LONDON,Uingereza
MWANAMUME na kijana raia wa Uingereza jana walifikishwa katika Mahakama moja mjini Birminghman wakikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya wanaume watatu waliogongwa
na magari wakati wakikilinda kitongoji chao dhidi ya waporaji.
Habari kutoka nchini humo zilieleza kuwa washukiwa ni wa kwanza kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria kwa vifo vilivyotokea wakati wa maandamano mabaya kuwahi kushuhudiwa nchini Uingereza katika kipindi cha miongo kadhaa.
Awali polisi walisema wamepata magari mawili katika uchunguzi wao na kupata vidhibiti 400 na taarifa zaidi ya 70 za mashahidi.
Bw.Haroon Jahan,(20), Bw.Shazad Ali (30), na kaka yake Bw.Abdul Musavir,(31) waliuawa Jumatano iliyopita kwenye lango la kituo cha mafuta kilichopo kwenye kitongoji cha Winson Green mjini Birmingham.
Baba yake Bw.Jahan, Bw.Tariq, amepongezwa kwa mwito wake wa kuwataka watu wasilipize kisasi kifo cha mwanawe.
Polisi wamekiri mwito wake huo umesaidia kutuliza hisia za watu, huku kukiwa na wasiwasi kuhusiana na uhusiano kati ya jamii za Burmingham.
Mbali na vifo vya watu watatu vilivyotokea mjini Birmingham, watu wengine wawili walikufa katika wimbi hilo la machafuko yaliyoanza mjini London Jumamosi wiki iliyopita na kuenea katika miji mingine mikubwa ya Uingereza.(BBC).
No comments:
Post a Comment