*Waamua kuunda Tume kufanya uchunguzi mwingine
*Wamshukia Luhanjo, wakidai kuwa wamedharauliwa
*Jairo naye atangaza kumsamehe Pinda, Shelukindo
Na Waandishi wetu, Dar, Dodoma
UAMUZI uliotangazwa na serikali wa kumrejesha kazini Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. David Jairo,umepingwa vikali na
wabunge huku wakisema imeonesha dharau kwa chombo hicho.
Moto wa kupinga kurejeshwa kazini Bw. Jairo uliibuliwa Bungeni mjini Dodoma jana na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe (CHADEMA) baada ya kuwasilisha hoja binafsi kwa kuzingatia kanuni ya 51 (3)ambayo inampa mbunge nafasi ya kutoa hoja bila kufuata utaratibu wa taarifa nyingine.
Baada ya kuruhusiwa na Spika, mbunge huyo alisema; " Leo (jana) wote tumesikia taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, juu ya suala la Bw. David Jairo, ambapo katika taarifa ile Bw. Philemon Luanjo, amemrudisha katibu huyo kazini."
Aliongeza kuwa; "Kwa kuwa suala la kusimamishwa kazi kwa Jairo ni hoja iliyoibuliwa hapa bungeni,kabla ya maamuzi hayo bunge lilipaswa kushirikishwa, lakini katibu kiongozi hakufanya hivyo, bali alitumia fursa ya kuonana na waandishi wa habari moja kwa moja kutoa taarifa, hii ni dharau kubwa kwa bunge."
Mara baada ya Bw.Zitto kutoa hoja bungeni, alisema taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za serikali (CAG) ipelekwe bungeni ili ijadiliwe kwa kuwa dharau hizo zinaonesha mwingiliano wa madaraka kati ya mhimili mmoja wa dola na mwingine.
Bw. Zitto alisema lengo la kuwasilisha hoja yake ni kwa sababu hivi karibuni Mbunge wa Kilindi Bi. Beatrice Shelukindo (CCM) alisema bungeni na kuwasilisha barua yake ya kueleza namna, Bw. Jairo alivyoelekeza taasisi zilizo chini ya wizara kuchangia fedha za kufanikisha bajeti hiyo.
"Jambo lile lilionekana kuvuta hisia kubwa na hata wakati ule ilifikia hatua Waziri Mkuu akasema kuwa yeye angekuwa na madaraka angeweza kumchukulia hatua Katibu Mkuu huyo, lakini kwa kuwa mwenye uwezo ni Rais, hawezi kufanya hivyo," alisema na kuongeza.
"Jambo hili lilianzia bungeni na bunge lilipaswa kupewa taarifa ya CAG baada ya uchunguzi kukamilika, lakini kitendo cha Luhanjo kutoa taarifa kwa vyombo vya habari bila kufuata tararibu za Bunge ni kudharau," alisema Bw. Zitto.
Alisema kuwa kitendo hicho kimeonesha dharau kwa waziri mkuu, hivyo angepaswa kujiuzulu mara moja ikiwa ni pamoja na kuingilia hadhi, kinga na madaraka ya Bunge na kusema kuwa Bunge linapaswa kujadili hoja hiyo chini ya kifungu 63 (2) cha katiba.
Baada ya kutoa hiyo kuonekana ina uzito,Bunge kupitia Kamati ya Uongozi,Maadili na Madaraka ya Bunge lilikaa chini ya Spika Bi. Anne Makinda na Naibu Spika Bw. Job Ndugai na kuijadili taarifa hiyo kwa kina, ili ipatiwe mwafaka.
Baada ya kamati hiyo kukutana ilifikia muafa wa kuuda Kamati Teule ya Bunge ya kuchunguza suala hilo, ikiwa ni pamoja na kukagua taarifa ya CAG na kumhoji Bw. Jairo mwenyewe.
Alisema kuwa hoja iliyotolewa bungeni hapo ni ya kutaka Bunge lisitishe kuendelea na kuhoji taarifa yeyote ya serikali hadi hapo taarifa ya CAG itakapotolewa mara baada ya kukaa na kamati chini ya spika wamefikia maamuzi ya kuunda kamati hiyo teule.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uratibu na Bunge)Bw. Willium Lukuvi alisema jambo hilo limegusa hisia za wabunge wengi, hivyo kupitia kifungu cha kanuni za bunge namba 55 cha haki na madaraka ya bunge, mtoa hoja alitakiwa awasilishe jambo hilo mapema ili liweze kutolewa maamuzi.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM)Bi. Zaynabu Vullu, alisimama na kuomba mwongozo wa spika kama suala hilo linaweza kurudishwa bungeni ili lijadiliwe.
Baada ya kusikiliza hoja zote, Bw. Ndugai alisema kabla ya kuahirishwa kwa bunge hilo, Spika ataunda tume huru ya kuchunguza jambo hilo, majibu yake yatatolewa katika Bunge la tano la kipindi kijacho.
JAIRO AZUNGUMZA
Wakati Bunge likiamua kuuda tume, jijini Dar es Salaam Bw. Jairo, alizungumza na gazeti hili ofisini kwake na kujibu mapigo ya wabunge hao. Aliwataka wabunge hao kuisoma ripoti ya CAG kwa umakini ili wajiridhishe.
"Ni lazima wabunge wakubali kuheshimu vyombo vyenye mamlaka ambavyo wao wanaviamini katika maamuzi ya kitaifa, kama watashindwa kuamini ripoti ya CAG na PCCB katika hili, basi kutakuwa na mtu ana maslahi yake mengine anayo yataka,"alisema Bw. Jairo.
Alisema mtu wa kawaida akituhumiwa bungeni hapewi nafasi ya kujitetea, lakini kama kamati itaundwa nafasi hiyo itatolewa kwa kuhojiwa na kupitia vielelezo mbalimbali na kanuni kama zinavyotaka.
Bw. Jairo kwa siku ya jana alionekana mwenye furaha, huku akisema alituhumiwa na muhimili mwingine na yeye yuko chini ya muhimili mwingine ambao una mamlaka halali za kufanyia kazi suala hilo na zimefanikiwa kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria. "Sasa kama imefanyika hivyo watu wanaongea nini?"Alihoji Bw. Jairo na kuongeza.
"Tuhuma zilikuwa za pesa na mamlaka inayoshughulika na pesa ni CAG, sasa kwa nini watu wanapata kigugumizi katika suala hili wakati mamlaka hii imefanya uchunguzi makini na wa kitalaamu zaidi hivyo naamini nilichokifanya ni kile ambacho niliagizwa na mwajiri wangu,"alisema Bw. Jairo.
Alisema serikali imejiridhisha kuwa anafaa kutenda kazi kwa nafasi hiyo, hivyo Bunge lizingatie taratibu na mipaka ya mihimili mingine hasa taratibu za serikali.
Alitangaza kutoa msamaha kwa wale wote waliomkejeli wakati wa sakata hilo tangu lilipoibuliwa bungeni na Mbunge wa Kilindi, Bi. Beatrice Shelukindo, huku Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, akisema kama angekuwa na mamlaka angemfukuza kazi.
KAULI ZA UPINZANI
Dkt. Sengondo Mvungi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliambia majira kuwa Bw. Luhanjo hakuwa na madaraka ya kutolea ufafanuzi tuhuma za Bw. Jairo.
Alisema majibu hayo yalitakiwa kutolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Edward Hoseah na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP), Elieza Feleshi. "Suala hilo, lingekwenda kwa DPP na Bw. Hoseah, wakiona hakuna kosa kutokana na upelekezi uliofanywa ndiyo warudishe bungeni kutoa maamuzi, simwelewi Bw. Luhanjo kubariki watu wasiobarikiwa" alisema Dkt. Mvungi.
Hata hivyo alisema hashangai kuona watanzania walivyo mahiri wa kuchakachua mambo. "Kitu cheupe kinabadilishwa kuwa cheusi na cheusi kunabadilishwa kuwa cheupe,lakini ukweli unabaki pale kuwa hoja za wabunge zimethibitika kuwa kuna kosa la jinai limetendeka," alisema.
Profesa Abdallah Safari alisema anashangazwa kuona mwingiliano wa madaraka kati ya maamuzi ya bunge na Katibu Mkuu Kiongozi, Bw. Luhanjo kumfutia tuhuma za kutaka kutoa rushwa na kurejesha kazini Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Jairo. "Haya yanayotokea ni aibu kwa Watanzania" alisema Profesa Safari.
Mwenyekiti wa APPT Maendeleo Bw. Peter Mziray alisema masuala hayo yanawachanganya Watanzania kwa sababu yanamdhalilisha Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda ambaye anaaminiwa na Watanzania kuwa ni kiongozi shupavu.
Sasa ndiyo hatuna imani tena na SERIKALI hii. Na kama BUNGE litashindwa kulisimamia jambo hili kidete, pia tutapoteza imani nalo. Hivi ni kweli huyu mkaguzi mkuu wa serikali amekagua na kutoa ripoti safi. Je inamaana wizara hii ilitenga pesa bajeti iliyopita kwaajili ya kufanikisha bajeti ya mwaka huu. Hizo pesa (zetu walipa kodi), zilijadiliwa wapi kwa kazi hiyo, maana hatujawahi sikia kitu hicho bungeni.
ReplyDeletePia tumepoteza imani kabisa na TAKUKURU pamoja na USALAMA wa taifa. Hivi hadi jambo lilipofikia, mlishindwa kuliweka mikononi kwenu na kulishughulikia kikamilifu, ama mlimwachia Katibu mkuu kiongozi Luhanjo awasaidie.
Kweli jambo hili lililo wazi limedhalilisha sana bunge letu pamoja na waziri mkuu. Je hayo yaliyojificha si ndiyo mabaya zaidiii????
Hizi ni fitna vs umwamba! chokochoko ya fitna ilipelekwa Bungeni na walioukosa Uwaziri, na huku ikulu kuna Umwamba! Rais kakaa kimyaaa!! anaelekeza tu nyuma ya pazia! Pinda naye anaropokwa tu bila kujua msimamo wa bosi wake, mwishoe ndio maana anadhalilika! Kitu cheo bwana hakina mchezo
ReplyDeleteKwa kweli Tanzania sasa ilipofika inaelekea shimoni, maana nchi imekaa kama haina Rais. Tumekuwa kama vifaranga vya kuku mama yao kafa watoto hawana mwelekeo, wanawindwa na kunguru. Watu wamelewa madaraka na kujichukulia maamuzi bila ya kuwa na mawasiliano na vyombo vinavyohusika. Hii inaonyesha jinsi gani nchi imepoteza mwelekeo kila mmoja ni mkubwa zaidi ya mwenziye. Hakuna mawasiliano kati ya uongozi na uongozi.
ReplyDeleteHima wabunge msimame imara ili kuikomboa nchi hii. Maana katika swala hili la Jairo kunaonekana kuna kitu kimejificha.
Laiti Mwl. Nyerere angeweza kurudi leo hii angelia kwa uchungu. Maana tumeachwa yatima.
kweli kabisa nchi yetu imepoteza mwelekeo.sina imani na serikali hii tena na wabunge wamedhalilishwa. mambo kama haya yanaweza kuvuruga amani nchi yetu.naomba wabunge wahakikishe Jairo anafukuzwa kazi rasmi.haiwezekani hata kidogo sis sio wajinga
ReplyDeleteHuu ni ulegevu wa Rais. Ameshindwa kazi!!
ReplyDeleteuhuru wa mihimili mitatu uko wapi? ni maandishi tu hakuna lolote. kanuni na taratibu zote za bunge ni sheria. haya sasa tuone nani amfunge paka kengere...
ReplyDeletehizi ndio sera za "Chukua Chako Mapema". ndugu kikikupitia na wewe chukua, ujiandae na yanayofuata punde. muda wa tanzania yenye amani umefika ukingoni
ReplyDeleteHuu ndio uongozi bora kwa wananchi wa Tanzania kutoka kwa kikwete.bado subini mtaona mengine mengi tu yanakuja.Na hili ndio litakuwa fundisho kwa wananchi.
ReplyDelete