23 September 2011

CCM yadai Chadema imengiza makomandoo

*Mukama asema wana ushaidi, wameripoti polisi
*Mbowe ajibu hizo ni tuhuma za kiongozi dhaifu
*Mnyaa ataka Igunga wakatae CCM wapate maendeleo


Na Waandishi Wetu, Igunga

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Wilson Mukama amekigeuzia kibao Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa kimewaingiza Igunga mabaunsa 35 waliopata mafunzo ya kikomandoo nje ya nchi ili kufanya vurugu na kudhuru maisha ya watu.

Madai ya Bw. Mukama ambaye anadai anao ushahidi wa kutosha, yamekuja ikiwa ni siku chache baada ya Chadema kudai kuwa CCM imewapeleka vijana wilayani Igunga na kupata mafunzo ya namna hiyo ili kufanya vujo wilayani humo na kuwatisha wafuasi wa vyama vya upinzani.

Kwa mujibu wa Bw. Mukama makomandoo hao wamesambazwa na Chadema katika kata tano za Igunga na kwamba tayari CCM imeshatoa taarifa kuhusu watu hao katika vyombo vya usalama kwa hatua zaidi, lakini Msemaji wa Polisi katika masuala ya Kampeni, Igunga, Bw. Isaya Mungulu alisema hana taarifa hizo.

Bw. Mukama katika mazungumzo yake na waandishi wa habari alizidi kulia na Chadema akikifananisha na chama cha magaidi cha Renamo cha Msumbiji kilichokuwa msituni kitaka kuchukua madaraka kwa nguvu kwa njia ya mapigano.

Alisema makomandoo hao walipata mafunzo ya ukomandoo katika nchi za za Libya, Israel na Pakstani lakini hakusema imewezekanaje makomandoo kuingizwa wakati kuna vyombo vya ulinzi na usalama.

Alitaja kata ambazo alidai makomandoo hao wamefichwa na idadi yao kwenye mabano kuwa ni Itobo (4), Burede (5), Isakamaliwa (9) Bukene (9) pamoja na Chamacholo (6).

Bw. Mukama alisema hali hiyo inaonyesha kuwa CHADEMA kinataka Tanzania iwe na siasa kama ya nchi zisizo na demokrasia.

Alivitaka vyombo vya habari kuwa waungwana kuandika habari bila upendeleo wala ushabiki na kuonya kuwa kuandika habari zinazoegemea upande wowote ni kudanganya umma.

Alisema CCM inao ushahidi wa barua inayodaiwa kuandikwa na kiongozi mmoja wa Chadema kuonesha kuwa makomandoo hao tayari wapo Igunga na CCM imechunguza na kubaini ni kweli.

Alisema uongozi wa Chadema hauna tofauti na ule wa Kiongozi anayetakiwa kuondoka madarakani nchini Libya, Kanali Muamar Gaddafi wa kuweka watoto wake na jamaa katika madaraka, hivyo Watanzania wasikubali kupigia kura chama hicho.

Kuhusu kampeni za chama hicho, Bw. Mukama alisema zimekwenda kama zilivyopangwa na wanashambulia kama nyuki katika sehemu zote za jimbo hilo na kwamba wananchi wanawaunga mkono na kuahidi kukipigia kura chama chake.

Alisema CCM imeondoa umaskini katika Jimbo la Igunga ambako mwaka 1994 ilikuwa wilaya ya mwisho katika mkoa wa Tabora lakini kwa sasa ni ya kwanza katika sekta mbalimbali.

Mbowe ajibu tuhuma

Akijibu tuhuma hizo, Mwenyekiti wa Chadema, Bw. Freeman Mbowe alieleza kusikitishwa na taarifa ambazo alisema si za kweli.

"Mukama ni mtu ambaye ameingia kwenye siasa uzeeni, Chadema haina kundi lolote iliyofundishwa nje ya nchi wala ndani ya nchi.

Kama Mukama anayo orodha na yeye ni Katibu Mkuu wa chama kinachotawala aweke wazi orodha hiyo ili wakamatwe haraka," alisema Bw. Mbowe.

Alisema chama chake hakijawai kufundisha vijana nchini Israel, Libya, Pakistana wala Afganistan na kwamba hayo ni maneno ya kiongozi dhaifu.

"Hayo ni maneno ya kiongozi mwenye hoja dhaifu ndani ya nchama legelege, chenye kuongoza serikali dhaifu, serikali isiyokuwa na kauli moja," alisema Bw. Mbowe.

Alisema uchaguzi wa Igunga ni mdogo na kwamba vyama mbalimbali ikiwemo Chadema vimepeleka watu kutoka maeneo mbalimbali kusaidia kampeni na kwamba hilo ni jambo la wazi kwa kuwa mji huo umejaa watu kila kona.

"Yeye mwenyewe Mukama ameweka kambi katika Kijiji cha Ulemo zaidi ya watu 400 wamefundishwa na tumelalamika, kama kweli wana ushahidi tumeleta makomandoo kutoka nje wakamatwe haraka, vinginevyo aombe radhi Watanzania," alisisitiza Bw. Mbowe

Alisema kauli hiyo ni udhaifu, unyonge na inaweza kutolewa na mtu ambaye anapiga kelele kutisha umma.

Mnyaa wa CUF ainanga CCM

Mbunge wa Jimbo la Mkanyageni, Kusini Pemba (CUF), Bw. Mohamed Habib Mnyaa amesema kama wananchi wa Jimbo la Igunga wanataka maendeleo ya haraka basi wasikipe kura CCM.

Akimnadi mgombea wa CUF, Bw. Leopold Mahona katika vijiji vya Kata ya Nkinga jana, Bw. Mnyaa pamoja na wabunge wengine zaidi ya 21 kutoka Zanzibar wanaoshiriki kampeni za uchaguzi mdogo alisema jimbo lake la Mkanyageni limepata maendeleo ya maji, umeme na barabara kwa asilimia 70 baada ya kuitakaa CCM.

“Katika Jimbo la Mkanyageni tangu liongozwe na upinzani mwaka 1995 wananchi walikuwa hawajawahi kupata barabara za lami na huduma muhimu za kijamii baada ya kufunguka macho na kubaini kuwa miaka 43 ya uhuru walikuwa wamefungwa na kukaa utumwani mwa CCM walikipigia kura CUF,” alisema Bw. Mnyaa.

Alisema CCM kwa miaka yote tangu Uhuru haijawahi wala kuthubutu kuleta maendeleo yaliyopo, na aliwataka wananchi wa Jimbo la Igunga kumchagua Bw. Mahona kwani atakapoingia bungeni atahakikisha anampa mbinu za kuwaletea maendeleo wananchi wa Igunga.

Bw. Mahona alisema Zanzibar zao lao kuu la biashara la karafuu limekuwa msaada mkubwa kwa wananchi, kwani tangu CUF iingie katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa bei imepanda kutoka sh. 2,500 hadi sh. 12,500 kwa kilo moja.

Aliwaomba wananchi hao ili asaidiane naye kuhakikisha zao la biashara jimbo la Igunga ambalo ni pamba linaimarika na wananchi wafaidike kwa kuuza bei nzuri tofauti na hii iliyopo sasa ya sh. 800 kwa kilo.

Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa CUF, Bw. Hassan Doyo alisema CCM imekuwa ikiomba kura kwa unyeyekevu wakipata madaraka hawakumbuki wananchi wake tena, bali hutumia nafasi hiyo kujilimbikizia mali na rasilimali za wananchi.

16 comments:

  1. Siasa yahitaji uzoefu na uelewa mkubwa sana. Ndugu yetu Mukama amejiingiza kwenye siasa uzeeni kwa vyovyote vile hatahimili mikiki mikiki ya siasa. Huyu atapata presha buuure mzee wa watu. Afadhali hata mgosi Makamba lakini huyu ambaye hajawahi hata kugombea ubalozi wa nyumba kumi halafu kapewa Ukatibu Mkuu wa chama kikubwa na chenye wajanja waliobobea kwa kweli shughuli anayo. Hiki ndio kikosi tulichoambiwa kitapambana na mafisadi walioko ndani ya CCM? Pole Mkuu wetu wa nchi huna watu bora walioondoka. Mwingine ndio huyo Mwigulu aliyefumaniwa na mke wa kada mwenzake Lo! CCM tumekwisha.

    ReplyDelete
  2. WASWAHILI HUSEMA"SIKU YA KUFA NYANI MITI YOTE HUTEREZA" CCM MNATAFUTA KILA NJIA YA KUSHINDA. LAKINI POLENI, HAPO HADANGANYWI MTU.

    ReplyDelete
  3. Mukama kwa nini usipumzike!

    ReplyDelete
  4. Mkama mbona unaongea kama mtu mwenye hangover. Juzi ni chama chako kilichomtetea Gadaffi, inakuwaje leo mnamgeuka? Nakushauri rafiki yangu uachane na hizi siasa za CCM. Wewe huziwezi. You are a technocrat sasa haya mambo unayoongea bila kufikiria acha ndugu yangu. Unatuangusha wana Bwiru Boys!

    ReplyDelete
  5. Serikali ilyoikataa bendera ya waasi wa Libya ndiyo hiyohiyo inayodai leo kwamba chadema wana siasa za Gaddafi, hapa nachelea sijui mukama anadhani watanzania hawasomi wala hawana uelewa wowote wa masuala yanayotokea nchini na nje ya nchi, mukama ninakusahuri ondoka huko igunga rudi mtaa wa Lumumba dar upumzike, mtu mzima na tena kiongozi mkuu kabisa unadanganya mchana kweupe namna hiyo? polisi wamekukana,wanasema taarifa zako hizo ni za kupika,jeshi la polisi limezikataa sijui umepeleka wapi ushahidi wako huo labda takukuru kwa marafiki zenu wanaoficha taarifa za mafisadi.

    ReplyDelete
  6. Ni mageuzi tu hata mseme nini. Mnaweza kushinda Igugunga kwa rafu, lakini sahauni 2015. Jitayarisheni kuwa wapinzani na mkubali hivyo. Mmetudanganya vya kutosha nyie ccm. Mafuriko hayazuiliki!Mmetuibia matrilioni ya shilingi sasa yatawatoka puani. Angalia mwenzenu Banda huko Zambia, miguu juu. Wale mafisadi anzeni kurudisha pesa zetu mlizotuibia kabla ya wakati kufika. Kwa maana mtakosa pa kukimbilia.

    ReplyDelete
  7. Hivi Bw. Mukama haelewi kwa kauli yake kuwa anawaeleza Watanzania kuwa Serikali yao haina mapolisi, makachero na wanausalama wenye kutambua kuwa kuna magaidi na makomandoo walioandaliwa kimasomo kuja kawadhuru raia wema? Ina maana CCM ina makachero zaidi ya vyombo vya Srikali? Kama wano huo uwezo , basi wawape mapolisi wataalam wao. Mukama asifanye mambo ya utani. Anaviabisha vyombo vya ualama wa ncchi mbele ya Watanzania.

    ReplyDelete
  8. Jamani hizi kampain tusizindeshe kilevi. Huyu Mkama anaongea kama mlevi. Kuna matatizo gani CCM? Yule mzee mwingine alikuwa anaongea kama chizi. Sasa amakuja mkama anaongea kama mlevi wa ulaka. Yaani katika wanachama wao milioni 5 hamna mwenye akili kuwashinda hawa? Huyu kweli kahitimu elimu ya chuo kikuu? Mbona anaongea kama mtuwa darasa la 7. Nanyie wafanya biashara mnaoichangia CCM angalia pesa zenu zinaishia kwenye ngono na ulevi! Huyo mwingine amefumaniwa akifanya mapenzi na mke wa kada mwenzie gesti Huyu nae alnalewa kupindukia mpaka anazungumza upuuzi asioweza kuhakikisha. Ama kweli wakati ukiwadia hamna wa kugeuza. Nadhani wakati wa ccm kufa umewadia. Wajitayarishe kuzikwa.

    ReplyDelete
  9. Strategically statement ya MUKAMA itakiathiri chama chake mwenyewe kwani anawatia hofu wanachama wa CCM hasa wanawake then siku ya uchaguzi turn out ya wakina mama itakuwa ndogo kwa hofu ya magaidi na makomandoo waliopewa mafunzo kutoka kwa wa taliban, alqaida na hamas.

    Hivi hawa watu wa ccm na siasa zao za everything goes zitafikisha kuzimu hakika.

    ReplyDelete
  10. Watu waliosoma bwiru Boys enzi hizo kama kina marehemu Jaji Fransis nyarali walikuwa na akili. Sasa hivi nashindwa kujitambulisha kama mtu aliyesoma bwiru Boys kwa sababu ya ujinga wa akina Mkama. Kwa kweli watu kama kina Mkama kuwa katibu mkuu wa chama tawala ni janga la kitaifa.

    ReplyDelete
  11. Ukiona Kiongozi Mkuu kama Mukama anatoa matamshi yasio na kichwa wala miguu ya kuwaongopea watanzania na kwamba anashikilia ngazi ya juu katika chama tawala basi ujue kuwa hiyo ndio picha halisi ya Uongozi wa juu wa nchi hii. Kama viongozi wa juu ndio wenye uwezo huo ndio maana nchi hii miaka 50 baada ya uhuru tumevuna uhaba wa maisha bora, reli isiyofanya kazi, matatizo ya maji, umeme, elimu, ufisadi, migomo vyuoni, serikali isiyo na vipa umbele makini,serikali tegemezi ya misaada kutoka nje, na utitiri wa uoza mwingi usiofikirika. SERIKALI YA NAMNA HII YA NINI KUWEPO MADARAKANI? KWA FAIDA YA NANI? KWA UHAKIKA SIO KWA FAIDA YA MWANANCHI WA TANZANIA!

    ReplyDelete
  12. Mimi ningekuwa Mheshimiwa sana wa Ngazi ya juu ktk chama tawala anayesemwa kwa matamko yake yasiyofanyiwa utafiti wa kina kama huyu mwenzetu anayeonekana katika jamii kama amekurupuka kutoka usingizini na kuanza kuwahutubia wananchi mambo ya kwenye ndoto, hakika nisingesita kujivua GAMBA na kuwaachia viongozi walio makini.

    ReplyDelete
  13. Kutapatapa kwa CCM huko

    ReplyDelete
  14. ama kweliujanja mwingi mbele giza!!MUKAMA wee!!!ulipokuwa wizara ya afya ulituletea wendawazimu wako ukiwa na mwafisi wako mkabadili sare za wauguzi na kuitoa cape waliyokuwa wakivaa wauguzi na kutuletea misare yenu ya ajabu,umeyabeba yale na kuja kutua nayo ccm,mzee unawaponza wenzio huko,''YA NGOSWE MWACHIE NGOSWE'',yako wapi sasa?hizo nchi ulizozitaja zikiamua kusema uthibitishe kauli uliyoitoa nguo hazitakubana mkubwa?au ndo ile kauli ya waosha vinywa ambao husema bila mpanglio wowote ule ilimradi limemtoka kinywani,CHADEMA mnamchekea huyo wa nini?mfikisheni panapohusika hata kama hatawalipa kwa udhalilishaji basi akajifunze japokuwa wanajifanya dola ni mali yao,BLOOD BASCKET mkubwa huyo.

    ReplyDelete
  15. Kujifanya ccm wasafi na wako sambamba na sheria na kuivunja kwao ni mwiko sindio?ni chama chenye watu wa tabia zote mbaya huku duniani ee Mungu wasaidie watu wako hao,si wanawake wala wanaume balaa tupu!
    Imagine kufumaniana wao,ufisadi wao,dhuluma wao na kila aina ya matatizo yasiyofaa,na diclair interest kuwa ni ccm pia but from now ccm bye!!!!kwani mwendo si mzuri ndg zangu,hivi hamjui kwamba ulimi uliponza kichwa?
    Sasa basi yangojeni na huyo domo kaya wenu sharubu kama kitu gani sijui,na pengine wenzie walimpa press conference kusudi wapime uelewa wake basi poti akaona aaah hapo sasa watamkoma,kama ndivyo wewe ndo mwenye hilo jukumu MUKAMA?mbona Nnauye asiseme?
    Mura utaisoma namba japo kimya kimya bila kelele habari ndo hiyo,utemi kila mahala sindio eeh?basi hapo umekwama kwa watanzania ndg yangu,chezea Igunga wewe.....UKIRI NA kuomba MSAMAA kwa umma,huyo RAGE wenu alichoweka kiunoni pale nini msomali wa hedi yule..au ndo ule usemi kwamba BATA AKI... KAHARIBU,ILA KUKU ANAKUWA KAJISAIDIA sindio hivyo?
    Nakuja....

    ReplyDelete
  16. MUKAMA...!!kwani ukikaa kimya unapungua nini mzee wewe?hivi kwa akili na mtazamo wa kawaida yanawezekana hayo uliyoyasema?kiukweli mara uatakpoingia kwenye hii kona na kusoma haya maoni ya watanzania mmmhh..
    Naamini umeoa na una watoto walio oa na kuolewa ambao mara kadhaa wamekuwa wakipitia mtandaoni,sijui wakwe zako pande zote mbili na wazazi wenzio pande zote mbili na viongozi wako wa dini wakiyaona haya sijui nafsi na serikali yako ya kichwa vinakupaje mwenzetu wewe?mengine huna hata haja ya kuambiwa tazama mkubwa!!sijui bwana kila mtu na alivyoumbwa na kulelewa ngd yangu kwani dhamana ya hayo uyafanyayo unayo mwenyewe mikononi mwako na kupanga ni kuchagua,zaidi ya yote pengine kinywa kisicho na hekima nilidhani ni mtaani tu kumbe ni hulka yako?POLE WEE....
    dakika sifuri.......

    ReplyDelete