18 August 2011

Wanyange Miss Tanzania kuwania taji la Photogenic

Na Mwali Ibrahim

WANYANGE 30 wanaowania taji la Vodacom Miss Tanzania 2011, leo watapanda jukwaani kumsaka mrembo bora katika picha 'Vodacom Miss Photogenic' kwenye
ukumbi wa Corridor Spring Hotel mjini Arusha.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka mkoani Arusha,  Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino International Agency, waandaji wa mashindano ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga, alisema kila kitu wamekamilisha ikiwa pamoja na majaji watakaomchagua mrembo mwenye kuonekana vizuri kwenye picha.

"Majaji wana kazi kubwa ya kumpata mshindi kesho (leo),   lakini tunaamini wataifanya kazi yao vizuri na kutuletea mshindi," alisema Lundenga.

Mbali ya mashindano hayo, warembo hao pia watashindana kuwania taji la vipaji, Mrembo bora wa michezo na mrembo mchangamfu, mwenye ushirikiano na nidhamu bora (Miss Personality), kabla ya kuingia katika fainali za mashindano hayo Septemba 10, mwaka huu.

Mashindano hayo yamepangwa kufanyika katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, kwa kuwapandisha jukwaani wanyange 15 walioshinda mataji mbalimbali.

Alisema  tayari mwakilishi kutoka Kanda ya Temeke, Mwajabu Juma, alikata tiketi ya kuingia fainali ya mashindano hayo baada ya kutwaa taji la Miss Top Model lililofanyika mwanzoni mwa kambi yao katika Hoteli ya Girrafe.

Warembo hao wapo mkoani Arusha katika ziara ya kujifunza mambo mbalimbali ya kijamii na utalii katika mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Morogoro.

Lundenga alisema lengo lingine la ziara hiyo ni kuhamasisha utalii wa ndani.

No comments:

Post a Comment