26 September 2011

Mokiwa akataa sekondari za kata

Na Patrick Kossima, Mbeya

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania,(KAT) Dkt.Valentino Mokiwa, amesema haungi
mkono shule za sekondari za kata kwa kuwa hazijaandaliwa
vizuri kuwawezesha
watoto kukomaa na kupata elimu iliyo bora.

Askofu Mokiwa alisema hayo jana katika mahubiri yake kwenye Kanisa Kuu la Anglikana Mbeya ikiwa ni siku ya mwisho ya ziara yake ya kutembelea Dayosisi ya Nyanda za Juu Kusini.

Alisema shule nyingi za kata hazikidhi mahitaji ya kielimu hivyo hata elimu inayotolewa katika shule hizo haiwezi kuwa na tija kwa mahitaji ya ushindani
wa kielimu.

Alisema kutokana na shule hizo kujengwa bila mpango thabiti wanafunzi wake wamekuwa
wakisoma kwa mtindo wa kinadharia zaidi na kukaririshwa hali ambayo hawawezeshi kuelewa vizuri.

“Vijana wa siku hizi mnafundishwa maswali yote mnapewa majibu ya kuchagua, mnapofundishwa suala la ufahamu mnashindwa kuelewa,”alisema Dkt.Mokiwa wakati akijibu swali alilowauliza vijana wa kipaimara.

Awali askofu mokiwa aliwataka vijana wake kujibu kuwa Yesu Kristo ni nani swali iliyowafanya vijana hao kushindwa kujibu kwa ufasaha licha ya kuwapa majibu ya kuchagua.

Askofu Dkt. Mokiwa alisema ili kurudisha elimu katika kiwango bora serikali inawajibika kurejesha shule za seminari kwa Makanisa ili waziendeleze kwa kuwa zilimjenga mwanafunzi kiroho na kiakili.

Alisema serikali ilizichukua shule hizo za seminari kama majengo na kuacha msingi
ambao ulikuwa umewekwa awali hususan mfumo mzuri wa ufundishaji uliozingatia maadili ya mwalimu na mwanafunzi.

Alisema ni muhimu kwa serikali kurejesha shule za misheni kwa kuwa zilikiwa mali ya Kanisa kwa lengo la kusaidia kujenga msingi imara wa elimu unaozingatia maadili kwa vijana wa kitanzania.

Akizungumzia suala la ufisadi, Dkt.Mokiwa alisema ufisadi ni roho na tabia mbaya
ambayo ipo katika kada mbalimbali kuanzia ngazi ya familia mpaka taifa.

Alisema roho hiyo mbaya ya ufisadi inapaswa kukemewa kuanzia ngazi ya familia na kuonya kuwa ikiachwa baadaye inakuwa na kuharibu taifa katika sekta zote za maendeleo hivyo kuzua malalamiko mengi kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment