06 September 2011

Magufuli ataka JK apuuze wanaompinga

*Aomba amuache atekeleze sheria zilizopo
*Asema wakisilizwa watajenga juu ya madaraja
*Rais naye ataka wabadhirifu wafukuzwe kazi


Gladness Mboma na Godfrey Ismaely

WAZIRI wa Ujenzi Dkt. John Magufuli amemuomba Rais Jakaya Kikwete kuzipuuza lawama ndogo ndogo zinazopelekwa
kwake na badala yake amuache atekeleze sheria.

Mbali na hilo Waziri huyo aliiagiza Bodi ya Usajili wa Makandarasi nchini kufanya ukaguzi katika miradi ya barabara ya Halmashauri mbalimbali nchini ili wakurugenzi watakaobainika 'kuchakachua' fedha hizo wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Dkt. Magufuli aliyasema hayo jana Dar es Salaam wakati Rais Kikwete alipokuwa akifungua mkutano wa pamoja wa Wabunifu, Wahandisi na Wakadiriaji Majengo.

"Mheshimiwa Rais tutafanya kazi mchana na usiku lakini tunakuomba zile lawama ndogo ndogo zitakazokuwa zinaletwa kwako zisikilize na kisha uziache halafu tuachie nafasi sisi tufanye kazi yetu kwa kuzingatia misingi na taratibu za sheria,"alisema.

Bw. Magufuli alisema kama malalamiko hayo yatakuwa yanasikilizwa watalegalega na itafikia hatua ya nyumba kujengwa hadi juu ya madaraja.

Akizungumzia juu ya fedha maalum kwa ajili ya mfuko wa ujenzi wa barabara Bw. Magufuli alisema, katiba ya nchi inaeleza kuwa kila mtu anapaswa kuzingatia sheria zilizowekwa kwa mujibu wa katiba bila kujali cheo chake ili kutimiza haki na kulijenga taifa.

"Hivyo basi kupitia ibara  ya 26 (1,2)ninatoa agizo kwa bodi zote tatu za makandarasi nchini kwa pamoja kukagua matumimzi ya fedha za mfuko wa maendeleo ya barabara katika kila Halmashauri kwa kuwa matumizi yake ni mabaya iwapo itabainika Mkurugenzi yeyote kuhusika na uchakachuaji ninaomba majina yao yote yaorodheshwe na muyawasilishe kwangu," alisema.

Alisema mara baada ya kukabidhiwa majina hayo ya wakurugenzi wabadhirifu wa miradi ya maendeleo ya barabara atayapeleka majina hayo kwa rais bila kuyachakachua. "Kwa hiyo kuanzia hapa mheshimiwa Rais ninakuomba mara baada ya kuwasilisha majina hayo kwako uyafanyie kazi mara moja ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidhi ya wahusika hao," alisema.

Dkt. Magufuli alisema kuwa wizara yake itaanza kuchukua hatua kwa wahandisi na wakandarasi watakaoshindwa kufanya kazi zao kwa ufanisi ambapo aliigiza Kitengo  cha Usimamizi wa Barabara kilichopo chini  ya (TANROADS)kibadilishwe.

"Mkurugenzi wa TANROADS naagiza kuwa kitengo cha usimamizi wa barabara kilichopo chini yako kivunjwe mara moja maana wasimamizi waliopo hawafai," alisema.

Alisema kuwa katika kusherehekea miaka 50 ya Uhuru Watanzania walipaswa kumsifu na kumpongeza Rais Kikwete kutokana na kazi nzuri alizozifanya  chini ya uongozi wake na kwamba wasiofanya hivyo wanamuonea wivu.

Alisema kuwa katika miaka 50 ya uhuru mambo mengi yamefanyika katika kipindi cha utawala wa Bw. Kikwete hususani katika upande wa miundombinu.

Alikiri kuwa wapo wakandarasi na wahandisi ambao wamejenga nyumba na barabara chini ya viwango, hivyo kuwaporomokea wananchi na kuwasababishia madhara mbalimbali.

"Ninawaomba radhi watanzania kwa niaba yao, hasa wale waliopata madhara, lakini wakandarasi walio wengi ni wachapakazi na wale wabaya inawezekana hata leo hawakufika katika mkutano huu,"alisema.

Naye Rais Kikwete alisema kuwa serikali itaanza kutoa upendeleo wa kazi kwa wakandarasi wazalendo ili kujijengea uwezo ikiwa ni pamoja na kukuza ajira na kuinua uchumi wa Taifa.

Rais Kikwete aliwataka wakandarasi kuwa na ushirikiano wa pamoja katika kazi zao ili waweze kuzifanya kwa ufanisi zaidi badala ya kufanya mmoja mmoja, ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wakandarasi wanawake.

Alisema kuwa wakandarasi wasiokuwa na ubora na kufanya kazi zisizomalizika kwa wakati na zenye gharama kubwa waachane nao ili kujijengea heshima.

"Kuwafukuza watu wasiokuwa waaminifu utawajengea heshimna katika kazi zenu, msioneane haya. Wasiofanya vizuri wanatia doa kazi zenu na kuonekana hazina heshima," alisisitiza.

2 comments:

  1. Yeye Raisi kafukuza wangapi?

    ReplyDelete
  2. Tunngekuwa na akina Magufuli kama watano kwenye sisteam nadhani nchi hii ingekuwa safi sana hata mheshimiwa president asingekuwa anakuna kichwa.

    ReplyDelete