RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, jana aliongoza mazishi ya marehemu Mussa Khamis Silima, Mwakilishi wa Jimbo la Uzini na
Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania.
Katika mazishi hayo yaliyofanyika kijini kwao marehemu Kiboje Mwembeshauri Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dkt. Mohamed Kharib Bilal.
Viongozi wengine waliohudhuria ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, Spika wa Baraza la Wawakilishi Bw. Pandu Ameir Kificho, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bi. Anna Makinda, Waziri Mkuu wa zamani Bw. Edward Lowassa, wabunge, wawakilishi, mawaziri wa serikali zote mbili pamoja na viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wengine na mamia ya wananchi.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Bw. Vuai Ali Vuai ambaye alitoa salamu kwa niaba ya CCM, na viongozi wake wote akiwemo Mwenyekiti wa Chama hicho Jakaya Kikwete. Bw. Pandu Ameir Kificho alitoa salamu za pole kwa niaba ya Baraza la Wawakilishi.
Wengine ni mwakilishi wa Wabunge wa Zanzibar Bw. Hamad Rashid, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni Bw. Freema Mbowe, Bw. Simba Chaweni ambaye alitoa
salamu za pole kwa niaba ya Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Aidha, Mhe. Willium Lukuvi alitoa salamu za pole kwa niaba ya Waziri Mkuu na Bw. Mohamed Aboud alitoa salamu za pole kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Nao wanafafamilia walitoa shukurani kwa viongozi wote waliohudhuria katika mazishi hayo pamoja na kutoa shukurani kwa msaada mkubwa walioupata katika msiba huo wa Bw. Silima tokea alipokuwa hospitalini hadi kufariki kwake.
Kifo cha Marehemu Mussa Ame Silima kilitokea Jumanne wiki hii katika Hospitali ya Muhimbili mjini Dar-es-Salaam alipokuwa akitibiwa baada ya kupata
ajali ya gari. Alipata ajali juzi ambapo mke wake Bi. Mwanakheir Fadhil alifariki hapo hapo kwenye ajali hiyo.
No comments:
Post a Comment