Na Zahoro Mlanzi
KAMATI ya Katiba, Sheria na Hadhi kwa wachezaji imetoa ufafanuzi juu ya sakata la Wazee waliofungua kesi ya kuwataka Mwenyekiti wa Yanga, Llody Nchunga na
wenzake waondoke madarakani kwamba, hukumu iliyozidi mwaka mmoja utekelezaji wake lazima yawepo maombi maalum ya kutaka kukazia.
Mbali na hilo, wazee hao wanatakiwa wawasilishe sababu za msingi kwanini tangu hukumu ilipotolewa, walikuwa kimya mpaka washindwe kutekeleza kwa wakati.
Wazee waliofungua kesi hiyo wanaongozwa na Salum Ngereza (Mwenyekiti), Leonard Lwekwama (Katibu), huku mmoja wa wajumbe akiwa ni Abeid Abeid 'Falcon', wakitaka Nchunga na wenzake waondoke madarakani na Yanga iongozwe kwa kutumia katiba ya mwaka 1968.
Akizungumza na kipindi cha michezo cha radio moja jijini Dar es Salaam juzi usiku, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Alex Mgongolwa, alisema kwa kawaida masuala ya mpira hayapelekwi mahakamani, kwani ana imani wana vyombo vinavyojitosheleza kuhakikisha masuala kama hayo, yanamalizwa.
"Hatutaki mambo hayo yapelekwe mahakamani kwani tunajitosheleza, tuna vyombo vya michezo vya kutosha vitakavyoweza kutatua migogoro kama hiyo, suala hilo tayari lipo katika kamati yangu na tutalijadili siku si nyingi," alisema Mgongolwa.
Alisema suala kama hilo ambalo hukumu yake ilitolewa zaidi ya mwaka mmoja, utekelezaji wake lazima kuwepo kwa maombi maalumu yakieleza sababu za kushindwa kutekeleza kwa wakati na kwamba, kama maombi hayo hayakupelekwa, hilo litakuwa suala lingine.
Alisema kamati yake itakutana wakati wowote ndani ya siku tatu zijazo kuanzia jana, ambapo baada ya kukutana wajumbe wote na kulijadili kwa kina, ndipo watajua wachukue uamuzi gani.
"Kwa mujibu wa sheria za nchi huwezi kutekeleza suala kama hilo moja kwa moja, bila kuwepo kwa maombi maalumu na ndivyo taratibu zinavyotakiwa kufuatwa na syoi vinginevyo," alisema Mgongolwa.
Kabla ya suala hilo kufika katika kamati hiyo, wazee wenzao walioongozwa na Katibu wa Kamati ya Muafaka ya Yanga, Ibrahim Omary, waliwaomba kukaa pamoja na kulimaliza suala hilo ili kuepushwa timu yao kufutwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), kwani masuala ya michezo hayaendi mahakamani.
Naye, Nchunga baada ya kutoka kwa taarifa hizo, alisema anashangazwa na wazee hao kwa kukaa kimya na hukumu yao tangu mwaka jana, na kuitoa wakati huu ambapo timu yao imeanza vibaya msimu wa Ligi Kuu Bara.
Nchunga alisema kwamba, wanachama hao hawaitakii mema timu yao na kuiweka katika nafasi ya kutaka kufutwa uanachama na TFF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania) na kwamba tayari, wametoa taarifa polisi.
No comments:
Post a Comment