12 September 2011

Madrid yapeta Hispania, Barca yavutwa shati

BARCELONA, Hispania

TIMU ya Real Madrid, imeendelea kujiimarisha mapema kwenye michuano ya Ligi Kuu Hispania, baada ya kuichapa timu ya Getafe 4-2 huku Barcelona, ikibanwa mbavu baada
ya kutoka sare ya  mabao 2-2 na Real Sociedad.

Katika mechi ya Barcelona, timu hiyo ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 takribani dakika 12 yaliyowekwa kimiani na wachezaji Xavi Hernandez na Cesc Fabregas, huku ikiwa imewapumzisha Lionel Messi na Andres Iniesta kwa ajili ya mechi ya kesho ya Klabu Bingwa Ulaya, dhidi ya AC Milan.

Wachezaji Imanol Agirretxe na  Antoine Griezmann wa Socieded wakasawazisha mabao hayo kipindi cha pili.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Marekani (AP), hali hiyo ilimlazimu kocha wa Barcelona, Pep Guardiola kuwaingiza Messi na Iniesta ili kusaka ushindi, lakini mlinda mlango Claudio Bravo, akazuia nafasai moja nzuri ya Messi akiwa ndani ya eneo la hatari zikiwa ni dakika 15, tangu aingie uwanjani.

“Makosa mawili kiulinzi ndiyo yaliyotugharimu,” alisema Xavi. “Hilo ndilo soka. Mechi tulikuwa tumeidhibiti na tungeweza kupata ushindi kwa kufunga bao la tatu,” aliongeza.

Wakati Barcelona wakivutwa shati, Real Madrid wao walikuwa wakizidi kujiimarisha baada ya Karim Benzema, kupachika mabao mawili dhidi ya Getafe.

Mshambuliaji huyo Mfaransa, aliipa Real Madrid bao la kuongoza dakika ya 14 kabla ya mshambuliaji wa Getafe, Nicolas 'Miku' Fedor kusawazusha bao hilo kipindi cha kwanza cha mchezo huo uliofanyia Jumamosi, kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.

Mbali na mabao hayo, mkwaju wa penalti iliyochongwa na Cristiano Ronaldo na bao la pili la Benzema liliashiria kama timu hiyo itaibuka na mvua ya magoli, baada ya timu hizo kutoka mapumziko, lakini Miku akapachika jingine lililoufanya mchezo kuendelea kuwa wa vuta nikuvute, kabla ya mchezaji, Gonzalo Higuain kuipatia bao la mwisho Real Madrid dakika za mwisho.

Matokeo hayo yanaifanya Real Madrid, kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi sita ambazo ni pointi mbili zaidi dhidi ya Barcelona.

No comments:

Post a Comment