29 August 2011

Wanne ngumi wametangulia All African Games

Na Amina Athumani

MABONDIA Emilian Patrick, Joseph Martin, Seleman Kidunda na Maximilian Patrick wamechaguliwa kuliwakilisha taifa katika michuano ya All African Games na wameondoka jana kwenda Maputo, Msumbiji.

Timu hiyo imewahi kuondoka tofauti na michezo mingine kutokana na kuwahi kupimwa uzito kesho na kupangwa kwa ratiba kwa ajili ya mapambano yao yatakayoanza Septemba Mosi, mwaka huu.

Emilian atakwenda kupambana katika uzito wa kilo 56 (Bantam), Martin kilo 69 (Welter), Kidunda kilo 75 (Middle) na Maximilian kilo 91 za zaidi (Heavy).

Timu hiyo imeondoka jana baada ya ratiba ya mashindano hayo kubadilika ambapo badala ya mashindano hayo kuanza Septemba 3 sasa yataanza Septemba Mosi, mwaka huu kwa upande wa mchezo wa ngumi pekee.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kuangwa kwa timu hiyo kabla ya kwenda uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Makore Mashaga alisema baada ya kupokea mabadiliko ya ratiba wameweza kuwasiliana na serikali haraka ili kufanya mabadiliko ya safari na kuiwahi timu hiyo Msumbiji.

"Kwa kweli tunaishukuru sana serikali kwa kushirikiana na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ambao wamefanya jitihada za haraka hadi kufanikisha timu hii kuondoka leo (jana), vinginevyo tungeondoka Agosti 31, mwaka huu ambapo tungekuwa wasindikizaji kwa kuwa tungekuta ratiba imeshapangwa," alisema Mashaga.

Alisema timu zote zitapimwa uzito kesho na keshokutwa kutachezeshwa droo kwa ajili ya kupanga ratiba katika mtindo wa makundi ambapo mapambano yataaza kuchezwa rasmi Septemba Mosi.

Timu hiyo imeambatana na makocha wao Hurtado Primentel kama Kocha Mkuu na Edward Emanuel kama Kocha Msaidizi.

No comments:

Post a Comment