28 September 2011

Helkopta Chadema yavuruga Igunga

*Yavunja mkutano CUF, Mbowe aonya polisi
*Watu waikimbilia kwa baiskeli, pikipiki
*CUF yaituhumu CCM kuhonga chakula, sukari
*Hatimaye nayo kufanya kampeni kwa helkopta


Benjamin Masese na Peter Mwenda, Igunga

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana kilianza kutumia helkopta katika mikutano yake ya
kampeni za ubunge katika Jimbo la Igunga na kusababisha baadhi ya mikutano ya vyama vingine vinavyoshiriki kampeni hizo kuvunjika.

Helkopta hiyo inayoendeshwa na Kapteni Paul Denge iliwasili saa 6:00 mchana katika kiwanja cha Shule ya Msingi Choma cha Nkola na kusababisha walimu na wanafunzi kuvunja vipindi vya masomo kushuhudia chopa, pia wananchi waliikimbilia kwa baiskeli na pikipiki, kitendo kilicholazimisha walinzi wa Chadema kufanya kazi ya ziada kuzuia wananchi walionekana kutaka kuishika na kupiga picha.

Wakati Chadema kikianza kutumia helkopita hiyo na kupata wananchi wengi kwenye mikutano yao, Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana kilikuwa kimesimamisha kampeni kusubiri helkopita zake mbili ambazo zilitarajiwa kuwasili muda wowote, zikitokea Dar es Salaam.

Nacho Chama cha Wananchi  (CUF), kilikutana na waandishi wa habari na kuwaeleza nia ya kuleta chopa kama hiyo, ili kuwafikia wananchi katika maeneo ya jimbo hilo ambalo kijiografia limekuwa na miundombinu isiyopitika kirahisi.

Mara baada ya helkopita hiyo kuwasili, iliwachukua viongozi wa Chadema, akiwemo Mwenyekiti, Bw. Freeman Mbowe, mgombea ubunge Bw. Joseph Kashindye na mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Morogoro, Bi. Susan Kiwanga pamoja na waandishi wa habari na kuelekea katika kijiji cha Chabiso.

Katika Kijiji cha Chabiso, CUF walikuwa wafanye mkutano eneo hilo lakini baada ya kukimbiwa na wananchi wote waliamua kuvunja mkutano na kuondoka.

Akizungumza katika mkutano kijijini hapo, Bw. Mbowe alisema CCM imekabwa kila kona na safari hii haitatoka, kisha akawataka wananchi kufumbua macho kwa kuwa saa ya ukombozi imefika kwani wameteseka ndani ya miaka 50 bila mafanikio.

“Nawaambia ndugu zangu Chadema imeikamata CCM kweli kweli hadi kufikia hatua ya kutuogopa, safari hii tutabanana na ninawahakikishia hawatoki, tumejipanga kupambana nao. CCM inaogopa sana Chadema ndiyo maana mnasikia kila siku kwamba wanasema chama chetu ni cha fujo, siyo kweli wameona tunakubarika kwa Watanzania roho imeanza kuwadunda,” alisema.

Aliwataka wananchi hao kuwa wanakabiliwa na mtihani mkubwa ambao hivi sasa Watanzania wote wameelekeza macho na masikio yao kwao, kusikia wataamua nini juu ya hatma ya kupata kiongozi atakayewasaidia matatizo yanayowakabili.

“Nimepata taarifa kwamba kuna matatatizo makubwa yakiwemo maji, zahanati na barabara, lazima mfanye maamuzi mazuri, CCM hii ni ya matajiri ambao wanawakumbuka kila uchaguzi unapofika lazima muonyesha miaka 50 ya uhuru wa Tanzania wameshindwa kumaliza kero zenu.

…Lakini pia nimesikia hapa kuna chakula cha msaada kinagawiwa, hizi ni fedha zenu si za CCM, kama wanavyopita humo wanawadanganya…kama kuna mwanachama wetu yeyote atakayenyimwa atoe taarifa kwa viongozi wetu haraka, kwa sababu ni haki yenu kupata chakula,” alisema.

Pia Bw. Mbowe amelionya Jeshi la Polisi na kulitaka likae pembeni ili lisiharibu uchaguzi kwa kuisaidia CCM kwa imekuwa kawaida askari hao kufanya kazi kwa kuagizwa na kutumika bila kufuata sheria na kanuni ingawa nao huumia kwa kupata manyanyaso ndani ya jamii.

“Nalionya jeshi la polisi liache mara moja kusaidia CCM katika uchaguzi huu, watuachie tupambane, hatutakubali kabisa uonevu kwa sababu ninyi ni wataalamu wa kuchakachua matokeo,” alisema.

Alisema kuwa kumekuwepo na tabia ya polisi kuisadia CCM katika baadhi ya chaguzi na kuwataka kulinda raia na kuepuka kutumiwa na vyama vya siasa, na kwamba anaamini haki na uhuru ukizingatiwa lazima Chadema itapiga bao tatu bila.

Aliwata vijana kujitokeza kupiga kura na kuhamasisha wazazi wao kushiriki, na kukaa mita 100 kutoka vituoni baada ya kupiga kura.

Kwa kutumia usafiri huo, Chadema jana ilifanya mikutano katika kata saba zikiwemo Chibiso, Igurubi, Mwamakoma, Iborogelo, Sunguzwi na Nkinga ambapo leo kitaendelea katika kata za Kinungu, Itunduru, Mwamashinga, Mwamashimba, Mbutu, Isakamaliwa, Kining'inila na Choma.

CUF yaituhumu CCM

Chama cha Wananchi (CUF) kimeituhumu Serikali ya CCM kuwa inataka kugawa chakula cha msaada na sukari kwa wananchi siku mbili kabla ya kupiga kura katika uchaguzi mdogo wa mbunge wa Jimbo la Igunga kama rushwa ili wakipigie kura CCM.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF-Bara, Bw. Julius Mtatiro akizungumza na waandishi wa habari jana alisema serikali ya CCM imepakia shehena ya sukari kwenye malori saba na chakula cha msaada kwa ajili ya kugawa katika kila kaya katika Jimbo la Igunga Septemba 30 na Oktoba Mosi ikiwa siku moja kabla ya kupiga kura.

“Waache wananchi wapige kura baadaye waendelee kugawa chakula cha msaada, CUF tumejipanga vya kutosha kuzuia, tutayakamata magari hayo na kutawaita waandishi wa habari, hawatagawa mahindi katika jimbo hili Septemba 30 na Oktoba Mosi, hili tutalidhibiti kwa sababu tumeshalijua, hatuwezi kukubali haki za Watanzania kupotea kwa ajili ya kilo moja ya sukari,“ alisema Bw. Mtatiro.

Alisema kama wananchi wamekaa na njaa kwa muda wote bila kufa hawawezi kufa kwa siku moja ambayo kunafanyika uchaguzi kwa sababu hiyo, na kufafanua kuwa hii ni rushwa ya waziwazi na kuitaka Tume ya Uchaguzi kushughulikia suala hilo kwa kuzuia.

Mafunzo ya Janjawidi'

Pia Bw. Mtatiro alisema vijana wa CCM wamemaliza mafunzo yao katika kambi Shinyanga “Janjawidi’ ili kutengeneza vitisho kwa wananchi hasa katika yale maeneo ambayo hawaungwi mkono katika kata 19 kati ya 26 za Jimbo la Igunga ili watu waachwe na majereha baada ya uchaguzi.

Alikitaka CCM ikubali kuliachia Jimbo la Igunga kwa sababu wamebanwa katika kila kona kwani wanayo majimbo lukuki katika nchi nzima ambayo yanawatosha na kuliomba Jeshi la Polisi kuchukua hatua za kuwathibiti kabla ya kuleta madhara.

Alisema CUF itachukua majina yote ya wapiga kura na kuingiza kwenye kompyuta ili kukabiliana na ujanja wa CCM kuondoa majina hayo siku ya kupiga kura na kubandika mengine ili kuwanyima nafasi wale wenye mwelekeo kwa upinzani.

Bw. Mtatiro alisema Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Bw. John Tendwa aache kuingilia uchaguzi wa Igunga pale aliposema uchaguzi huo usimamishwe kwani anatakiwa awaachie Tume ya Uchaguzi (NEC).

Pia alikitaka CHADEMA kiaache kukifuata chama hicho katika mikutano yake ya kampeni kwani kufanya hivyo ni kutibua mbinu za ushindi ilizojipangia katika uchaguzi wa Igunga.

“Tunaomba wenzetu wa Chadema waache kutufuata fuata katika mikutano yetu, mimi mwenyewe nimekutana nao mara nne, hakuna haja ya kuanza kufuatiliana wasifuate siasa za CCM wanatuma usalama wa taifa kutufuatilia wakiacha kuzuia twiga na nyara za serikali zikisafirishwa,” alisema Bw. Mtatiro.

Alisema tunahitaji baada ya uchaguzi wananchi wa Igunga waishi kwa amani na utulivu, wasiachwe wamekufa au kujeruhiwa wakati bado shida zao za maji, afya, elimu na maisha bora yakiwa kitendawili.

Bw. Mtatiro alisema katika maandalizi ya mwisho ya CUF imeongeza nguvu kwa wabunge wengine 13 kuwasili katika Jimbo la Igunga kummwombea kura mgombea wao Bw. Leopold Mahona.

Alisema kwa mara ya kwanza CUF itatumia helkopta katika siku nne zilizobaki ili kurahisisha mgombea wao kuwafikia wananchi kwa urahisi baada ya kuona gharama zake ni za kawaida ambako wanatarajia kufanya mikutano 16 kwa siku katika vijiji 96 vya Jimbo la Igunga.

Akijibu tuhuma hizo Katibu wa Fedha na Uchumi wa CCM ambaye pia ni Meneja wa Uchaguzi wa Igunga, Bw. Mwigulu Nchemba alisema hakuna mpango wala mzigo wa sukari unaopelekwa Igunga kwa ajili ya kugawa.

Alisema si kweli CCM kuandaa vijana (Janjawidi) kwa ajili ya kufanya fujo na kama wamewaona hao ni vijana wa chama na kuhusu chakula, kilianza kugawiwa kabla ya kampeni kuanza na tarehe hizo chakula kitagawiwa kama ilivyo sehemu nyingine za Iramba na kwingineko kwa uhaba wa chakula.

7 comments:

  1. hip hop hureeeeeeeeyyyyyyyyyyyyyy!!!! Sisiemu mavi yanagonga chupi yanarudi ndani!!!!

    ReplyDelete
  2. Tunaomba wanaigunga mbadilike safari hii

    ReplyDelete
  3. CUF hamna haja ya kuzuia chakula cha msingi ni kuwaelimisha wananchi kuwa chakula hicho si hisani kutoka CCM bali ni haki yao kwani kinatokana na kodi yao wenyewe.

    ReplyDelete
  4. CCM hoi,kazi kwenu watu wa Igunga

    ReplyDelete
  5. C.c.m Mmekwisha Na Ufisadi Wenu Nchi Ni Ya Chadema Kazi Ni Kwenu

    ReplyDelete
  6. Mataji wa Maskini ni kura yake wana igunga tunawategemea mtoe dira ya mabadiliko nchini

    ReplyDelete
  7. Muwe macho wanaigunga maana saa ya ukombozi imewadia! Ni CHADEMA tuuuuuu!!!,la sivyo MTAZIDI KUVUMILIA KUWA WANAIGUNGA ....,badala ya...KUJIVUNIA KUWA WANAIGUNGA! na JAMES JOSEPH JAMES wa ILBORU SEKONDARI (R-CHUGA)!

    ReplyDelete