Na Mwandishi Wetu
MWANARIADHA atayayevunja rekodi ya Taifa ya sasa ya dakika 59, katika mashindano ya riadha ya kilomita 21 ya Rock City Marathon 2011 yatakayofanyika jijini
Mwanza, Septemba 4, mwaka huu kwa wanaume na wanawake, atapata zawadi ya sh. milioni moja.
Mratibu wa mashindano hayo wa Kampuni ya Capital Plus (CPI), Zaituni Ituja, alisema wameamua kuweka kiwango hicho kama motisha, lakini pia iwe chachu ya kuongeza ushindani miongoni mwa watakaojitokeza kushiriki.
Alisema wigo wa zawadi mwaka huu umepanuliwa zaidi, ikiwa na lengo la kuwatia moyo wanariadha watakaojitokeza ili mashindano hayo yaweze kuzalisha vipaji vya wanariadha nchini.
"Mwanariadha atakayevunja rekodi iliyopo, atazawadiwa sh. milioni moja, ikiwa ni changamoto ya ushindani kwa washiriki, lakini zawadi tumezigawanya kwa wigo mkubwa mwaka huu ili wanaridha wengi wafarijike na ushiriki wao," alisema Zeituni.
Akifafanua mgawanyo wa zawadi katika mashindano hayo, Zaituni alisema washindi wa kilometa 21 watapata sh.500,000 kwa wanaume na wanawake, na watakaoshika nafasi ya pili watapata sh. 300,000.
wanariadha watakaoshika nafasi ya tatu watapata sh. 200,000, wakati nafasi ya nne hadi 12, kila mmoja atapata sh.90,000 na watakaoangukia katika nafasi ya 13 hadi 50, kila mmoja ataondoka na sh. 30,000.
Alisema washindi 21 wa mbio za kilometa 5, kilometa 3 kwa walemavu, kilometa 3 za wazee na kilometa 2 kwa watoto watazawadiwa sh. 25,000, kila mmoja kama kifuta jasho.
"Kiujumla tumekuwa na maboresho makubwa katika zawadi kwa kuongeza wigo wa watu wanaozawadiwa, lengo letu ni kuongeza hamasa kwa wote watakaoshiriki ili tuendelee kuamsha ari ya ushiriki na kuibua vipaji vya riadha nchini," alisema.
Zaituni alisema mpaka sasa tayari mikoa 14 imeonesha nia ya kushiriki na ni faraja kwao na hiyo inathibitisha kukua kwa mashindano hayo kila mwaka na kuonesha ushindani mkubwa.
CPI inaandaa mashindano hayo kwa mara ya tatu, ambapo ya kwanza yalifanyika mwaka 2009, yataanzia Uwanja wa CCM Kirumba kuelekea njia tofauti za Jiji la Mwanza na kumalizikia katika uwanja huo.
Alisema mashindano ya mwaka huu yamedhaminiwa na Geita Gold Mine, Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), New Africa Hotel, Mfuko wa Pensheni wa Taifa (PPF), Mfuko wa Taifa wa
Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bank M, MOIL, New Mwanza Hotel, Shirika la Hifadhi ya Wanyapori Tanzania (TANAPA) na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).
Alisema fedha zitakazopatikana kutokana na fomu za usajili, zitapelekwa katika mfuko wa kuwasaidia watu wenye ulemavu mkoani Mwanza.
Fomu kwa ajili ya kujisajili zitapatikana Ofisi za uwanja wa CCM Kirumba, Ofisi za CPI- DSM, Makao Makuu ya Chama cha Riadha Tanzania (RT) Dar es Salaam, Ofisi za MRAA Mwanza.
Pia, zinapatikana katika tovuti ya www.rockcitymarathon.blogspot.com or info@capitalplus.co.tz.
No comments:
Post a Comment