27 September 2011

Tibaijuka: Mafisadi wa ardhi ondokeni kabla ya kufukuzwa

Na Grace Ndossa

WAZIRI wa Ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka, amewataka watumishi mafisadi wa sekta ya hiyo wanaoyumbisha sheria na kanuni kwa
makusudi kujiondoa wenyewe kabla ya kufukuzwa.

Amesema kutokana na watumishi hao kuisababishia serikali kero na malalamiko bila sababu kutokana na kukiuka sheria, nafasi zao hazipo tena hivyo ni bora wakijiondoa mapema kabla hawajaondolewa.

Waziri Tibaijuka alitoa kauli hiyo Dar es Salaa jana, wakati akifungua mkutano wa sekta ya ardhi kwa watumishi kutoka sehemu mbali mbali.

Alisema kila mtu anatakiwa kuwajibika kuzielewa sheria na kanuni za ardhi popote alipo kazini au nje ya kazi kwa kadri ya uwezo wake na kutoa ushauri stahiki kwa serikali kupitia viongozi wake.

"Kwa masikitiko makubwa napenda kutamka kuwa kwenye ofisi zetu kuna udhaifu mkubwa katika utekelezaji wa sheria hizi.

Watumishi wa sekta hii wasio waadilifu wamekuwa wakiziyumbisha sheria na kanuni hizi kwa makusudi, napenda niseme hapa leo kuwa waliozea tabia hiyo hatuna nafasi hiyo kwa ajili yao tena, wajiondoe kabla hawajaondolewa,"alisema Prof. Tibaijuka.

Aliwataka wadau wa sekta ya ardhi kujipanga   kuzipatia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta hiyo ili kubadili taswira mbaya iliyojengeka dhidi yao.

Alisisitiza umuhimu wa watumishi wa sekta hiyo kujipanga na kuifanya ardhi kuwa mtaji wa kweli kwa wananchi na wadau wengine wa maendeleo hivyo kubadili muonekano uliojengeka miongo mwao kwa jamii kuwa wao ni mafisadi wakubwa.

Waziri Tibaijuka alisema sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbali zinazoitia aibu na kuwapaka matope watendaji wote licha ya kusababishwa na watu wachache miongoni mwao.

Alitaja baadhi ya changomoto hizo kuwa ni  utoaji wa huduma kwa wateja ulio chini ya kiwango na matarajio ya wanaopewa huduma hizo, ukusanyaji hafifu wa maduhuli ya serikali.

Changamoto nyingine ni ukiukwaji wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo, kutozingatia utaalamu na miiko ya taaluma pamoja na ukosefu wa kumbukumbu sahihi za ardhi na makazi.

Aliwataka watumishi walioshiriki mkutano huo kujitathimini, kujichunguza na kujibainisha binafsi na kitaasisi kwa kiasi gani  anachangia kupunguza au kuongeza changamoto hizo.

"Ni dhahiri kuwa watanzania wanataka huduma bora hawataki migogoro ya ardhi, wanachukia huduma zilizo chini ya kiwango, wanataka kufaidika na ardhi yao pale inapotwaliwa kwa matumizi ya serikali au uwekezaji wa aina yoyote,"alisema Prof. Tibaijuka.

Aliwataka watumishi hao kuwa makini zaidi   kufanya tathimni ya ulipwaji fidia kwa wakazi au wananchi ambao wanahamishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine ili kuondoa malalamiko yanayotokea mara kwa mara.

Kuhusu mji mpya wa Kigamboni alisema ili uweze kuendelezwa unahitaji jumla ya sh.trilioni 11 kiasi ambacho ni kikubwa karibu sawa na bajeti nzima ya serikali.

1 comment:

  1. Mhe. Waziri Tibaijuka, Sisi wanawake na wanaume Watanzania tunakuheshimu sana ila:-
    1. Ulianza vizuri sana kututetea wanawake na ukawa mstari wa mbele kushinikiza uanzishaji wa Baraza la Wanawake wote Tanzania. Ulipopewa "PIPI" ya kwenda UNEP ukatusahau. Ulipomaliza mkataba UNEP tukadhani ungaliendelea na harakati hizo.Ungepewa Nobel ungeendelea na harakati za akina MAMA. Tukastukia umepewa "ANDAZI" ukawa waziri. 2. Ukiwa Waziri usituhadae tena kwa kutamka kuwa utavikomboa viwanja vya wazi huku ukijua karibu viwanja hivi vimerubuniwa na chama tawala vikiungana na madhehebu ya dini n.k. Baadhi vina kila hati kisheria ambazo zilipindwa kwa makusudi na wakuu wa Wizara yako. Mfano viwanja vya mipira, vya maonyesho ya wakulima n.k. Waguse uone! Sana sana utavunja majengo ya Pateli na Juma ambao watakupeleka hadi commercial Court au ICC. Fanya home work kwanza.Ya Mhe. Mangufuli umeyapata? Kwanza nenda kwa Rais, Baraza la Mawaziri, Bungeni, kwa wanasiasa kwa wananchi pata baraka zao. Usifanye masihara. Ni suala tete. Usipoteze muda kuwahadaa Watanzania.Watafuatilia! Wasomaji, mpeni habari huyu mama. Watanzania tunaona sasa!

    ReplyDelete