Na Godfrey Ismaely
KAMPUNI ya Uchimbaji Madini ya African Barrick Gold (ABG) imezindua mfuko wa maendeleo ambao utaratibu na kuongoza mipango mbalimbali ya uwekezaji
katika shughuli za jamii hapa nchini.
Mfuko huo utakuwa unajikita zaidi vijijini huku ukitengewa dola za Marekani milioni 10 (Sh. bilioni 16) kila mwaka.
Akizungumzia juu ya ujio wa mfuko huo, Dar es Salaam jana, Makamu wa Rais wa ABG,Bw. Deo Mwanyika, alisema mfuko huo umelenga kutoa usaidizi kwenye maendeleo ya jamii pamoja na kubeba uzito wa mahitaji ya miradi mbalimbali.
"Mfuko huu wa maendeleo umelenga kukuza mkakati wa jumla wa maendeleo ya jamii pamoja na kuunganisha juhudi za vituo vyote hapa nchini, hivyo mfuko huu utasaidia kubeba uzito wa mahitaji na uzito wa miradi mbalimbali ya wananchi," alisema Bw. Mwanyika.
Alisema mfuko huo ambao unaanza kazi mara moja baada ya kuzinduliwa jana, utakuwa hauna kikomo katika masuala ya afya, mazingira, uendelezaji stadi na mafunzo.
"Kimsingi mfuko umeundwa ili kutoa usaidizi kwa maendeleo ya jamii kwenye vijiji jirani na migodi ya AGB nchini Tanzania pia mipango ya maendeleo ambayo inaendana na mkakati wa maendeleo ya kitaifa kote nchini itazingatiwa na kupewa kipaumbele," alisema BW.Mwanyika.
Bw.Mwanyika alisem ili kuhakikisha fedha hizo zinatumika ipasavyo, tayari ABG, imeunda kamati ambayo itakayosimamia uratibu wake na maombi ya wananchi ambao wanahitaji miradi iendelezwe.
Kwa upande wake Mjumbe Huru wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mampuni AGB, Balozi Juma Mwapachu, alitumia fursa hiyo kuzishauri sekta binafsi makampuni yaliyopo hapa nchini kuchangia maendeleo ya jamii bila kujinadi kwamba kufanya hivyo ni kufanyiana hisani.
"Kwa mtazamo wangu ninazishauri kampuni zilizopo hapa nchini, nje ya kuchangia katika pato la taifa kwa njia ya kodi zitambue shughuli za maendeleo ya jamii inayowazunguka, zinapaswa kuwezeshwa nao pasipokuweka uhisani, hiyo ni haki ya wananchi kupata msaada wa hali na mali kwao," alisema Balozi Mwapachu.
No comments:
Post a Comment