26 September 2011

Barca, Real Madrid zazidi kutesa

BARCELONA, Hispania

MIAMBA ya soka Hispania, timu za Real Madrid na Barcelona imezidi kuchachafya katika mechi za Ligi Kuu ya nchi hiyo, baada ya kuendelea kuondoka na ushindi
mnono dhidi ya wapinzani wao.

Katika mfululizo wa mechi za timu hizo, zilizopigwa usiku wa kuamkia jana mchezaji Lionel Messi, aliendeleza wimbo lake la kuondoka uwanjani na mabao matatu mguuni na kuifanya Barcelona kuondoka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Atletico Madrid.

Naye Cristiano Ronaldo, alipachika idadi kama hiyo katika mchezo ambao timu yake ya, Real Madrid iliyokuwa na wachezaji kumi iliiadhibu Rayo Vallecano kwa mabao 6-2.

Kwa mujibu wa Shirika la Habri la Marekani (AP), katika mtanange uliofanyika kwenye Uwanja wa  Camp Nou, utamu ulikuwa ni kati ya mchezaji mpya wa Atletico Madrid, Radamel Falcao na nyota mara mbili wa Dunia, Messi.

Hata hivyo kwa mujibu wa AP, mshambuliaji huyo mpya wa  Atletico, hakuweza kufurukuta hadi dakika ya 30 huku Messi akiwa ameshazifumania nyavu akiwa amefuata nyayo za David Villa aliyepachika bao la kwanza.

Messi alifanikiwa kulazimisha goli pili ambalo mchezaji Miranda, alijifunga kabla ya kuongeza la tatu ambalo liliifanya Barcelona, kujiweka sawa ili kupata ushindi wa tano mfululizo, ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani dhidi ya wageni wao.

Baada ya bao hilo, Messi tena alipachika mabao mengine mawili dakika za mwisho na hivyo kumpiku Ronaldo, katika nafasi ya mfungaji bora akiwa na magoli manane.

“Ilikuwa ni mechi ngumu ukiangalia jinsi Atletico, walivyocheza lakini tuliwadhibiti vizuri,” alisema Messi, ambaye hadi sasa ameshafunga mabao matatu kwenye mechi tano alizocheza msimu huu.

“Wana timu nzuri sana, lakini tuliwafunga kwa haraka na baadaye tukafanikiwa kudhibiti mchezo,” aliongeza.

Matokeo ya mechi nyingine ya juzi, bao lililofungwa kipindi cha kwanza na Frederic Kanoute, liliipa ushindi wa bao 1-0 Sevilla, dhidi ya timu iliyokuwa na wachezaji 10 Valencia.

Villarreal ikatoka sare ya bao  1-1 na Athletic Bilbao, huku  Basques ikiendelea kuondoka bila ushindi dhidi ya kocha wake mpya, Marcelo Bielsa.

Matokeo hayo yanazifanya Barcelona na Sevilla kubaki nyuma kwa pointi moja dhidi ya vinara wanaoongoza ligi hiyo Real Betis, yenye pointi 12 wakati Madrid imefikisha pointi 10 sambamba na  Valencia.

No comments:

Post a Comment