29 August 2011

Usajili Rocky City Marathon waanza

Na Zahoro Mlanzi

CHAMA cha Riadha Tanzania (RT), kinatoa wito kwa wanariadha mmoja mmoja, Taasisi na Vyama  vya michezo mbalimbali kujisajili na mashindano ya  riadha ya
Rock City Marathon yanayotarajiwa kufanyika Septemba 4, mwaka huu mkoani Mwanza.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa chama hicho, Suleiman Nyambui alisema kuwa mashindano hayo ni nafasi nzuri ya kujiongezea uwezo kwa wanariadha nchini.

Alisema tayari baadhi ya taasisi kama Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Wananchi (JWTZ) pamoja na mikoa 14 imethibitisha kushiriki lakini bado wanaona kuna haja ya kuhamasisha washiriki zaidi katika mashindano hayo.

Nyambui alisema fomu kwa ajili ya usajili zinapatikana katika ofisi za RT Dar es Salaam na ofisi za Capital Plus International ambapo kwa upande wa Mwanza zinapatikana katika ofisi zao.

"Kwetu sisi mashindano ya Rock City ni msaada mkubwa katika kuibua vipaji na nafasi nzuri kwa wanariadha wengine kujijengea uwezo zaidi hivyo tunatoa wito kwa wadau wote kujitokeza kwa wingi kujisajili na mbio hizo," alisema Nyambui.      

Kwa upande wake, Mratibu wa mashindano hayo wa Kampuni ya CPI, Zaituni Ituja  alisema pia fomu za usajili kwenye tovuti yao katika kurahisisha ambapo wahusika watajaza na kuzirudisha kupitia barua pepe.

"Lengo letu ni kupanua wigo wa ushiriki katika shindano la mwaka huu na ndiyo maana tumetoa vyanzo mbalimbali vya upatikanaji wa fomu za usajili", aliseza Zaituni.

Mashindano hayo mwaka huu yanadhaminiwa na Kampuni ya Airtel, Geita Gold Mine, Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), New Africa Hotel, Mfuko wa Pensheni wa Taifa (PPF), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bank M, MOIL, New Mwanza Hotel, Shirika la Hifadhi ya Wanyapori Tanzania (TANAPA) na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

No comments:

Post a Comment