03 August 2011

TFF kuongeza wanne All Africa Games

Na Zahoro Mlanzi


SIKU moja baada ya serikali kutangaza michezo itakayoshiriki Mataifa ya Afrika pamoja na idadi ya wachezaji wanaotakiwa kwenda na timu zao, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), litawagharamia wachezaji wanne zaidi, wa timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars), tofauti na ile iliyoangazwa na serikali.


Kwa mujibu wa taarifa ya serikali iliyotolewa juzi, ilieleza kwamba, timu hiyo imepewa nafasi ya kulipiwa wachezaji 20 na kuviagiza vyama kama vina uwezo, viongeze idadi ya wachezaji wanaotaka.

Mbali na soka, michezo mingine itakayokwenda mjini Maputo, Msumbiji kuanzia Septemba 3, mwaka huu ni, ngumi, judo, riadha, netiboli na michezo ya walemavu (PARALIMPIKI).

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura, alisema wanatarajia kuikabidhi timu hiyo kwa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Agosti 5, mwaka huu, iendelee na maandalizi, kwani kamati hiyo ndiyo inayohusika kwa sasa.

"Kabla ya kuikabidhi katika idadi yao ya wachezaji wanayoitaka, TFF tumeona ni bora tukaongeza wanne ili angalau wafikie wachezaji 19 au 20, kwani hayo si mashindano ya siku moja," alisema Wambura na kuongeza;

"Tutawagharamia wachezaji hao, kama unavyojua katika msafara wa watu 20 unaotakiwa na serikali, kutakuwepo na viongozi wengine, sasa ukiwatoa hao wachezaji, watabaki wachache na kama unavyojua kuna suala la majeruhi," alisema.

Alisema timu hiyo ilianza kambi na kwamba kuna wachezaji wengine kutoka Mkoa wa Ruvuma walitarajiwa kuwasili jana tayari kwa maandalizi ya mashindano hayo.

Akizungumzia suala la Kocha Mkuu wa timu hiyo, Charles Mkwassa kuitumikia timu hiyo na Ruvu Shooting, alisema tayari wamekubaliana na kocha huyo kwamba, atakapoondoka na timu hiyo, awasilishe programu kwa Ruvu ili msaidizi wake katika timu hiyo, aifuate.

No comments:

Post a Comment