19 August 2011

Stars, Algeria kupigwa Mwanza

*Yanga, Simba zapata pigo

Na Mwandishi Wetu

MECHI ya mchujo ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN), zitakazofanyika mwakani nchini
Equatorial Guinea na Gabon, kati ya timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) na Algeria (Desert Warriors), itachezwa Septemba 3, mwaka huu jijini Mwanza.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema  mechi hiyo ilipangwa kuchezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wambura alisema uamuzi wa kuihamishia mechi hiyo mkoani Mwanza, umefanyika baada ya jana kupata barua kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, ikiwaeleza kuwa Uwanja wa Taifa utafungwa kwa ajili ya matengenezo.

Alisema kutokana na taarifa ya Wizara, uwanja huo utakuwa katika matengenezo baada ya kuharibika wakati wa mechi za Kombe la Kagame iliyofanyika mwanzoni mwa mwezi uliopita.

 Msemaji huyo wa TFF, alisema mbeli na mechi hiyo kupelekwa CCM Kirumba, pia timu za Yanga na Simba, zitaathirika.

Miamba hiyo ya soka nchini iliomba kuutumia uwanja huo katika mechi zake za Ligi Kuu Bara.

"Tayari leo (jana), tumeziandikia rasmi klabu za Simba na Yanga kuzifahamisha kuhusu uamuzi huo wa Wizara, hivyo zitafute viwanja vingine kwa ajili ya mechi zao za ligi," alisema.

Hatua hiyo ya uwanja kufungwa, kutailazimisha TFF ifanye mabadiliko kwenye ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom kwa kuzingatia viwanja ambavyo klabu za Yanga na Simba zitakuwa zimeamua kuvitumia.

Wambura alisema mabadiliko hayo, yataziathiri timu za African Lyon, Azam, JKT Ruvu, Moro United na Villa Squad ambazo licha ya kutumia Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam kwa mechi zao, zilipanga mechi zao za nyumbani dhidi ya Simba na Yanga, zichezwe Uwanja wa Taifa.

Kwa sasa msimamo wa wamiliki wa Uwanja wa Azam, ni klabu za Yanga na Simba kutoutumia kwa vile uwezo wake wa kuchukua watazamaji ni mdogo.

Wakati huo huo, Mwandishi Addolph Bruno anaripoti kuwa, kikosi cha vijana wenye miaka chini ya 17 'Serengeti Boys', itashuka uwanjani kesho kujipima nguvu na vijana wenzao wa Azam FC, jijini Dar es Salaam.

Serengeti Boys inajiandaa na michuano ya vijana ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), itakayochezwa mwishoni mwezi huu mjini Nairobi, Kenya.

Kocha Mkuu wa timu za Taifa za vijana chini ya umri wa miaka 23 na 17, Mdenmark Kim Poulsen, jana alisema mechi hiyo itapigwa kwenye Uwanja wa Azam Fc uliopo Chamanzi, Dar es Salaam.

Kocha huyo alisema programu yake ni kufanya mazoezi kila baada ya wiki mbili na kucheza mechi za kirafiki na timu mbalimbali za vijana za nyumbani, na kutafuta mechi za kimataifa za kirafiki.

Poulsen alisema kikosi chake kwa kisasa kimebakiwa na wachezaji 24, badala ya 37 waliochaguliwa awali.

No comments:

Post a Comment