01 September 2011

Kiongozi Yanga SC ang'aka

*Walioshinda kesi wasimamishwa

Na Suleiman Mbuguni

MJUMBE wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Theonest Rutashoborwa, amewajia juu wanachama walioshinda kesi ya katiba na kusema kamwe klabu hiyo haiwezi
kurudishwa enzi za ujima za miaka 1960.

Baadhi ya wanachama wa Yanga chini ya Mwenyekiti wao, Salum Ngereza, walikwenda mahakamani kupinga katiba iliyowaingiza viongozi wa klabu hiyo madarakani, kwa kuwa ilikiuka katiba ya mwaka 1968, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 1998.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, kiongozi huyo alisema alishtushwa na wanachama hao kumjumuisha katika Kamati ya Muda iliyoundwa na wanachama hao walioshinda kesi hiyo.

Alisema kamwe hataweza kujiunga na wanachama hao kwa kuwa, kwa kufanya hivyo atakuwa ameugeuka uongozi uliopo madarakani chini ya Llyod Nchunga.

"Nikiwa kama mjumbe halali wa Kamati ya Utendaji ya Yanga niliyechaguliwa kwa kura nyingi mwaka jana, kamwe siwezi kujiunga na wanachama hao, kwanza nitakuwa nimejing'oa mwenyewe," alisema.

Alisema, hata hivyo hukumu waliyoshinda mahakamani tayari wameikatia rufani na mahakama hiyo imeamua kuirudisha TFF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania), kwa kuwa, awali wanachama hao walipotosha ndiyo maana wakashinda kesi hiyo.

Rutashoborwa alisema ana uhakika wanachama hao watakuwa hawana chao baada ya suala hilo kurudishwa TFF, kwa kuwa katiba ya shirikisho hilo, hairuhusu mambo ya soka kupelekwa mahakamani.

Katika hatua nyingine, Rutashoborwa alisema Kamati ya Utendaji ya Yanga imewasimamisha wanachama hao walioshinda kesi, ambao sasa suala lao litapelekwa katika Mkutano wa wanachama utakaofanyika Jumapili.

Rutashoborwa alisema kwamba, hatima ya wanachama hao kwa sasa ipo kwa wanachama ambao ndiyo watakaoamua kuwarudisha ama kuwafukuza kabisa uanachama.

Alisema kamati hiyo imefikia hatua hiyo kutokana na wanachama hao kwenda mahakamani kwa makusudi, huku wakijua kufanya hivyo ni kukiuka katiba ya klabu hiyo, TFF na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA).


No comments:

Post a Comment