07 September 2011

Balozi awataka kikapu kuzingatia elimu

Na Mwali Ibrahim

BALOZI wa Marekani nchini, Alfonso  Lenharnt, amewataka wachezaji wa mpira wa kikapu kuzingatia elimu kwani ndio itakayowawezesha kufika mbali katika mchezo
huo.

Akizungumza mjini Dar es Salaam jana, Balozi Lenharnt, wakati wa ufunguzi wa kliniki ya siku tatu ya mpira wa kikapu, alisema watoto wenye miaka chini ya miaka 16, kwenye Uwanja wa Don Bosco mjini Dar es Salaam.

Katika kliniki hiyo zaidi ya watoto 100 kutoka katika mikoa ya Dar es Salaam, Kagera, Mara, Tabora, Mtwara, Ruvuma, Singida, Zanzibar, Shinyanga, Kigoma, Iringa, Rukwa, Lindi na Kilimanjaro.

Kliniki hiyo inaendeshwa na wachezaji wa zamani wa mchezo huo waliowahi kucheza ligi ya NBA na WNBA nchini Marekani, Tamika Raymond, Dee Brown na Becky Bonner.

Balozi  Lenharnt, alisema wachezaji wengi wa mchezo huo wa Marekani wamefika mbali kimaisha kupitia mchezo huo kutokana na kuwa na elimu ya kutosha kwani inawasaidia hata katika kuingia mikataba mbalimbali.

"Kucheza kikapu bila elimu, ni sawa na bure, lazima uwe na elimu ndipo uweze kufaulu mchezo huu, hata hawa wakufunzi mnaowaona, bila kuwa na elimu, wasingeweza kufika hapa, hivyo zingatieni elimu mtaona mafanikio ya kikapu," alisema.

Hata hivyo, balozi huyo ameihakikishia Tanzania kushirikiana nayo katika kuhakikisha mchezo huo unakuwa na sifa na kutoa ajira kwa vijana kama ilivyokuwa Marekani.

Kwa upande wake mlezi wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Jaji mstaafu Agustino Ramadhani, alisema changamoto inayoikabili TBF ni ukosefu wa makocha wenye mafunzo ya kimataifa.

Alisema walimu wawili ndio waliopata mafunzo hayo hivi karibuni, hivyo amewaomba ubalozi wa Marekani kuwasaidia kutoa mafunzo kwa walimu wa mchezo huo nchini ili kuweza kuleta mafanikio zaidi ya mchezo huo.

"Ukosefu wa walimu waliopata mafunzo ya kimataifa, ndio changamoto kubwa iliyo mbele yetu, mpaka sasa tuna makocha wawili waliopata elimu ya kimataifa, tunawaomba mtusaidie wakufunzi wa kimataifa ili waweza kuwanoa walimu wetu," alisema.

Naye, mdhamini mkuu wa kliniki hiyo,  Meneja Masoko wa Kampuni ya Coca Cola Kwanza kupitia kinywaji cha Sprite, Vida Nasali, alisema kampuni yake itaendelea kusaidia michezo yote kwa watoto.

"Tunadhamini mashindano ya Copa Coca-Cola kwa upande wa soka na hata kikapu kwa lengo la kuhakikisha tunafikisha michezo katika ramani nzuri duniani," alisema Nasali

No comments:

Post a Comment