19 September 2011

Mayweather amtwanga Ortiz

LAS VEGAS, Marekani

FLOYD Mayweather Jr. ameendelea kuwa bondia ambaye hajawahi kupigwa, baada ya kumsimamisha mpinzani wake Victor Ortiz, katika pambano la kuwania
ubingwa wa Welter, lililofanyika usiku wa kuamkia jana mjini Las Vegas nchini Marekani.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Marekani (AP), Mayweather aliibuka na ushindi huo, baada ya kumchapa Ortiz, dakika ya 2:59 ya raundi ya nne kwa kumshindilia makonde mfululizo yaliyomfanya mpinzani wake kwenda chini.

Kwa mujibu wa AP, kisago hicho kilikuja baada ya mabondia hao kutoka mapumziko ambapo Ortiz, alimfuata moja kwa moja Mayweather katikati ya ulingo na baada ya kugonganisha mikono, Mayweather aliachia konde la mkono wa kushoto na lingine la kulia yaliyomfanya Ortiz, kuanguka chini.

AP ilieleza kuwa baada ya Ortiz, kuanguka chini alijaribu kunyanyuka kwa shida, lakini mwamuzi Joe Cortez, akaamua kumaliza pambano.

“Tuligonganisha glove na tukawa tayari kupambana, baadaye nikaachia konde la mkono wa kushoto na kulia,” alisema Mayweather. “Ulingoni unapaswa kujilinda mwenyewe muda wote,” aliongeza bondia huyo.

Hata hivyo kabla ya pambano hilo kumalizika, raundi hiyo ilionekana kuwa na utata, baada ya Ortiz, kumpiga kichwa makusudi Mayweather jambo ambalo lilimfanya aonywe na mwamuzi Cortez, lakini baada ya hapo bondia huyo akaenda kumbusu Mayweather juu ya shavu.

No comments:

Post a Comment