26 September 2011

NCCR: NEC ndio kiini cha Vurugu Igunga

Rachel Balama na Anneth Kagenda

CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimesema vitendo vya vurugu vinavyokumba kampeni za uchaguzi mdogo Jimbo la Igunga ni matokeo ya Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) kushindwa kuweka sheria ya maadili ya uchaguzi.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es salaam jana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw.Samuel Ruhuza, wakati akitoa tamko la NCCR Mageuzi kuhusu matokeo ya uchaguzi Mkuu wa Zambia kwa waandishi wa habari.

Bw. Ruhuza alisema kuwa NEC inawajibika kwa vitendo vyote viovu vinavyoendelea kutokea  Igunga kutokana na kutoandaa sheria ya  maadili ya uchaguzi ambapo kila chama kinaamua kufanya kinavyotaka.

"Uchaguzi uliopita Tume kwa kushirikiana na vyama vya siasa viliandaa sheria ya maadili ya uchaguzi, lakini kwa uchaguzi huu mdogo na ule wa madiwani katika kata 22 kwenye majimbo mbalimbali ya Tanzania Bara Tume imekataa sheria hiyo kutumika kwa madai kwamba ina makosa," alisema.

Alisema kutokana na Tume hiyo kutoandaa sheria hiyo watanzania wanashuhudia vurugu kila wakati huku kukiwa hakuna mtu wala chama anayechukuliwa hatua zozote za kisheria.

"Uzembe na ukiritimba wa NEC ndio maana watu wamekuwa wakidiriki hata kupanda majukwaani wakiwa na bastola kiunoni kwa kujua kwamba hakuna hatua yoyote ya kisheria watakayo chukuliwa," alisema.

Bw. Ruhuza aliongeza kuwa ipo haja ya kuwepo kwa Tume huru ambayo itakuwa na idadi ya watu, vigezo vya wafanyakazi hata kama itateuliwa na rais.

Alidai kuwa hiviu sasa Mkurugenzi wa NEC yuko juu ya sheria na kwamba hali hiyo imekuwa ikichangia kutokea kwa vurugu katika hcaguzi ndogo.

Hata hivyo kwa mujibu wa Katiba ya nchi na sheria hakuna aliye juu ya sheria.

Katibu huyo alitoa pongezi kwa Tume ya Uchaguzi ya Zambia kwa kuepusha taifa hilo kuingia kwenye vurugu kwa kuzingatia sheria ya uchaguzi hatimaye kumtangaza Bw.Michael Chilufya Sata kuwa rais kutoka chama pinzani.

Alisema Tume hiyo inastahili pongezi kwa  kuepusha vurugu kwa kuwa nchi nyingi za kiafrika zinaingia katika vurugu wakati wa uchaguzi kutokana na matokeo.

Alisema sio jambo trahisi kuona tume iliyoteuliwa na mtawala ikitangaza aliyeiteua kushindwa.

1 comment:

  1. NCCR Mageuzi, hivi hiki Chama kipo? au ndiyo kinatapatapa, mtaishia kutoa Pongezi kwa Wengine tu ninyi hakuna lolote la Maana mnasubiri mpaka CCM iteleze Mpate pa kuanzia, Sasa kwa Taarifa zilizopo hao CCm wenzenu wamekwishajua walijikwaa wapi, huo moto wao wakiuwasha sijui nani atauzima, kalieni hivyohivyo na midomo kama vikundi vya ngonjera.Tunataka sera na mikakati ya kumnufaisha mtanzania kutokana na Umasikini.

    ReplyDelete