Jovither Kaijage, Ukerewe
KITUO cha Sheria za Haki za Binadamu (LHRC) kimeshauri ufanyike utafiti wa mila kandamizi dhidi ya wanawake hasa ile ya kutakasa wajane na hatua za kuondokana
nazo zichukuliwe.
Hayo yalisemwa na mmoja wa wanasheria wa kituo LHRC, Bi. Felista Mauya, wakati wa semina ya siku tano
ya wasaidizi wa sheria vijiji wapatao 30 yaliyoanza mjini hapa jana.
Alisema licha ya mabadiliko makubwa ya kijamii yanayoendelea kutokea nchini, lakini kuna baadhi ya mila na desturi zinazotakiwa kufanyiwa utafiti na kupata mbinu ya kuzikabili.
Bi, Mauya alisema baadhi ya mila kandamizi kwa wakazi wa Ukerewe ni utakasaji wa wajane.
Akichangia mada hiyo, Bw. Israel Manyama,alisema mila hiyo ya kutakasa wajane inaendelea kushamiri katika Kisiwa cha Ukara.
Wajati huo huo imeshauriwa sheria ya ndoa ya mwaka 1971 na ile ya mirathi ya mwaka 1963 zifanyiwa mabadiliko haraka iwezekanavyo ili kupunguza vitendo vya ukiukaji wa haki za wanawake na watoto.
Wakichangia mada ya haki za wanawake ukatili wa kijinsia, baadhi ya washiriki walisema sheria hizo zimepitwa na wakati na ni chanzo cha ukatili ndani ya jamii.
Walitoa mfano wakisema kuwa sheria ya ndoa ya mwaka
1971 inamyima matunzo mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa. Sheria hiyo inaelekeza kuwa mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa, awe anapatiwa matunzo ya sh. 100 kwa kila mwezi na baba yake.
Kwa upande wa sheria ya mirathi ya mwaka 1963, walisema inamnyima mwanamke haki ya kurithi mali.
Akizungumzia hilo Bi. Mauya alisema shirika hilo likishirikiana na wadau wengine wanaotetea haki za binadamu kuishinikiza serikali kuzifanyia mabadiliko sheria hizo.
No comments:
Post a Comment