 13 ambapo Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Profesa Ibrahim Lipumba ndiye atakuwa mgeni rasmi.
Bi. Kimwanga alisema CUF kimejiandaa kuomba kura katika kata zote 26 za jimbo hilo ikiwashirikisha vijana, wanawake na wazee kuomba kura kwa wananchi.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Vijana Taifa wa CUF Bw. Mohamed Babu amekanusha tuhuma zilizoelekezwa kwao kuwa wao ni chanzo cha vurugu zilizosababisha mtafaruku wakati wa kurudisha fomu za wagombea wa Chama hicho na CHADEMA.
Alisema kuwa wafuasi wa CHADEMA ndio walikuwa wa kwanza kumzuia mgombea wa CUF Bw. Leopoad Mahona asiweze kurudisha fomu katika kipindi hicho ambacho na wao walikuwa wamejiandaa kurudisha fomu za mgombea wao.
Hata hivyo Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Igunga Bw. Christopher Saye alisema nao wamewasilisha malalamiko yao kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo (OCD) wakidai kuwa walifanyiwa fujo.
No comments:
Post a Comment