Na Rehema Maigala
WACHEZAJI wa timu ya soka ya 'Aston Villa' ya Kigogo, Dar es Salaam juzi wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kujibu shitaka la
kufanya fujo.
Ilidaiwa Mahakamani hapo kuwa, Septemba 14 mwaka huu saa 9 alasiri, washitakiwa walimsumbua na kumfanyia fujo askari mwenye namba D.7590 Koplo Habibu, ambaye alikuwa doria katika eneo ambalo timu hiyo inafanyia mazoezi.
Pia washitakiwa hao kwa pamoja, walimpiga mawe sehemu mbalimbali katika mwili wake Jeremia Mhando, ambaye alikuwa anawakataza wasimfanyie fujo askari huyo.
Mahakama hiyo iliwataja washitakiwa hao kuwa ni Peter Lihamba (33), Saidana Nyalise (14), Peter Selestine (18), Simon Masigata (25), Amiri Abdallah (18), Fortunatus Fande (25) na Faridi Isihaka (23).
Washtakiwa wengine ni Kim Mkamba (25), Nyarise Umary (40), Ally Hemed (25) na Mrisho Hemed (24) ambao wote ni wakazi wa jijini Dar es Salam.
Kesi hiyo ilikuwa mbele ya Hakimu Suzan Mkabwa na Mwendesha Mashitaka, Inspekta wa Polisi Benedict Nyagabona.
Hata hivyo kesi hiyo imehairishwa hadi Oktoba 10, mwaka huu na washitakiwa wamerudishwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
No comments:
Post a Comment