LONDON, England
MICHUANO ya Klabu Bingwa Ulaya, iliendelea usiku wa kuamkia jana na kushuhudiwa mechi nyingi zikitawaliwa na sare.Hata timu zilizoshinda, nazo ziliibuka
na ushindi mwembamba kama ilivyokuwa katika mechi za juzi.
Katika mfululizo wa michuano, huyo timu mbili za Uingereza, Manchester City na Manchester United zililazimishwa sare ya bao 1-1 na wapinzani wao.
Timu za Real Madrid na Bayen Munich zenyewe ziliibuka na ushindi mwembamba dhidi ya wapinzani wao.
Katika mchezo uliozikutanisha Man United na Benifica mjini Lisbon, Ureno jitihada za mchezaji Ryan Giggs ndizo ziliifanya timu yake kuambulia pointi katika mchezo huo wa kwanza, ambao ulionekana kuwa mgumu.
Ilikuwa ni pasi ya Nicolas Gaitan iliyomfikia Oscar Cardozo, ikiwa ni dakika ya 24 ya mchezo huo na kisha akautuliza kifuani kabla ya kuachia mkwaju mkali, akiwa umbali wa yadi 16.
Hata hivyo zikiwa zimebaki dakika tatu, kabla ya mapumziko, Giggs aliambaa na mpira kupitia wingi ya kulia na kuachia mkwaju mkali, akiwa umbali wa yadi 20 na kusawazisha bao hilo.
Shujaa wa mchezo huo alionekana kuwa kipa wa Manchester United, Anders Lindegaard ambaye aliokoa mashuti ya wachezaji Nolito na Gaitan na kuinusuru timu hiyo isiambulie kichapo.
Wakati Man United ikabanwa mbavu, mambo yalikuwa vilevile kwa Man City ambayo ilisawazisha bao kupitia kwa Aleksandar Kolarov ambaye alipiga shuti la mpira wa adhabu lililotinga wavuni na kuinusuri timu yake kupata pointi dhidi ya Napoli.
Pamoja na vijana hao wa Roberto Mancini, kuanza vyema katika michuano ya Ligi Kuu lakini usiku wa kuamkia jana, wakajikuta mambo ni magumu katika michuano hiyo ya Klabu Bingwa Ulaya, baada ya kupelekwa puta na Napoli ya Italia.
Man City inashiriki michuano hii kwa ya mara ya kwanza baada ya kukosekana kwa miaka 43.
Timu hiyo nusura iondoke na kumbukumbu mbaya, baada ya Edinson Cavani kumalizia shambulizi safi na kuipa Napoli bao la kuongoza dakika ya 69.
Hata hivyo bao hilo lilisawazishwa kwa mkwaju mkali wa Kolarov, lililojaa wavuni dakika sita baadaye.
Matokeo mengine ya michuano hiyo yalikuwa kama ifuatavyo, Ajax ilitoka suluhu na Lyon huku Basle ikiifunga SC Otelul Galatimabao 2-1.
Dinamo Zagreb ilala bao 1-0 dhidi ya Real Madrid, huku
Inter Milan ikichapwa bao 1-0 na Trabzonspor, Lille ilitoka sare na CSKA Moscow mabao 2-2 na Bayern Munich ikainyuka Villarreal mabao 2-0.
No comments:
Post a Comment