MILAN, Italia
TIMU ya Inter Milan inakaribia kufikia makubaliano ya kumpeleka mchezaji wake, Samuel Eto'o, katika klabu ya Anzhi Makhachkala ya nchini Russia, ambapo uhamisho
huo utaweza kumfanya Mcameroon huyo kuwa, ghari kuliko wachezaji wote duniani.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Marekani, Anzhi inatarajia kumpa Eto'o mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya pauni milioni 20 kwa kila mwaka, kiasi ambacho kitakuwa kimezidi pauni milioni 12, anazolipwa Cristiano Ronaldo katika klabu ya Real Madrid ,na pauni milioni 10.5 anazolipwa Lionel Messi katika klabu yake ya Barcelona.
Shirika hilo liliripoti kuwa, kwa hivi sasa Inter Milan inajadiliana na maofisa wa Anzhi mjini Milan ili iweze kupewa pauni kati ya milioni 20 na 30 ili imwachie mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30.
"Tupo karibu mno kukubaliana, tunaweza kufikia makubaliano kati ya leo, kesho ama wiki ijayo," alisema mwakilishi wa Anzhi, German Tkachenko katika mahojiano na Shirika la Habari la Italia (ANSA).
Mwakilishi huyo alisema kuwa, juzi Eto'o alikutana na maofisa wa Anzhi mjini Milan.
Timu ya Anzhi, ina maskani yake katika Jimbo la Dagestan lililopo Kusini mwa Russia inamilikiwa bilionea muuza mafuta, Suleiman Kerimov.
Katika orodha ya sasa ambayo inatolewa na jarida la Forbes la Marekani kuhusu watu matajiri duniani, Kerimov anakadiliwa kuwa na mali zenye thamani ya dola bilioni 7.8, fedha ambazo zinamfanya awe katika nafasi ya 118 sawa na Waziri Mkuu wa Italia na familia yake, ambaye pia ni Rais wa AC Milan, Silvio Berlusconi.
No comments:
Post a Comment