29 August 2011

Wananchi wamepoteza imani na CCM-Msekwa

*Atoa ushahidi kudhibitisha suala hilo
*Azungumzia viongozi kutochukua hatua

Benjamin Mesese na Rachel Balama

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bw. Pius Mseka, amekiri wananchi kupoteza imani na chama hicho, kutokana na
matukio mbalimbali yanayojitokeza, huku viongozi wa chama na serikali wakishindwa kuchukuliwa hatua.

Pia alisema kutokana na hali hiyo, ndio maana katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010, CCM ilipata ushindi wa asilimia 61 ikilinganishwa na asilimia 82 ambazo chama hicho kilipata mwaka 1995.

Bw. Msekwa, alitoa kauli hiyo jana wakati akuhojiwa na kituo cha televisheni cha Star Tv katika kipindi cha Medani za Siasa na Uchumi.

Alisema chama tawala kinapaswa kutambua kuwa kina wajibu wa kutimiza majikumu yake sasa, kwani inapofika mahala chama kikasahau wajibu wake wananchi wana haki ya kutokukichagua.

"Ili chama kichaguliwe ni lazima kioneshe kwa vitendo nia  na malengo ya kutimiza wajibu kwa wananchi, ili waweze kukiamni," alisema.

Bw. Msekwa alisema kiongozi yoyote anayeficha  ukweli kwamba wananchi wamepoteza imani na CCM, mtu huyo hayuko makini na hatakiwi kuendelea kuwa mwanachama.

Alisema kuwa kutokana na mambo yanavyoendelea  na viongozi wa serikali kushindwa kuchukua hatua ni chanzo cha wananchi kupoteza imani na chama.

Aliongeza kwa kutambua hilo, ndio maana chama kimekuja na dhana ya kujifua gamba kwa kuwataka wanaotuhumiwa kukipotezea mwelekeo chama hicho, wajiondoe wenyewe.

Hata hivyo alijigamba kwamba vyama vya upinzani kama Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) kilipata wabunge wengi bungeni kutokana na wanachama wa CCM waliokuwa wanagombea ubunge kuachwa katika kura za maoni na kukimbili upinzani.

"Ni kweli kabisa kuna baadhi ya makosa tulifanya kwa kuwapitisha wagombea wasiokubalika kwa wananchi na wale waliokubalika tuliwaacha na wao kuhamia CHADEMA na ndio hao wameshinda," alisema Bw.Pius.

Alisema vya upinzani havikuwa na uwezo wa kuwashawaishi wananchi ili wavichague, bali ilitokana na nguvu ya CCM kwa kuwa wananchi walikuwa na imani na CCM na ndio maana walichaguliwa kupitia mgongo wa CCM.

Aliongeza kuwa  CCM iliwaacha watu hao waliokimbilia  vyama vya upinzani kwa kuwa CCM ilikwishawabaini kwamba si watu wema ndani ya chama.

Bw. Msekwa alisema si  jambo jema kwa wananchi kuelekeza matatizo yote yanayotokea hivi sasa kwa chama cha mapinduzi japo kinashika dola.

Alisema kiwango cha uadilifu kwa  watendaji kwa sasa kimepungua tofauti na zamani, kwa kuwa zamani kulikuwa na chama kimoja na watendaji pia walikuwa waaminifu sana tofauti na sasa.

"Zamani uadilifu ulikuwa mkubwa kwa watendaji kwa kuwa kulikuwa na mfumo wa chama kimoja na wanachama wote macho yao yalikuwa yakilinda uadilifu tofauti na sasa", alisema.

Alisema watu wanaotakiwa kujivua gamba wapo kwenye ngazi zote.

Akizungumzia suala la makundi ndani ya chama, alisema hali hiyo inatokea wakati wa kura za maoni, ambapo majungu yanaanzia hapo na siri nyingi kuvuja na hatimaye wale walioachwa kuanzisha makundi na kuwashawishi wanachama kutowapigia kura waliopitishwa.

Alisema wanapaswa kukaa chini na kutafuta njia za kuondoa makundi ndani ya chama. "Changamoto si  kuyafumbia macho kwa kuwa yasipofanyiwa kazi yatapeleka chama pabaya," alisema.

Alisema katika uchaguzi uliopita, kuna makosa ya utendaji yalifanyika ambayo yaliwaudhi wananchi na kusababisha kutochagua viongozi waliopitishwa na chama.

"Kuna makosa ya utendaji yalitokea kwa kugawa kadi pasipo kufuata utaratibu na baada ya uchaguzi wanachama walinyimwa fursa," alisema Bw. Msekwa.

Kuhusu hali ya uendehsaji wa bunge wakati wa kipindi chake,  alisema bunge lilikuwa machachari na makini na si kitu kigeni kwake kwa haya yanayotokea katika bunge la sasa kwa kuwa kipindi chake wananchi hawakuwa na mwamko wa kusikiliza.

Alifafanua kuwa wakati huo mwamko  ulikuwa mdogo na hakukuwa na matatizo  ambayo yanajitokeza kama sasa.

"Enzi zangu bunge lilikuwa machachari kwa kuwa kulikuwa na wapinzani kama kina Stephen  Wassira ambaye hivi sasa yupo CCM na  Mabere Marando (CHADEMA) ambao wote walikuwa NCCR-Mageuzi", alisema Bw. Msekwa.

Alisema kuwa  katika bunge la sasa changamoto zipo, lakini utendaji na utatuzi wa matatizo kwa wakati ndio tatizo na kusababisha kuonekana kwamba kuna changamoto ukizingatia hivi wananchi wana mwamko wa kisiasa.

Kuhusu uchaguzi mdogo wa Igunga, alisema kuwa CCM itashinda.

13 comments:

  1. Kwa nini watu wamekosa imani na CCM? Jibu ni rahisi viongozi wa CCM mmewasahau wananchi na kuwakumbatia matajiri na wazungu. JK aliwahi kusema kuwa atakuwa rafiki wa matajiri. Matokeo yake tumeyaona ni kuhujumu uchumi wa nchi hadi kufikia hatua Kamati Kuu ya CCM kuidhinisha malipo ya bilioni 90 kwa kampuni ya Rostam Aziz. Ni mwananchi gani atakubali kuendelea kuona upuuzi huu unafanywa na viongozi wa chama halafu aendelee kuipenda CCM? CCM iwe na uongozi mpya wa kitaifa. Mwenyekiti atoke. Tuanzie hapo bwana Msekwa. La sivyo CHADEMA inachukua 2015.

    ReplyDelete
  2. Mimi sio tu siipendi CCM. Hata rangi ya kijani imebidi niichukie kwa vile kila nikiiona inanikumbusha upupu wa CCM.
    Bw. Msekwa mshauri huyo mwenyekiti wako aanze kufanya kazi na kama hawezi atoke. Ama sivyo 2015 jitayarisheni kuwa wapinzani.

    ReplyDelete
  3. CCM ndo iko mbioni kufa. Mpaka sasa imedhihirisha kuwa uongozi wa juu wa CCM na Serikali hauna uwezo wa kufanya maamuzi na kusimamia serikali na ndio maana Hata mambo haya yanayotokea Viongozi wake wamekuwa kimya kabisa. Lakini labda mimi nimuulize Ndugu Msekwa kazi yake katika Chama ni nini ikiwa tunaona Chama kinashindwa kutekeleza majukumu yake kwa wananchi? Je, yeye si ndio msaidizi wa mwenyekiti hawezi kumshauri? Haya sasa naona mwisho wa CCM ndo uko ukingoni maana alikuwa Gaddaf akitamba sana lakini pamoja na tambo zake kajificha kusikojulikana. Hivyo tambo zenu CCM wakati hatuoni chochote zinatukera sisi wananchi na hatuwachagui tena 2015.

    ReplyDelete
  4. VIONGOZI WA CCM KUANZIA NGAZI YA JUU HADI CHINI HAWAWAJIBIKI KWANI HAWAITISHI MIKUTANO YA HADHARA YA WANANCHI ILI KUELEZA KITU GANI KINAENDELEA HAPA NCHINI. WAKUMBUKE KIMYA KIKUU KINA MSHINDO MKUBWA!!

    MSEKWA UKIWA MAKAMU MWENYEKITI ONYESHA NJIA ILI WENGINE WAFUATE, USILAUMU TU.

    ReplyDelete
  5. kuhusu hali ngumu ya maisha msekwa anasema watu wasiilaumu serikali, nami namuuliza ni nani anayeendesha uchumi wa nchi na nani yuko ikulu na anatoka chama gani? ni nani alihaidi kuwa akiingia madarakani atatua matatizo na kero za wananchi? NI CCM NA NDIO WANAOPASWA KULAUMIWA KWA KUSHINDWA KUTIMIZA AHADI ZAO.

    ReplyDelete
  6. Hivi CCM mlikuwa hamjui kwamba tumepoteza imani na nyinyi.. CCM ni wezi wakubwa wa mali za nchi hii.. badala ya kuchukua hatu eti manacheka cheka tuu kweli nchi hii haina viongozi na sasa tumeshawashtukia tukishindwa kuwatoa tutamfuata fisadi mmoja mmoja kwa wakati wake na kumfundisha adabu kama tunavyowapa kibano vibaka na nyinyi kama serikali imewashindwa then tutawapa mambo wezi wakubwa nyini..

    ReplyDelete
  7. ccm wezi wa kura hata hiyo 61% ilisukwa mezani na wapigakura kuandaliwa kupitia SYNOVATE ili waridhie dhuluma dhidi yao..........

    ReplyDelete
  8. Tangu pale siri ilipovuja kuwa Richmond, kuchota pesa za EPA bila huruma kupitia mikononi mwa watendaji wakuu wa serikali hii ya CCM. Majibu mepesi ya viongozi hao hao, watendaji wa ngazi zilibaki wakaelewa kuwa mtu ye yote anayepata fursa anachota kiasi kingi cha fedha anavyoweza maana usemi ni huu "je nani yu mwema katika Tanzania?" Hakuna mtu atakayeshughulikia. Vyombo vyote vya dola kila kiongozi anajiuliza kumbe mimi nimezubaa wakati wengine wanavuna nchi hii. Akipata fursa anamega kiasi anachoweza kubeba. Watendaji walikuwa wa kwanza kusuka ili CCM iweze kushinda kumbuka yale ya Karagwe, ya Arusha je. CCM inalipa fadhila kwa watendaji wa ngazi za Halmashauri imefikia hali ambayo CCM haiwezi kuwagusa.CCM< haina ubavu wanaulizwa kuwa kama si watendaji CCM ingeweza kushinda? CCM sasa ni mzigo kwa wananchi wa kawaida.
    Polisi wameanza kubambikiza watu kesi huko Arusha ili kupunguza makali bila shaka CCM ijiandae kununua mabomu ya kutosha kutoa machozi kwenye uchaguzi ujao.

    ReplyDelete
  9. Hakuna cha mambomu kwani mbona gadafi alikuwa nayo na ametoka.. halafu hapa kwetu ni rahisi tuu yani nina uhakika tukilianzisha polisi na wanajeshi wote watatuunga mkono kwani hata wenyewe wamechoka mbaya ila issue ni nani wa kumfunga paka kengele..

    ReplyDelete
  10. Ukifahamu kuwa unashindwa au umeshindwa heri kuwa na wazo jipya ya uboreshaji wa hali iliyozorota. Chama kimekufa, sera kimefilisika, utupu uko kila mahali wanaleta mabavu katika kuendesha serikali. Wananchi wamechoka, watakacho amua miaka ijayo waliopo madarakani watafikishwa kwenye vyombo maalumu bila kujali umri wao.

    ReplyDelete
  11. Msekwa heri umekuwa muwazi, maana
    viongozi wengine wabishi wanapingana na ukweli kama Nape vile

    ReplyDelete
  12. CCM WAMEGANDA AKILI, WANAPINDISHA UKWELI, LAANA YA BABA WA TAIFA INAWAANDAMA. WAMETAFUNA NCHI IMEBAKI MIFUPA,NYAMA WAMEJAZA MATUMBO YAO, MASIKINI WAMESAULIKA NA HAWASIKILIZWI.KIAMA CHAO KINAKUJA MUDA SI MREFU.

    ReplyDelete
  13. jamani kwa kweli tumechoka na upuuzi mnaofanya utafikiri unaongoza wanyama

    ReplyDelete