Na Edmund Mihale
TUME ya Uchaguzi nchini (NEC) imetoa tamko la kulaani vitendo ambavyo imedai kuwa ni vya kihuni na visivyo vya kiistarabu vinavyofanywa na baadhi ya wanachama wa
vyama vinavyoshiriki katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Igunga kwa kuwa ni kinyume na sheria ya Uchaguzi.
Tamko hilo la NEC limekuja huku zikiwa zimebaki siku tano kuanzia jana kufanyika kwa uchaguzi katika jimbo hilo.
Akizungumuza katika mkutano wa waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Prof. Amon Chaligha aliwataka wote wanaofanya na kuendeleza vitendo hivyo kuacha mara moja kwa ajili ya usalama wa taifa na ustawi wa wananchi wa Jimbo la Igunga.
Alisema kuwa tangu kuanza kwa kampeni hizo msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo amepokea malalamiko mbalimbali ambayo yanaonesha kwamba baadhi ya vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo haviendeshi kampeni kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi.
Alisema kuwa malalamiko yaliyowasilishwa kwa Msimamizi wa Uchaguzi katika jimbo hilo ni kumwagiwa tindikali, kudhalilishwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Bi. Fatma Kimario na kujeruhiwa kwa kukatwa mapanga.
Alisema kuwa malalamiko hayo yalijadiliwa na na wajumbe wa Kamati ya Maadili ngazi ya jimbo na maamuzi yaliyotolewa na kamati hiyo ni kwamba kwa kuwa masuala hayo yalifikishwa mahakamani, mhimili huo umeachwa uendelee kuyashughulikia bila kuingiliwa.
Alisema kuwa muda mfupi baada ya malalamiko hayo, pia matukio ya kurushiana risasi, kuwa na silaha katika mikutano ya kampeni, kuharibu mali, yakiweno magari; kutumia lugha za matusi na vitisho katika mikutano ya kampeni, kutumia lugha za kikabila badala ya Kiswahili katika mikutano ya kampeni za uchaguzi pia yameripotiwa.
Alisema kuwa baada ya msimamizi wa uchaguzi kupokea malalamiko hayo aliwasilisha katika Kamati ya Maadili ya Uchaguzi Ngazi ya Jimbo kwa mujibu wa maadili ya Uchaguzi wa 2010 ambayo inaundwa na wajumbe kutoka vyama vyote vya siasa vinayoshiriki uchaguzi huo.
"Baadhi ya matukio hayo tayari yamewasilishwa katika Kamati ya Maadili ya Uchaguzi ngazi ya jimbo kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343 na maadili ya uchaguzi ya 2010 ambapo yatajadiliwa na kutolewa maamuzi.
"Ni mategemeo ya tume kwamba wale wote wanaoshiriki katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga na kata 22 katika halmshauri mbalimbali nchini wataendelea kuendesha kampeni zao kwa kuzingatia sheria za uchaguzi maadili ya uchaguzi na maendeleo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi," alisema Prof. Chaligha.
Alisema kuwa tume hiyo inawaomba wananchi wa Jimbo la Igunga na kata 22 zinazofanya uchaguzi mdogo kuendelea kushiriki katika mikutano ya kampeni za uchaguzi kusikiliza sera za vyama vya siasa kuzipima na ifikapo Oktoba 2, mwaka huu kujitokeza kwa wingi na kupiga kura.
Mbona hii tume ya maadili haijazungumzia suala la kufumaniwa pia? Hilo pia ni ukosefu wa nidhamu na maadili na kiongozi/kada kama hawa walitakiwa kupigwa marufuku kuendelea kuwepo kwenye kampeni Igunga.
ReplyDelete