30 August 2011

Viongozi Afrika wakubaliana kushirikiana usafiri wa anga

Rais Jakaya Kikwete akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Usafiri wa Anga jijini Dar es Salaam jana.

Na Benjamin Masese

WAKUU wa Nchi za Afrika wamekubaliana kushirikiana kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga kwa kuongeza vivutio vya watalii ili kuondokana na
utegemezi wa mataifa makubwa.

Wakati wakuu hao wakiazimia hilo, Tanzania imeweka bayana kuwa haina uwezo wa kukunua ndege mpya kutokana na changamoto zinazoikabili.

Muafaka wa mataifa hayo kushirikiana ulifikiwa Dar es salaam jana katika mkutano uliofunguliwa na Rais Jakaya Kikwete na kuhudhuriwa na viongozi wa nchi za Afrika zikiwemo za Botswana, Namibia, Nigeria, Kenya, Burundi, Rwanda, Ghana, Tanzania, Afrika Kusini.

Akifungua mkutano huo, Rais Kikwete alisema Tanzania inakabiliwa na changamoto nyingi katika suala la usafiri wa anga, kutokana na miundombinu kuwa mibovu, mabadiliko ya hali ya hewa, uchumi, uhaba wa watalaam, ukosefu wa watalii na mambo mengine madogo madogo.

Rais Kikwete alisema imekuwa ni bahati na wakati muafaka mkutano mkuu wa 17 wa nchi za Afrika kufanyika Tanzania kwa  lengo la kujadili jinsi ya kuboresha usafiri wa anga namna ya kuimarisha uwekezaji wa ndani kupitia ushirikiano wa viongozi.

Alisema mbali ya Tanzania kuwa na rasilimali nyingi, lakini bado inakabiliwa na changamoto ambazo zinahitaji ushirikiano wa karibu ili kuondokana na hali iliyopo.

Alisema nchi za Afrika zinakosa mapato  makubwa kutokana na mioundombinu ya anga kuwa mibovu.Pia alisema kukosa wawekeza husababisha ndege za mataifa tajiri kushindwa kufanya nao biashara kwa kuwa mazingira ya viwanja hayaridhishi.

"Nchi za Afrika bado zinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na hali ya hewa, watalaamu tulionao wachache, tuliowasomesha ndiyo wanaokimbilia mataifa makubwa kwa sababu ya mishahara minono pia uwekezaji wa ndani kama ujenzi wa viwanja vya kisasa unahitaji fedha nyingi, istoshe hivi sasa Tanzania hatuna uwezo wa kununua ndege mpya...hatuwezi kupambana na Emirates, hivyo lazima tuunganishe nguvu pamoja,"alisema.

Rais Kikwete alisema Tanzania inakosa watalii wengi kutokana kutozwa bei kubwa, hivyo kusababisha wageni kwenda nchi nyingine zilizopo karibu na kuongeza kwamba asilimia kubwa ya wawekezaji wanaokuja nchini hupenda kuomba zabuni ya ujenzi wa barabara.

Aliwataka viongozi hao kuweka mikakati dhabiti ya ushirikiano ili kuimarisha uchumi wa nchi kupitia usafiri wa anga na kuondokana na utegemezi wa matifa makubwa.

Naye Waziri wa Uchukuzi Bw. Omari Nundu, alisema mpango wa sasa uliopo ni kubadilisha bodi na menejimenti ya usafiri wa anga iliyopo na kuweka watu wanaostahili wenye uwezo wa kufanya kazi ya ushirikiano na nchi za Afrika katika kukabiliana na changamoto zinazoikabilia sekta ya anga.

Bw. Nundu alisema mbali ya kubadilisha menejimenti hiyo, wataweka mkazo wa kubadilisha majengo na matengenezo ya viwanja na kutoa mwanya kwa mashirika yenye uwezo wa kuendeleza na kuongeza ufanisi wa usafiri wa anga.

Alisema serikali ipo katika mkakati wa kukarabati ndege mbili, ambazo tayari zimetengewa fedha.

Bw. Nundu alisema katika mkutano huo na viongozi wa Afrika wamekubaliana kuweka sera pamoja na maofisa wa usafiri wa anga ili kubadilishana uwezo na uzoefu.

Aliongeza kuwa wamefikia kuweka mbali itikadi za siasa na kuamua kujenga umoja wa pamoja wa maendeleo ya kiuchumi ili kukabiliana na changamoto zilizo mbele yao.

1 comment:

  1. Maskini JK wanamburuza kufungua mkutano wakati shirika lake la ndege halina hata ndege moja? That was very embarrassing. Hivi kwa nini washauri wake wasingemshuri angalau ufunguzi ufanywe na Waziri?
    People! Lets stop embarrassing our President!

    ReplyDelete