Na Esther Macha, Mbeya
SIKU mbili baada ya watu watatu kufa kwa kugongwa na lori eneo la Mbalizi wilaya ya Mbeya Vijijini, watu wengine 14 wamekufa baada ya lori aina ya Fuso kupinduka
eneo la Msangamwelu wilayani Chunya.
Ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana wakati gari hilo likitoka mnadani eneo la Mbuyuni wilayani Chunya lilipoteza mwelekeo kutokana na hitlafu ya mfumo wa breki kisha kupinduka.
Maiti wamehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya na baadhi yao walitambuliwa kwa jina moja moja.
Waliokuwa wametambulika na wafanyabiahara wenzao na majina yao kubandikwa nje ya chumba hicho cha kuhifadhia maiti ni pamoja na Galahenga, Mwakalasya, Meshack, Mama Anna na Mwakilasa.
Wengine ni Exavel, Kaloli, Lembo, Masai, Kashinje na Noah. Maiti nyingine tatu zilikuwa zimehifadhiwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Mbeya, Ifisi.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Anacletus Malindisa alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kwamba taarifa zaidi angezitoa baada ya kukamilisha uchunguzi wa awali.
Taarifa kutoka Hospitali Teule ya Wilaya ya Mbeya zilieleza kuwa majeruhi waliokuwa wamelazwa katika hospitali hiyo walikuwa zaidi ya 20. Muuguzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Bi. Rhoda Kasongwa hakupatikana kuthibitisha hilo wala kuwataja majeruhi waliofikishwa katika hospitali hiyo.
Sisi sote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea!!Bwana ametoa na Bwana ametwaa, kila mmoja ana njia yake ya kurejea kwa Mungu
ReplyDelete