09 September 2011

Liyumba apandishwa tena kizimbani

*Ni kwa kosa la kukutwa na simu gerezani

Na Rehema Mohamed

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Amatus Liyumba, ambaye pia ni mfungwa namba 303/2010 amepandishwa
kizimbani akikabiliwa na kosa la kukutwa na simu gerezani.

Bw.Liyumba alifikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu, Bw.Stuwart Sanga, na kusomewa makosa yake na Wakili wa Serikali Bi.Elizabert Kaganda.

Akisoma shitaka hilo Bi.Kaganda alidai kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Julai 27 mwaka huu katika Gereza la Ukonga, Dar es Salaam kinyume na sheria ya magereza namba 86 kifungu namba 1 na 2 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Bi.Kaganda alidai kuwa mtuhumiwa akiwa gerezani alikutwa na simu aina ya Nokia 1280 nyeusi iliyokuwa na laini namba 0653 004662.

Alidai mtuhumiwa alikutwa akiitumia simu hiyo binafsi gerezani humo bila ya ruhusa kutoka kwa mamlaka husika.

Bw.Liyumba alipohojiwa na hakimu kama ametenda kosa hilo alikana kutenda kosa hilo.

Hakimu Bw.Sanga alitaja masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na mdhamini mmoja wa kuaminika anayefanya kazi serikalini ama taasisi inayotambulika na serikali atakayesaini dhamana ya sh.50,000.

Kutokana na masharti hayo, Bw.Liyumba alifanikiwa kudhaminiwa na kesi kuahirishwa hadi Septemba 29 mwaka huu.

Hata hivyo kwa kumujibu wa wakili wa mshitakiwa huyo, Bw. Liyumba anatarajiwa kumaliza kifungo chake Septemba 28, mwaka huu hivyo atakuwa nje kwa dhamana katika kosa hilo la kukutwa na simu.

Awali mshitakiwa huyo alisomewa shitaka hilo ambapo wakili wake Bw.Magafu alipinga shitaka hilo na kutaka hati ya mashitaka ifanyiwe marekebisho kutokana na mawakili upande wa mashitaka kutobainisha kifungu kidogo cha sheria kinachomshitaki mteja wao.

Kabla ya hati ya mashitaka kufanyiwa marekebisho,ilikuwa ikisomeka kuwa mtuhumiwa ametiwa hatiani kwa kukiuka sheria magereza namba 86 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Hali hiyo ilimfanya Bw. Magafu kuiomba mahakama iuamuru upande wa mashitaka kufanyia marekebisho hati hiyo kwa kubainisha kifungu kinachomtia hatiani mshitakuwa kwakuwa sheria hivyo ina vifungu vidogo vitatu.

Pamoja na madai hayo wakili wa serikali Bi. Kaganda alidai kuwa wao wanamshitaki mtuhumiwa kupitia sheria hiyo pamoja na vifungu vyake ambapo Bw.Magafu alipinga kwa kuwa kifungu cha pili cha shera hiyo kinafafanua kosa na cha tatu kinampa nguvu Ofisa wa magereza kuchukua kitu kisichoruhusiwa gerezani na kukiharibu au kukitaifisha.

Kutokana na mabishano hayo Bw.Sanga aliamua kusimamisha kusomewa mashitaka kwa mtuhumiwa na kuuamuru upande wa mashitaka kwenda kuifanyia marekebisho hati ya mashitaka na kisha kumsomea upya mtuhumiwa.

1 comment:

  1. masikini liyumba, kwanini kikwete anakufanyia hivyo? ni wale wanawake uliokuwa unampora tu au na mambo ya igunga yameingia hapo? msalimie babu seya.

    ReplyDelete