TRIPOLI, Libya
WAASI wanaompinga kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi wameteka makazi ya kiongozi huyo huku moshi pamoja na milio ya risasi na mizinga ikisikika
katika viunga vya Jiji la Tripoli.
Shambulio hilo limetokea muda mfupi baada ya mtoto wa kiongozi huyo aitwaye Bw.Saif al-Islam, kujitokeza hadharani na kutangaza kwamba hajakamatwa.
Usiku mzima, mtoto wa Kanali Gaddafi, Bw.Saif al-Islam alionekana hadharani, ikipingana na ripoti kuwa alikuwa amekamatwa.
Bw.Saif al-Islam, ambaye awali waasi walidai kuwa wamemkamata, alijitokeza katika hoteli moja inayoshikiliwa na wafuasi wa Kanali Gaddafi.
Mapema milio ya risasi na milipuko imekuwa ikisikika karibu na hotel inayotumiwa na vikosi vya serikali pamoja na eneo la makazi ya kiongozi wa Libya ya Bab al-Aziziya.
Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC,Bw. Matthew Price alizungumza na Bw.Saif al-islam na kusema kuwa anaonekana kuwa mchangamfu na shauku kuu.
Katika mahojiano hayo na BBC Bw. Saif al-Islam alisema waasi wameingia kwenye mtego mjini Tripoli na kwamba wanajeshi wanaomuunga mkono Kanali Gaddafi walikuwa wamevunja uti wa mgogo wa waasi hao'
Habari nyingine zinasema waasi wanaopigana kuudhibiti mji mkuu wa Libya, Tripoli , wamerudishwa nyuma na wanajeshi wanaomuunga mkono Kanali Muammar Gaddafi.
Lakini wakati mapigano yanapoendelea katika maeneo mbalimbali ya mji, msafara wa waasi kutoka Mashariki mwa nchi ulirudishwa nyuma.
Jumapili iliyopita waasi walidai kuwa walikuwa wamemkamata Bw.Saif al-Islam, pamoja na familia yake. Waasi hao walioingia mjini Tripoli Jumamosi iliyopita walikaribishwa watu waliokuwa wakisheherekea katika bustani ya Green Square wakati walipowasili siku ya Jumapili.
Waasi hao walisema kuwa wameweka vizuizi katika sehemu mbalimbali za mji lakini wanakabiliwa na upinzani mkali katika baadhi ya maeneo.
Kiongozi wa Baraza la Mpito la kitaifa (NTC), Bw. Mustafa Abdel Jalil, alisema wakati wa ushindi halisi utakuwa pale watakapomkamata Kanali Gaddafi.
Rais Barrack Obama amewapongeza watu wa Libya kwa kile alichokitaja kama kujitolea mhanga kusipokuwa kwa kawaida huku akisema kuwa watu wa Libya wanakaribia kupata kile wanachohitaji.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Bw. Ban Ki-Moon naye amewakumbusha wanachama wa Umoja huo kuwa, wanajukumu la kuheshimu mahakama ya kimataifa ya jinai, ambayo imetoa hati za kuwakamata Kanali Gaddafi, mtoto wake wa kiume Bw.Saif al Islam na mkuu wake wa idara ya ujasusi.
Hata hivyo baadhi ya viongozi wa waasi wanasema afadhali wafunguliwe mashtaka nchini Libya na sio katika mahakama ya kimataifa ya ICC, mjini The Hague.(BBC)
Pole sana Gadafi,waafrika wote tunakuombea,ww ni kiongoz Jasir,big up
ReplyDelete