26 August 2011

Kanumba awakumbuka watoto yatima

Na Mwandishi Wetu

MWIGIZAJI wa filamu nchini, Steven Kanumba 'Kanumba' jana ametoa msaada kwa watoto yatima wanaolelewa katika kituo cha CHAKUWAMA kilichopo
Sinza, Dar es Salaam.

Kanumba alitoa msaada huo kwa kushirikiana na Kampuni ya Usambazaji wa filamu nchini ya Steps Entertainment ambao ni mchele, sukari, sabuni na nguo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, wakati wa kukabidhi msaada huo, Kanumba alisema ameona ni jambo la busara wakati wa sikukuu ya Idd el Fitri kusheherekea pamoja na watoto hao japo kwa kuwapa msaada huo, ili nao wajisikie kwamba kuna watu wanawajali.

"Sifanyi kwa ajili ya promosheni eti kwa kuwa nakaribia kuachia filamu yangu mpya, lakini kama mngejua historia yangu, mngejua nini namaanisha lakini pia napenda watoto ndiyo maana hata katika baadhi ya filamu zangu nimeigiza na watoto kama filamu ya Uncle JJ," alisema Kanumba.

Kwa upande wake Ofisa Habari wa Steps, Sales Mapunda alisema kwa kutambua umuhimu wa watoto katika filamu, watafanya mchakato wa kutafuta watoto wenye vipaji vya kuigiza katika kituo hicho na kuwashirikisha kwenye filamu wanzotarajia kuziandaa hivi karibuni.

Naye Katibu Mtendaji wa CHAKUWAMA, Hassan Khamis alisema kituo hicho kina jumla ya watoto 80, kuanzia mwaka mmoja hadi 18 ambapo wamefurahishwa na msaada huo kwani wanaimani watasheherekea sikukuu kwa furaha kama watoto wengine.

"Watoto wakiwa wanasaidiwa kama hivi, wanakuwa wanajisikia faraja mno kwani wanajihisi ni miongoni mwa jamii, hivyo tunashukuru sana," alisema Khamisi.

No comments:

Post a Comment