Kuanza na 'wanajeshi' katika ufunguzi
Na Zahoro Mlanzi
WAKATI miamba ya soka nchini, timu za Yanga na Simba zikiendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo wa Ngao ya Jamii utakaopigwa Agosti 17, mwaka huu, miamba hiyo itakutana tena Oktoba 29, katika mfululizo wa michezo ya Ligi Kuu Bara.
Pamoja na timu hizo kukutana mwezi huo, pazia la ligi hiyo litafunguliwa rasmi Agosti 20, kwa kupigwa michezo mingine mitano, tofauti na Simba yenyewe itaanzia ugenini kwa kuumana na JKT Oljoro, huku Yanga ikiwa nyumbani kucheza na JKT Ruvu, ambapo michezo hiyo itapigwa siku inayofuata.
Mbali na hilo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limepokea taarifa kutoka serikalini, ikieleza kwamba, mara baada ya kufanyika kwa sherehe za Uhuru Desemba 9, mwaka huu, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam utakuwa tayari kuchezewa ligi kuu.
Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura, alisema ratiba hiyo imezingatia mechi mbalimbali za timu za taifa, hususan katika mzunguko wa kwanza.
"Mzunguko wa kwanza utaanza Agosti 20, mwaka huu kwa kupigwa michezo mitano, ambapo Villa Squad itacheza ugenini dhidi ya Toto African ya Mwanza, Coastal Union ya Tanga itaikaribisha Mtibwa Sugar ya Morogoro na Kagera Sugar itaialika Ruvu Shooting," alisema Wambura na kuongeza;
"Pia, Polisi Dodoma itaumana na African Lyon nyumbani kwao, na Azam FC itacheza na Moro United katika uwanja wao mpya uliopo Chamazi na kwamba, Simba na Yanga zitacheza siku inayofuata," alisema.
Alisema Simba itakuwa ugenini Arusha kucheza na JKT Oljoro, wakati Yanga wakianzia uwanja wao waliouchagua wa Taifa kuumana na JKT Ruvu, michezo hiyo itakamilisha michezo ya kwanza ambayo mzunguko huo utamalizika Novemba 5, mwaka huu.
Akizungumzia kuhusu ratiba hiyo na mechi za timu za taifa, alisema katika mzunguko wa kwanza, michezo kwa timu za taifa haibani ratiba hiyo, hivyo hakutakuwa na mwingiliano wowote na mechi hizo.
Alisema katika mzunguko wa pili, kuna mechi za kuwania kucheza Kombe la Dunia, ambayo mpaka sasa hawajui kama wataanzia nyumbani au ugenini dhidi ya Chad, na mechi ya kuwania kucheza Mataifa ya Afrika dhidi ya Morocco, hivyo inawezekana ratiba ikabadilika.
Mbali na hilo, pia alizungumzia maendeleo ya Uwanja wa Uhuru ambao ulifungwa kwa ajili ya matengenzo, ambapo alisema wamepokea taarifa kutoka serikalini ikiwaeleza kwamba, baada ya Desemba 9, uwanja huo utakuwa umekamilika.
"Nina imani baadhi ya timu ambazo zilikuwa zimeathirika kutokana na uwanja huo kufungwa, zitarudi kuutumia uwanja huo, hususan zile zilizoomba kuchezea Chamazi, kitu ambacho kitakuwa kimerahisisha mambo mengi," alisema Wambura.
No comments:
Post a Comment