*Vyaanza kutumia helkopta kukamilisha kampeni zao
*Magufuli aunguruma, aahidi kutoa bajeti maalumu
*Rage apigwa faini 100,000/- kukampeni na bastola
Na Benjamin Masese, Igunga
VYAMA vya CCM na CUF vimefanikiwa kujibu mapigo ya CHADEMA katika kampeni za
lala salama katika Jimbo la Igunga baada ya kuanza rasmi matumizi ya helkopta ili kufikia maeneo mengi zaidi.
Helkopta hizo ambazo juzi zilikwama kufika Igunga, jana ziliwasili kwa nyakati tofauti, ambapo ya CCM iliwasilia asubuhi na kuanza kazi huku ya CUF ikiwasili jioni ikitarajiwa kuanza kazi leo.
Helkopta hiyo ya CCM ilitua katika viwanja vya Sabasaba saa 4:00 asubuhi na kulakiwa na umati wa wapenzi na mashabiki wa CCM na wafuasi wa vyama vingine
Magufuli na bajeti maalumu
Katika mkutano wa CCM, Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli jana alitinga Igunga na kueleza kwamba atatoa bajeti maalumu kwa ajili ya barabara na daraja la Mbutu ambalo limekuwa likilalamikiwa sana na wananchi wa Igunga kwa miaka zaidi ya 10.
Akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni za mgombea ubunge wa CCM jimbo la Igunga, Dkt. Dalaly Kafumu katika viwanja vya Sabasaba, Dkt. Magufuli alisema katika mwaka wa fedha wa 2012/2013 Wizara yake itatoa bajeti maalumu ili kuhakikisha barabara za Igunga zinatengenezwa na kuwa katika hali nzuri tofauti na ilivyo sasa.
Alisema serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi imejitahidi katika upande wa barabara katika Mkoa wa Tabora, na baadhi yake zipo katika matengenezo kwa kiwango cha lami.
Alizitaja barabara hizo kuwa ni ile ya kutoka Igunga hadi Shelui yenye urefu wa Kilometa 110, Tabora hadi Nzega (km. 115) na Tabora hadi Urambo Kilometa 90 ambazo kwa pamoja zimeanza kujengwa kwa kiwango cha lami.
“Hawa wenzetu wanashangaza sana, wakati wanasema CCM haijafanya chochote kwa miaka 50, wanatoka Dar es Salaam kuja na kupita kwenye barabara hii nzuri ya lami hadi Igunga iliyojengwa na CCM, hawa watu kweli wanasema wanachokiamini?”
“Msiwachague wale ambao katika kupitisha bajeti wanatoka, je, watajengewaje barabara?”
“Ndugu wana Igunga, achaneni na uongo wa Chadema na CUF, leo hii mkichagua Chadema, hata wakipata wabunge wengine 10 hawawezi kuitoa CCM madarakani, nawaombeni vyama vyote kura zote kwa Dkt. Kafumu ili akafumue maendeleo ya Igunga,” alisema.
Aidha Dkt. Magufuli alimgeuzia kibao Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) na mgombea ubunge wa chama hicho, Bw. Leopald Mahona kwamba kitendo cha wao kwenda kwenye ufunguzi wa kampeni zao huku wakiwa wamepanda wanyama (Punda) ni kosa kwa mujibu wa sheria za wanyama No. 18 na 19 ya mwaka 2008, sheria hiyo ya ustawi wa wanyama ya mwaka 2008 inazuia kuwatumia wanyama kwa mtindo huo,” alisema.
Awali Dkt. Magufuli aliwaeleza wananchi hao kuwa amekwenda Igunga kama Waziri wa CCM, ambaye ametumwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa wamchague Dkt. Kafumu kwa sababu ana sifa zote za uongozi.
“Nilisikia kuna mmoja wa wagombea anasema mkimchagua atajenga daraja la Mbutu kwa siku 60, wakati daraka hilo lina kilometa tatu, linatakiwa kujengwa tuta kwanza na madaraja mengine matatu, lakini cha kushangaza wakati tunapitisha bajeti hawa wenzetu wa CUF na Chadema huwa wanaondoka nje ya Bunge, sasa nawaambia nikitoka hapa nakwenda kukagua daraja la Mbutu,” alisema.
Naye Mbunge wa Bumbuli Bw. Januari Makamba aliwaeleza wananchi waliofurika katika mkutano huo kuwa dunia nzima imeelekeza macho Igunga, kwamba CCM itaibuka mshindi na kumpeleka Dkt. Kafumu bungeni.
“Dunia nzima inawaangalieni wana Igunga, msituletee mtu anayekwenda kuomba mwongozo bungeni, mgombea wa CCM, Dkt. Kafumu ni mzito kuliko wengine, kuanzia uwezo, uzoefu, usomi na maarifa,” alisema Bw. Makamba.
Vijana Chadema wakamatwa
Katika hatua nyingine vijana watatu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa Chadema walikamatwa na walinzi wa CCM maarufu kwa jina la Green Guard katika mkutano uliofanyika katika uwanja wa mpira Igunga muda mfupi baada ya helkopita ya chama hicho kuwasili.
Tukio hilo lilitokea jana saa sita mchana baada ya Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano ya Umma, Bw. Stephen Wassira
kuwauliza wananchi waliokuwa katika mkutano huo kama watakipigia kura Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo baadhi ya vijana walionesha alama ya 'V' inayotumiwa na Chadema.
Bw. Wassira alilazimika kuuliza kama kuna vijana wa Chadema
na hakuna aliyenyosha mkono, ndipo alishukuru kwa kutokuwepo kwa vijana hao, lakini ghafla walianza kupiga kelele na miruzi na vigelegele kutoka kila kona ya viwanja huku wakitamka 'Peoples Power' kaulimbiu inayotumiwa na Chadema ikimaanisha nguvu ya umma.
Baada ya kelele hizo, walikuwepo walinzi wa CCM ambao hawakufurahishwa na hali hiyo waliwakamata vijana watatu na kuwaingiza kwenye gari lao la ulinzi lenye Namba za Usajili T 479 ABT Toyota Land Cruser Hard Top na kuondoka
uwanjani hapo kwa mwendo wa kasi na kuelekea kusikojulikana.
Baada ya gari hilo kuondoka, vijana wengine waliondoka mkutanoni hapo na kwenda kufunga barabara iendayo Kituo cha Mabasi Igunga ili kulizuia gari hilo lililoteka wenzao.
Kutokana na tafrani hiyo waandishi wa habari walilazimika
kufika Kituo cha Polisi Igunga ili kujua kama vijana waliochukuliwa na Green Guard wamefikishwa hapo lakini Mkuu wa Kitengo cha Tathmini, Ufuatialiaji na Upelelezi wa Makosa ya jinai kutoka Makao Makuu, Bw. Isaya Mngulu hakuwepo
kituoni.
Alipotafutwa kwa njia ya simu alisema kuwa yupo nje ya
kituo na kuomba muda ili kuliwasiliana na kikosi chake.
Ilipotafutwa baadaye alisema kuwa kwa mujibu wa taarifa
alizopata vijana waliokamatwa na CCM wamefikishwa kituoni hapo saa nane mchana.
“Taarifa nilizo nazo vijana hao wamefikishwa kituoni na wengine tuliowakamata maeneo mengine, sielewi hizi siasa zinafanywaje?" alihoji Bw. Mungulu.
Mkutano wa Bw. Wassira haukuwa na ulinzi wa Jeshi la
Polisi kwa kuwa haukuwa katika ratiba ya mikutano
ya kampeni. Polisi walifika katika eneo hilo baada ya
kupata taarifa za kutekwa kwa wafuasi wa Chadema.
Baada ya kumalizika mkutano huo viongozi wa CCM wakiwemo
Mjumbe wa Baraza Kuu la Vijana UVCCM, Bw. Hussein Bashe
pamoja na wabunge wa wawili, Bw. Januari Makamba wa Jimbo la
Bumbuli na Bw. Aeshi Hilaly wa Jimbo la Sumbawanga Mjini
walikwenda katika Ofisi za Chadema kufanya mazungumzo juu
ya tukio hilo.
Viongozi hao walikutana na Katibu Mkuu wa Chadema, Dkt.
Willibrod Slaa na kumweleza suala hilo ambapo aliwataka
waseme vijana hao walipopelekwa.
Wakati mazungumzo yakiendelea vijana walizidi kufika katika ofisi hiyo na kutaka kuwashambulia viongozi hao wa CCM kwa lengo la kulipiza kisasi, huku wakiwataka kuwaonesha vijana wenzao walikofichwa.
Dkt. Slaa alilazimika kuwatuliza na kuwaeleza kwamba wamefika hapo kwa nia ya kuomba radhi kwa kitendo walichokifanya, hivyo hakuna sababu ya kuendelea kuwazonga.
“Vijana wangu hao hawakuja hapa kwa nia ya mbaya, hata hivyo hawana ubavu wa kuja hapa kupamba na Chadema, acheni tuwasikilize. Wameanza kwa kuniomba radhi kwa kitendo walichokifanya kwa wanachama wetu," alisema Dkt.
Slaa.
Mbali ya Dkt. Slaa kuwatuliza, bado walizidi kupandisha
mukhari na jazba wakimtaka Bw. Hilaly aondoke kwenye eneo
hilo na kubaki Bw. Makamba na Bw. Bashe kwani hao wanaoneka
kuwa na uungwana.
Bw. Bashe alilazimika kusimama na kusema: "Kwa hekima ya hali ya juu vijana tunapaswa kuwa watulivu kwani wote ni Watanzania, hatupaswi kugombana kwa jambo ambalo tunalishughulikia, tungekuwa wabaya tusingekuja hapa," alisema na kuongeza:
“Kwanza mimi ni jirani yenu wa hapo Nzega tunataka kampeni
ziishe vizuri ili Igunga tuiache salama, tatizo la vijana
wenzenu waliokamatwa tumeshalimaliza kwa lugha safi, tunakwenda kuwatoa,” alisema na vijana hao kushangilia.
Akizungumza na Majira Dkt. Slaa alisema kuwa siku zote
Chadema haianzishi fujo bali zinaanzishwa na CCM na kuongeza
kwamba ndio maana walifika hapo kuomba radhi na katika
kazungumzo yetu nimewaeleza wawaachie vijana hao na tayari
wako nje.
"Vijana waliokamatwa sijawaona kwa macho yangu na sina
majina yao lakini nasikia wamekamatwa, binafsi nachotaka
wawe huru na sitaki kusikia tena CCM inawanyima uhuru
vijana wangu, nimewaonya," alisema.
Rage apigwa faini
Mbunge wa Tabora Mjini, Bw. Ismail Rage ametozwa
faini la sh. 100,000 kwa kosa la kuhutubia mikutano ya
kampeni za uchaguzi mdogo wa Igunga akiwa na silaha aina
bastola.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Kamati ya Maadili kuketi na
kujadili suala hilo na kufikia hatua hiyo.
Akitangaza faini hiyo jana baada ya kikao kumalizika,
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Igunga, Bw. Magayane Protace alisema
kuwa kutokana na kosa hilo kamati imeamuru kutozwa faini
hiyo na kuonywa kutorudiwa kitendo hicho.
Alisema kuwa faini hiyo imetolewa wakati huo huo ambapo
aliwaonya viongozi na wanasiasa wengine wenye tabia hiyo
kuacha mara moja.
WEWE MHE. WAZIRI WASSIRA UKOJE? UZEE UNA MAZURI NA TAABU ZAKE. WEWE KTK MIKUTANO YA IGUNGA SI UNAHUTUBIA WANANCHI KWA UJUMLA NA WALA SIO WANACCM PEKE YAO? UNATOKA WAPI KUWACHAMBUA WANACHADEMA, WANACUF, WANASAU? WATAKAOKIPIGIA CHAMA CHAKO SIO CCM PEKE YAO. ONA MATUNDA YAKE SASA - VIONGOZI WAKO WA CCM KWENDA KUPIGA MAGOTI(Wazee wazima) KWA CHADEMA. VIJANA AMBAO LABDA WANGEPIGIA CCM KURA WAMEUMIA, POLISI WAMEHANGAIKA. CHUNGA SANA KAULI NA MATAMSHI YAKO. WEWE UNAJIDAI MPINGA FUJO LAKINI WEWE NDIO WA KWANZA KUANZISHA FUJO. OMBA MSAMAHA KWA VIONGOZI WA CCM AU UKAE KANDO NA KAMPENI HIZI
ReplyDelete