25 August 2011

'Wanachama COTWU jitokezeni kuwania uongozi'

Na Grace Michael

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Uchukuzi Tanzania (COTWU-T), Bw. Mathias Mjema, amewataka wanachama wa chama hicho kujitokeza
kwa wingi kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Septemba mwaka huu.

Nafasi zinazogombewa ni pamoja na Mwenyekiti Taifa, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Mweka Hazina na Wajumbe wa Mkutano Mkuu na Baraza Kuu ambao wamemaliza muda wao kama katiba ya chama hicho inavyosema.

Bw. Mjema alitoa rai hiyo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na Majira juu ya mchakato wa uchaguzi ambao kwa mujibu wa katiba yao, unatakiwa kufanyika kila baada ya miaka mitano.

“Nawaomba wanachama wajitokeze kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali ili wafanyakazi wapate wawakilishi wazuri wa kulinda maslahi yao.

“Pamoja na muda tulioweka kumalizika, nimeamua kuuongeza ili wagombea wapate nafasi ya kujaza fomu,” alisema Bw. Mjema.

Nafasi zinazowaniwa katika ujumbe ni sekta ya mawasiliano kwa njia ya simu za mezani, mkononi, tovuti, barua pepe, faksi, mawasiliano kwa njia ya barua na vifurushi, televisheni, radio, magazeti, upakuaji na upakiaji mizigo bandarini, usafirishaji mizigo kwa njia ya barabara, huduma ya abiria na mizigo katika viwanja vya ndege.

Sekta zingine ni usafirishaji wa abiria kwa njia ya anga, bahari, maziwa, usafirishaji mafuta kwa njia ya bomba, barabara, uwakala wa kupokea, kutunza na kukabidhi mizigo, usajili na usimamizi wa vyombo vya mawasiliano, usafirishaji wakimbizi, abiria na watalii kwa njia ya barabara.

Akizungumzia mafanikio yaliyofikiwa katika uongozi wake, Bw. Mjema alisema ni pamoja na kuongeza matawi ya wafanyakazi kutoka 88 hadi 105 ambayo ni hai, ongezeko la mikataba ya hali bora kazini kutoka mikataba minne hadi 33 na idadi ya wanachama kutoka 5,000 hadi 11,000.

Alivitaka vyombo vya habari kuona umuhimu wa kuwa na wawakilishi hasa katika uwakilishi wa magazeti, nafasi ambayo imekuwa ikibaki wazi na kukosa uwakilishi ndani ya Baraza Kuu.

No comments:

Post a Comment