23 September 2011

BP yanywea yaomba radhi

Na Gladness Mboma  

KAMPUNI ya Mafuta BP imesalimu amri kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kwa kuiomba radhi serikali, wananchi wateja wote nchini kwa kitendo
chake cha kukataa kufuata amri ya utii iliyotolewa na mamlaka hiyo ya kuuza mafuta kwa bei elekezi, hivyo kusitishiwa leseni.

Mbali na hilo kampuni hiyo ya BP itailipa EWURA gharama zote za kesi ikiwa ni pamoja na kufuta mashauri yake yote yaliyopo mahakamani.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Bw. Engelhardt Kongolo aliyasema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya kuondoa rufani hizo na kuwaomba radhi Watanzania kwa usumbufu uliotokea.

"BP Tanzania imemwelekeza mwanasheria wake kwenda kuziondoa rufani mbili ambazo zilikuwa katika Mahakama ya Tume ya Ushindani (FCT) ili kuendelea kutekeleza wajibu wa kufanya biashara kwa mujibu wa maelekezo ya EWURA," alisema Bw. Kongolo.

Alisema kuwa kampuni hiyo itaanza kufanya biashara zake za kuuza bidhaa na usambazaji wa mafuta kwa kuzingatia muongozo, taratibu na kanuni za EWURA wakati wowote.

Alisema kwa sasa hivi BP Tanzania ambayo Agosti Mosi mwaka huu kwa kushirikiana na BP Africa ambao walikuwa wanamiliki hisa 50 na serikali kumiliki hisa 50, wameshirikiana na kampuni ya Puma kwa ajili ya kutoa huduma hapa nchini.

"Kuanzia Septemba Mosi mwaka huu Kampuni ya Puma ilichukua utawala wa BP Tanzania baada ya kuchukua hisa zao, hivyo kutokana na mabadiliko hayo muda siyo mrefu jina la kampuni litabadilika baada ya kukamilisha taratibu zingine," alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Bw. Haruna Masebu alisema kuwa BP wamepitia yaliyotokea na wamefikia uamuzi wa kuomba radhi serikali na Watanzania kwa yale yaliyotokea.

Alisema kuwa BP walikuwa wamefungua kesi dhidi ya EWURA, lakini watayaondoa mashauri ikiwa ni pamoja na kufuata sheria na maelekezo yote na EWURA wataondoa kesi ili BP waweze kuendelea na biashara.

"Na sisi tumewasamehe baada ya kuomba radhi, kwani wametuambia kwamba wameathirika katika biashara na kwa kuwa wameeleza kwamba watatekeleza taratibu zote na maelezo yetu, hatukuona sababu ya kutowasamehe," alisema.

Naye Mkurugenzi wa Sheria EWURA, Bi. Mariam Grace Maanyu alisema kuwa mamlaka hiyo imewasamehe kwa kuwa wameomba radhi baada ya kupewa mashariti manne, ambayo waliyatekeleza.

Masharti hayo ni kuomba radhi serikali na Watanzania, kufuta kesi zao na kulipa gharama za kesi ilizoingia EWURA.

Alisema kuwa mpaka sasa bado hawajaruhusiwa kufanya biashara mpaka pale watakapopigiwa gharama za kuilipa EWURA ndipo watakaporuhusiwa kufanya biashara.
 
Kampuni ambazo zilifungiwa ni pamoja na BP ni Engen, Oil Com na Camel. Tatu zilitii lakakini BP ilikaidi, kitendo ambacho kiliifanya Ewura kusitisha leseni yake ya biashara kwa miezi mitatu.

No comments:

Post a Comment