25 August 2011

Meya awapa siku moja watendaji Kinondoni

Na Anneth Kagenda

MSTAHIKI Meya wa Halmashauri ya Kinondoni Yusuph Mwenda, ametoa siku moja kwa wakandarasi na wahasibu kukaa na kujibu tuhuma zinazowakabili za kukabidhi gofu
la ghorofa la vyumba vya madarasa nane Kimara King'ongo.

Wengine ni wajumbe wa bodi, wahasibu, mkandarasi wa jengo hilo, diwani, wahandisi pia atakuwepo Naibu Meya Bw. Songoro Mnyonge kufanya kikao hicho na kukitolea maamuzi ya papo kwa papo ikiwa ni pamoja na kuelezea madarasa hewa yaliyokabidhiwa yanayodaiwa kuwa thamani yake ni sh. milioni 24.

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Bodi ya Shule kufanya mkutano na waandishi wa habari na kueleza tuhuma za ufisadi unaodaiwa kufanywa na halmashauri hiyo ambapo ilisema kuwa imekabidhiwa gofu hilo, madarasa mawili hewa na kumlipa mkandarasi wakati hajakamilisha majengo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, baada ya kufanya ziara ya kushtukiza shuleni hapo Meya  Mwenda alisema kuwa kinachohitajika haraka iwezekanavyo ni watu hao kukaa na kuzungumza ni kitu gani kilichosababisha kuwapo utata huo na kutoa majibu ya papo kwa papo kwenye kikao hicho.

"Ninawaagiza kujua utatuzi wa tatizo hili na muamue ujenzi wa majengo mengine yote usitishwe badala yake ghorofa lijengwe na likamilike lakini pia tupate taarifa juu ya madarasa mawili hewa,” alisema.

Juzi Bodi ilikaa na  kushutumu kwa kukabidhi magofu ya madarasa ambayo ni jengo la ghorofa nane ambayo hayajakamilika ujenzi wake.
Ilidai kuwa halmashauri hiyo hiyo imekula sh. milioni 151 pamoja na kukabidhi vyumba hewa vya madarasa mawili ambayo yanadhamani ya sh. milioni 24.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bw. Thomas Haule, alisema kuwa kitendo kilichofanywa na halmashauri hiyo ni cha  udhalilishaji na kusema hata pale wanapofuatwa huwa wanakosa majibu ya kueleweka.

"Jengo la ghorofa la madarasa nane lilianza ujenzi mwaka 2007, nyaraka zinaonyesha mkandarasi alipewa kujenga kwa sh. milioni 160, ripoti zinaonyesha kuwa jengo hili lilikamilika mwaka 2010 na kati ya hizo tayari sh. milioni 151 zililipwa lakini sisi hata huyo mkandarasi hatumjui hata bango hana,” alisema.

No comments:

Post a Comment