29 August 2011

Tanzania yakiri Gaddafi kuangushwa

*Bendera ya waasi yapandishwa 'Dar'
Bendera ya waasi ikipepea katika Ubalozi wa Libya nchini uliopo jijini Dar es salaam jana. Kushoto ni waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe akitoa ufafanuzi kuhusu msimamo wa Tanzania na kuanguka kwa utawala wa Kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi.

 Na Charles  Lucas

TANZANIA imekiri utawala wa kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, kuangushwa huku ubalozi wa nchi hiyo nchini, ukipandisha bendera ya waasi.Kuangushwa
kwa utawala wa Kanali Gaddafi, kumethibitishwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

"Kimsingi utawala wa miongo minne wa kiongozi wa Libya Kanali Ghaddafi umeanguka kutokana waasi hao wanasaidiwa na mataifa ya magharibi kuteka na kudhibiti miji mingi ukiwemo Mji Mkuu wa Tripoli," alisema Bw. Membe na kuongeza kuwa mapigano bado yanaendelea ndani ya nchi hiyo.

Alisema Tanzania na Umoja wa Afrika (AU) zinasisitiza mazungumzo ya amani ili kufikia makubaliano. Aliongeza kuwa Tanzania  imekuwa ikifanya hivyo kutafuta suluhu la   migogoro mingi kwenye nchi nyingi za Afrika.

Alisema mgogoro wa Libya una sura ya koo mbalimbali kupingana, hivyo si rahisi kuutambua utawala wa waasi ambao bado haujawa na mfumo unaoeleweka.

"Unapozungumzia serikali si kikundi kinasimama na kusema ni utawala, hapana serikali ni lazima iwe mfumo unaokubalika wa Mahakama, Bunge na Utawala,  sisi tunataka wafikie hapo kwa faida ya Walibya," alisema Bw. Membe.

Alisema pamoja na nchi nyingi kutambua Baraza la Waasi, Tanzania haitafanya hivyo hadi hapo taratibu muhimu zitakapofuatwa kwa manufaa ya pande zote zinazohusika katika mgogoro huo.

Aliongeza kuwa awali AU ilionya hatua ya kuwaunga mkono waasi, lakini Balaza Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kudhibiti matumizi ya anga ya Libya, kwa nia ya kulinda usalama wa raia dhidi ya mashambulizi ya vikosi vya serikali, lakini baadhi ya mataifa ya magharibi yalitafsiri vibaya azimio hilo, kwa kutumia nafasi hiyo kushambulia utawala uliopo madarakani.

Alipoulizwa kuhusu hatua ya ubalozi wa Libya nchini kupandisha bendera ya waasi, Bw. Membe alisema Libya kama nchi ina haki ya kufanya jambo ndani ya ubalozi, bila kuathiri uhusiano wa kimataifa.

Alisema sehemu ile (ubalozini) kwa mujibu wa sheria za kimataifa ni ardhi ya nchi nyingine na kuwataka Walibya waliopo nchini kuwa watulivu katika kipindi hiki.

Bw. Membe pia alizungumzia tatizo  la njaa kwenye nchi ya Somaria na kuelezea kuwa ni janga la kutisha linalohitaji msaada wa haraka.

Alisema Tanzania inashiriki  kuhakikisha msaada wa chakula unapelekwa haraka kuokoa maisha ya binadamu.Alisema Tanzania itatoa kiasi cha dola za Marekani 200,000 kusaidia wananchi wa nchi hiyo.

Alisema ili kuunga mkono juhudi za jumuiya za kimataifa za kuokoa maisha ya Wasomaria wanaokufa kwa njaa, Tanzania imetoa msaada wa tani 300 za chakula na pia itauza kwa bei ndogo chakula cha akiba tani 11,000 kwa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) ili kisaidie kunusuru watu zaidi ya milioni 12 wanaokabiliwa na njaa.

9 comments:

  1. Waganda nao wafuate mkondo! ving'ang'anizi wote out soon! Kwani ni Museveni au Mugabe tu! peke yao ndio perfect kuongoza nchi? Na wananchi wake hawana akili kuendelea kuwapigia kura watu kama hao

    ReplyDelete
  2. Haya yaja kwa CCM muda si mrefu kama Mwenyekiti wake ataendelea kuwa mwoga wa kupambana na rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma pamoja viongozi kujitajirisha. Ukoo wa viongozi wa CCM nao ukoo kama mwengine katika maeneo ya nchi za kiafrika yenye misukosuko. Ukoo huu wa CCM sawa koo za Libya na Somalia una tabia chafu za kurithishana vyeo na kupeana nafasi kirafiki au kishikaji. Matokeo yake ni kuiweka nchi njia panda. Yetu macho. CCM imekeosa haiba kama ukoo wa Mubaraka na Ghaddafi. Kazi kwako Mwenyekiti Jakaya Mrisho Kikwete.

    ReplyDelete
  3. Huyu Membe ni MZANDIKI, anakubali kwamba utawala wa Gaddafi umeangushwa, wakati huo akataa kuwatambua waasi waliomuangusha Gaddaffi wakati wanapeperusha bendera yao ktk ubalozi wao DSM. Huu ni undumila kuwili sijui utawafikisha wapi CCM?!

    Acheni unafiki get real Gaddafi is the past history najua bado humuamini lakini kibunga kinasongea, hata kama utajishaua!

    ReplyDelete
  4. haieleweki membe anaposema hautambui uongozi wa waasi na huku tayari wamepandisha bendera katika balozi zao. Hivi ni nani aliyepandisha bendera katika ubalozi wa Libya nchini?

    ReplyDelete
  5. Hata mimi nashindwa kumwelewa sasa kama bendera ya waasi imepandishwa si ina maana wamewakubali waasi.. kwa hiyo tuseme kama ubalozi wa Libya wakipandisha bendera ya Alqaida ubalozini kwao serikali itakaa kimya hawa jamaa zetu sijui vipi.. haya mliobobea kwenye mambo ya uhusioano wa kimataifa mtufafanulie hapo..

    ReplyDelete
  6. Serikali yote imefulia. Ni kweli ubalozi ni nchi nyingine kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Lakini ni nchi nyingine inayotambuliwa serikali ya nchi husika uliko ubalozi huo. Ndio maana kila balozi lazima apeleke hati ya utambulisho kwa mkuu wa nchi ili kujitambulisha kuwa awakilisha nchi fulani. Sasa hawa waasi wametuma lini hiyo kwa JK na wamejitmbulisha lini kwake? Kama bado na kwa kuwa serikali haiwatambi iweje leo wapeperushe bendera yao pale ubalozini? Membe hacha kujikanyaga. Huo ni woga wa kutamka kwa sababu mnaogopa kuwakera wakubwa zenu wa NATO. Mnaogopa wasiwafungie misaada. Penye haki simama na useme ukweli. Kemea. Kosoa. Sahihisha. Yote haya yamewashinda. Hatujawasikia mkisema lolote. Unafiki mtupu.

    ReplyDelete
  7. Nimesoma kwenye Michuzi eti ndiyo sasa hivi Membe amaeamka usingizini na kumwita balozi wa libya kueleza kwa nini wamebadilisha bendera.. hawa viongozi wetu naona wanatumia uti wa mgongo kufikiri na wala sio akili zao. Masaa machache yaliyopita membe amwatangazia watanzania na dunia kupitia waandishi wa habari kwamba ubalozi una haki ya kufanya wanachokitaka ubalozini kwao halafu sasa namwita tena balozi kumhoji.. hawa si ndio viongozi lege lege wanaounda serikali legelege?

    ReplyDelete
  8. Utawla legelege huongozwa na viongozi legelege hivyo siyo rahisi kutoa maamuzi magumu na kuchukua msimamo wake. Haya yamedhihirishwa na serikali ya tanzania na viongozi wake kama Kikwete, Membe na wenzake. Aibu kubwa Membe kaonyesha kwa watanzania.

    ReplyDelete
  9. Nivizuri viongozi wa juu kabla ya kutangaza jambo lolote watafakali na kuchambua,Membe amekurupuka katika kujibu swala la Ribya kupandisha bendera yao Ubalozini Tanzania.

    ReplyDelete