18 August 2011

TFF yazibadilikia Yanga, Simba

Na Addolph Bruno

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limesema litazijadili kauli mbovu zilizotolewa na viongozi wa klabu za Simba na Yanga wakati  zikielekea katika mechi ya Ngao ya Jamii iliyofanyika jana katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kauli hizo zilitolewa na uongozi wa Yanga za kugomea mechi kama hawatalipwa na deni lao la sh. milioni 18.6 walizopata katika michuano ya Kombe la Kagame.

Alisema kwa upande wa Simba, watajadiliwa kauli ya uongozi wao baada ya kutoa tamko kuwa, kama TFF isingemruhusu mchezaji wao wa kimataifa kutoka Afrika ya Kati, Gervas Kago, kucheza mechi ya jana,  wasingepeleka timu uwanjani.

Osiah alisema shirikisho hilo limezichukulia kwa uzito kauli hizo na kuweza kudhibiti mizizi inayochipua ambayo ingeweza kukua na kusambaa.

Alisema kauli hizo zimeonesha mfano mbaya kwa klabu nyingine, ikizingatiwa kuwa, wakati ambao wadhamini wameanza kujitokeza kununua mechi.

Mechi ya Simba na Yanga imenunuliwa na Kampuni ya Mafuta ya Big Bon ya jijini Dar es Salaam.

"TFF tumesikitishwa sana na kauli ya viongozi wa Yanga na Simba, hazilingani na matendo yao, matokeo yake tunawakimbiza watanzania ambao wanatuunga mkono, jambo hili hatutaliacha likipita hivi hivi," alisema.

Oseah aliongeza "Stekeholders (wanahisa) wanapanga mambo mengi katika kipindi kama hiki, hasa katika soka, sasa wanaposikia kauli kama hizi,  zinawachanganya katika kuwekeza, lazima klabu hizi ziwajibishwe."

Alisema Sekterarieti ya Shirikisho hilo italizungumzia suala hilo katika moja ya vikao vyake vitakavyofanyika hivi karibuni na kulipeleka kwenye Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho hilo ili kulitolea hukumu, ikiwa watabainika kutenda makosa hayo.

Alisema kauli hizo zitajadiliwa kwani zinalenga kuharibu sura ya shirikishio hilo.

No comments:

Post a Comment