*Waziri yatangaza 197,polisi 240
*Baharia atoa ushuhuda alichokiona
Na Mwajuma Juma, Zanzibar
KUMEIBUKA utata mkubwa kuhusu idadi ya watu waliokufa katika ajali ya kuzama kwa meli ya MV Spice Islanders, baada ya
Serikali kutangaza watu waliokufa kuwa ni 197, wakati Jeshi la Polisi likisema ni 240.
Mapema akizungumza na waandishi wa Habari Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Bw. Mohammed Aboud Mohammed, alisema watu 816 wamepatikana wakiwemo walionusurika 619 na waliokufa 197.
Alisema maiti 158 zimetambuliwa na ndugu zao, wakati maiti 39 zilizikwa na serikali katika eneo la Kama baada ya kushindwa kutotambuliwa.
Alisema meli hiyo ina uwezo wa kubeba mizigo tani 500 na abiria 600, lakini kumbukumbu zinaonesha abiria waliorodheshwa walikuwa ni 610 na mizigo tani 160.
Akifafanua alisema kuwa meli hiyo baada ya kuondoka katika bandari ya Dar Es Salaam ilichukuwa tani 65 za mzigo na abiria 166 wakiwemo watoto 65 kabla ya kuongeza idadi ya abiria abiria 610 na tani 95 za mzigo katika bandari ya Malindi.
Alisema serikali inaendelea na operesheni ya kutafuta watu, baada ya kujitokeza watu wakidai kuwa hawawaoni ndugu zao.
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar Bw. Mussa Ali Mussa, aliwaeleza wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama alipotembelea kituo cha kuwatambuwa watu walioathirika na ajali hiyo kuwa idadi ya maiti imefikia 240.
Kamishna huyo alimwambia Mkuu wa Jeshi la Polisi Inspekta Jenerali Saidi Mwema na mwenzake wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenelali Bw. Devis Mwamunyange kuwa waliokufa 240.
Bw. Mwema alisema Serikali itaendelea na juhudi za kufanya uchunguzi katika meli iliyozama ili kujua kama kuna watu ndani yake kwa kushirikiana na wazamiaji wa ndani na nje.
Hata hivyo Waziri Aboud alikiri kuwa kuna uzembe umefanyika kwa sababu meli ilikuwa imepakia abiria kupita kiwango chake.Alisema mapema kueleza chanzo lakini Serikali haitakubali lazima itaunda kamati itakayofanya uchunguzi na wale watakaobainika walichangia kufanyika uzembe huo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Alisema serikali imechimba makaburi 134 kwa ajili ya kuzikia maiti ambao hawatatambuliwa na jamaa zao, ambapo maiti 39 zimeshazikwa usiku wa kuamkia jana.
Kwa upande wake Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad ametoa onyo akisema serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kuhusika kutengeneza mazingira ya uzembe katika ajali hiyo.
Baharia aliyesalimika katika meli hiyo Bw. Rashid Said Rashid alisema hadi sasa hajui mabaharia wenzake 11 walipo.
Hata hivyo alisema walifanyakazi kubwa kusaidia abiria lakini Mwenyezi Mungu naye ana nguvu zake kwa sababu yeye binafsi alitumia muda mwingi kusaidia kuokoa abiria hao.
Baharia huyo ambaye amelazwa Hosiptali ya Mnazimmoja alisema kuwa wakati meli hiyo inakaribia kuzama walipishana na Mv Jithada ambayo waliweza kuipa ishara ya kuomba msaada, lakini hawakuweza kufanikiwa.
“Tulijaribu kufanya kila jhitihada za kuweza kuokoka na ilipita meli ya Mv Jitihada na kuipa ishara ya kuomba msaada bila ya mafanikio”, alisema.
Rekodi kutoka Hospitali ya Bububu, Kivunge, Mnazimoja na kituo cha dharura bandarini Malindi zinaoesha watu waliopatikana ni 851 wakati Bububu walipatikana 90, Mnazimmoja 409, Kivunge 57 na katika kituo cha Bandarini 103.
Majeruhi hadi jana kwa mujibu wa rekodi za Hospitali ya Mnazimmoja ni 28 wakati serikali imetangaza kuwepo kwa majeruhi watano katika Hospitali hiyo, mmoja kati yao hali yake ni mbaya na atahamishiwa Dar Es Salaam.
Wakati huo huo Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umetowa msaada wa shilingi milioni 13 kwa ajili ya kusaidia Serikali katika kukabiliana na janaga hilo.
Waziri Aboud alisema kuwa hitma hiyo itaongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohammed Shein na kuwataka wananchi wajitokeze kwa wingi katika kuwaombea dua marehemu hao.
Salamu za rambirambi
Wakati huo huo salamu za za rambirambi zinaendelea kutumwa kwa Rais wa Zanzibar na Dkt. Ali Mohamed Shein, kutokana na ajali ya kuzama kwa meli ya Mv Spice iliyotokea alfajiri ya kuamkia jana.
Salamu za rambirambi kwa jana zilitumwa na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Bw. Alfonso Lenhardt na Ubalozi Mdogo wa China uliopo Zanzibar zilitumwa na Balozi Bi Chen Qiman.
Wengine ni Balozi Mdogo wa India Singal, Balozi Mdogo wa Ujerumani Bw. Hans Koeppel na huku nyingine zikitumwa na mabalozi wa Tanzania wanaofanya kazi nje.
Miongoni mwa Mabalozi hao ni mabalozi hao ni Bi Mwanaidi Maajar, Bw.Peter Kalaghe, Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Oman, Bw.Abdalla Abass Kilima na Bw. Radhia Msuya.
Mabalozi hao walieleza kuwa wanaungana na ndugu zao katika msiba huo na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu maisha mema peponi.
Misaada yaanza
Katika hatua nyingine misaada mbalimbali ilianza kutolewa ili kuwasaidia waathirika. Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), jana lilipatia Serikali Zanzibar sh. milioni 13 kwa ajili ya kusaidia waathirika.
Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa NSSF Bw. Juma Kintu, alikabidhi fedha hizo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bw. Mohammed Aboud, mjini Unguja jana.
Bw. Kintu alisema NSSF imeguswa msiba huo mkubwa kwa taifa na kuchangia kiasi hicho cha fedha ili zisaidie shughuli za mazishi pamoja na hitima.
Wengine waliotoa rambi rambi zao jana ni pamoja na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF).
Baada ya kukabidhi fedha hizo kwa Waziri Aboud, Bw. Kintu aliwaomba watanzania wengine hususan mashirika ya umma na binafsi kuichangia serikali ya mapinduzi Zanzibar.
Kwa upande wake Waziri Aboud ameyashukru mashirika hayo kwa kutoa misaada kwa wakati, hususan katika kipindi hiki kigumu kwa taifa.
Poleni, Poleni na Poleni ndugu zetu, watoto wetu, kaka zetu, dada zetu na wote waliopatwa na msiba huo. Msiba huo ni wetu sote Mungu awape faraja inayoweza kuhimili wakati mgumu kama huu.
ReplyDeleteNatoa rambirambi zangu kwa ndugu na jamaa wote waliofiwa na jamaa zao katika ajali ya Meli iliyozama katika Kisiwa cha Pemba nawaombea marehemu wote Mungu awaghafirie dhambi zao na awalaze mahana pema Peponi. Na nawaombea shifaa njema kwa wote waliopatwa na madhara mwilini na waliopoteza mali zao Mungu awanusuru na awajaalie shifaa haraka na awariziki kheri zaidi ya ile waliopoteza. Napenda kutoa tahadhari kwa Wahusika wote wanaochukua jukumu la USALAMA wa wasafiri wa aina yoyote ile inayotumika nchini ikiwa ni ya Bara au Bahari au Angani. Wakumbuke kuwa maisha ya wasafiri iko katika jukumu lao na nijuu yao kuhakikisha kuwa hakuna upendeleo wa kusaidia mtu yoyote kama nafasi zimeisha kamilika maana yake hakuna nafasi tena ya kujaza watu kama Nzige na baadae kusababisha mauwaji ya makusudi. Kesho kwa Mungu utaulizwa kwa nini umeuwa watu Barii hawana makosa yoyote. Kumbuka kuwa utateseka hapa Duniani na kesho Akhera utakuwa katika Jahamu As Saira.
ReplyDeleteAsanteni sana ndugu yenu Hilal Masaud Aljabri kutoka Sultanate of Oman.