30 August 2011
Serikali ya Japan yaimwagia Tanzania mabilioni ya fedha
Na Ngaillo Ndatta,Tudarco.
SERIKALI ya Japan imeipatia Tanzania sh. bilioni 39 kwa ajili la kusaidia upanuzi wa daraja la Kimataifa la Rusumo, linalounganisha Tanzania na Rwanda.Pia serikali hiyo
imekubali kuipatia Tanzania sh. bilioni 37 kwa ajili ya upanuzi wa Barabara ya Kilwa kwa lengo la kupunguza foleni ya magari.
Msaada huo ulisainiwa na Waziri wa Fedha Bw. Mustapha Mkulo na Balozi wa Japan nchini hapa Bw.Hiroshi Nakagawa, Dar es Salaam jana na kushuhudiwa na maofisa wengine wa ubalozi wa Japan na Wizara ya Fedha.
Katika hafla hiyo, Bw. Mkulo alisema msaada huo umekuja wakati muafaka kwa kuwa utasaidia kuimarisha miundombinu ambayo ndio nguzo katika kufikia maendeleo, hasa
wakati huu ambao nchi hizo ziko katika Shirikisho la Africa mashariki.
“Hii itasaidia kuondoa hali ngumu ya kiuchumi kwa pande zote mbili za wanachi wa Tanzania na Rwanda, hivyo tutahakikisha fedha hizi zinafanya kazi iliyokusudiwa,”
alisema Bw. Mkulo na kuongeza;
"Kwa sasa daraja la Rusumo lina uwezo wa kupitisha tani 20 hadi 25, lakini mara baada ya kukamilika kwa upanuzi litakuwa na uwezo wa kupitisha tani 60.”
Kwa upande wake Balozi Nakagawa alisema ujenzi wa daraja hilo utasaidia kurahisisha gharama za usafiri kutoka bandari ya Dar es Salaam kupitia Kigali,” alisema.
Wakati huo huo, Japan imeahidi kutoa sh. Bilioni 37 kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa barabara ya Kilwa.
Kukamilika kwa ufumbuzi wa barabara hiyo kutawezesha kupunguza msongamano uliopo jijini Dar es Salaam.
"Mradi huu ni wa Kilomita 1.3 kuanzia Kamata Barabara ya Kilwa ambapo daraja la gerezani litapanuliwa, hivyo kuongeza tija ya usafiri,” alisema.
Balozi huyo alitumia mwanya huo kuishukuru serikali ya Tanzania kwa ushirikiano iliopata katika kipindi alichokuwa nchini. Balozi huyo anatarajia kuondoka nchi kurejea kwao baada ya kumaliza muda wake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment